Dar es Salaam. Vyama vya siasa 12 vimesema ni wakati mwafaka kwa Serikali kurahakisha mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya na maridhiano kama ilivyopendekezwa na Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Vimesema ingawa Katiba mpya sio dai geni, lakini kitendo cha tume hiyo kupendekeza mchakato huo upatikane mwaka 2028 kinapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa ili kuondoa mazonge ya kisiasa nchini na kuweka mustakabali mwema wa Taifa.

Vyama hivyo vya DP, NRA, NLD, AAFP, Ada Tadea, Demokrasia Makini, UPDP,  UDP, Sau, CCK, UMD, TLP, vimetoa kauli hiyo leo Jumapili Aprili 26,2026 wakati wakizungumza na wanahabari kuhusu ripoti ya tume hiyo iliyowasilisha matokeo yake Aprili 23, 2026 mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Mjumbe wa jukwaa hilo linalounganisha vyama 12, Doyo Hassan amesema Katiba mpya imebeba dhana nzima ya mvurugano wa siasa katika Taifa, ndio maana mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Othman Chande aliitaja kama chanzo kimojawapo kilichosababisha ghasia Oktoba 29.

Katika uwasilishaji wa matokeo ya Tume hiyo, Jaji Chande amesema walibaini ghasia zilizotokea siku hiyo na baada yake zilichochewa na changamoto sugu za kijamii na kisiasa zilizojengeka kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi huku akitaja madai ya Katiba mpya kuwa chanzo kimojawapo.

Akizungumzia suala hilo, Doyo aliyekuwa mgombea urais katika uchaguzi huo kwa tiketi ya NLD ameiomba mamlaka kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya.

“Nasema mazonge kwa sababu wenzetu waliposema mabadiliko ya Katiba muhimu, wakakimbia uchaguzi, sisi tukashiriki kwa sababu huwezi kukimbia changamoto za kisiasa,” amesema Doyo.

Doyo amesema upatikanaji wa Katiba mpya hautaondoa mazonge ya kisiasa pekee bali utaliponya Taifa kwa changamoto mbalimbali inazozipitia kwa nyakati tofauti.

“Tunawaambia Watanzania tunakwenda kuliponya Taifa kwa upatikanaji wa Katiba mpya haraka iwezekanavyo na kuunda kwa maridhiano,”amesema.

“Mamlaka ziharakishe utekelezaji wa mapendekezo hayo yanakwenda kuliponya Taifa na nchi kisiasa kuwa amani na utulivu katika chaguzi zijazo,” ameeleza Doyo ambaye ni Katibu Mkuu wa NLD.

Mbali na hilo, Doyo amesema kwa kuwa vile tume imetaja baadhi ya kauli mbiu kuwa zikiwamo za’ Oktoba tunatiki’ na ‘No reforms no election’ wahusika wachukuliwe hatua akisema hakuna haja ya kufanya uchunguzi.

Wataka Baraza Vyama vya siasa liihitishwe

Mwenyekiti wa jukwaa la vyama hivyo, Abdul Mluya ambaye pia aligombe urais katika uchaguzi huo, amesema wanaipongeza tume ya Jaji Chande kwa kazi walioifanya na wanaipokea kwa mikono miwili matokeo ya ripoti walioiwasilisha.

Mwenyekiti Jukwaa la Vyama vya Siasa,Abdul Mluya akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.Picha na Michael Matemanga

“Ukifuatilia hotuba ya Jaji Chande ametaja masuala kadhaa yanayohusu vyama vya siasa, sasa kama tumetajwa ni wakati mwafaka kuhitisha Baraza la Vyama vya Siasa ili tukajidiliane yanayotuhusu kutokana na ripot.

“Huko tutajadiliana, tukakosoana na kuambizana ukweli na kukumbashana kuhusu umuhimu wa vyama kutii sheria ya Sheria za Vyama vya Siasa na sheria nyinginezo,” amesema Mluya.

Aidha, Mluya amesema ni wakati pia mwafaka kwa vyombo ulinzi na usalama kuvifanyia kazi vichocheo vilivyotajwa na tume hiyo na haitaji kuundwa kwa tume nyingine.

“Vyombo vihakikishe vinashughulikia yote yaliyotajwa kwenye ripoti ile na wahusika wote wanawekwa hadharani ili iwe fundisho kwa wengine,” amesema Mluya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *