Dar es Salaam. Rais wa Marekani, Donald Trump amesema mshambuliaji aliyefyatua risasi katika hafla ya Chama cha Waandishi wa Habari wa Ikulu ya Marekani alionekana mtu mwenye sura ya uovu.

Ametoa kauli hiyo baada ya kushirikisha picha na taarifa za mtuhumiwa kupitia mitandao yake ya kijamii.

Mamlaka za usalama zimemtambua mshukiwa huyo kwa jina la Cole Tomas Allen, mkazi wa eneo la Los Angeles mwenye umri wa takriban miaka 31. Taarifa za awali zinaonesha alikuwa na bunduki aina ya shotgun, bastola pamoja na visu kadhaa wakati wa tukio hilo.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia leo Jumapili Aprili 26, 2026 katika Jiji la Washington, D.C,  Trump na mkewe Melania Trump walilazimika kusindikizwa haraka nje ya ukumbi wa hafla na maofisa wa usalama wa United States Secret Service baada ya mtu mwenye silaha kufyatua risasi za moto karibu na eneo la ukaguzi wa usalama.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, mshambuliaji huyo alifyatua risasi akimlenga mmoja wa maofisa wa Secret Service, lakini askari huyo alinusurika baada ya kuvalia koti la kuzuia risasi.

Trump alisema askari huyo yuko katika hali nzuri na anaendelea kupatiwa matibabu.

Picha inayoonesha Maofisa wa vyombo vya dola wakimkamata Cole Tomas Allen, mtuhumiwa wa tukio la ufyatuaji risasi katika hafla ya Chama cha Waandishi wa Habari wa Ikulu ya Marekani (White House Correspondents’ Association), jijini Washington, D.C. Marekani.

Akizungumza na waandishi wa habari baadaye Ikulu, Trump amesema mshukiwa huyo alikimbia kwa kasi kuelekea eneo la ukaguzi akiwa na silaha kadhaa kabla ya kuzuiwa na kutiwa mbaroni na maafisa wa usalama.

“Alikuwa umbali wa kama yadi 50, lakini alikuwa anakimbia kwa kasi kubwa. Alionekana kuwa mtu mwenye sura ya uovu,” amesema Trump.

Mkuu wa Polisi wa muda wa Washington, Jeffery Carroll amesema mshukiwa huyo alipelekwa hospitali kwa uchunguzi wa afya ya akili huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo cha shambulio hilo.

Aidha, maofisa wanaamini huenda alitekeleza tukio hilo peke yake bila kushirikiana na kundi lolote.

Katika picha na video zilizosambazwa na Trump kupitia mtandao wake wa Truth Social, mtu mmoja anaonekana akikimbia kwa kasi katika eneo la ukaguzi kabla ya kuzidiwa nguvu na walinzi waliokuwa doria.

Tukio hilo lilizua taharuki kubwa miongoni mwa wageni wapatao 2,600 waliohudhuria hafla hiyo maarufu ya kila mwaka.

Mashuhuda walisema milio ya risasi iliposikika, wageni walianza kupiga kelele na kujificha chini ya meza huku baadhi ya wahudumu wakikimbia kuokoa maisha yao. Maofisa wa usalama waliwaangusha chini baadhi ya viongozi wa juu wa serikali ili kuwakinga na hatari kabla ya kuwaondoa mmoja mmoja nje ya ukumbi.

Hafla hiyo, ambayo hufanyika katika Hoteli ya Washington Hilton, ilisitishwa mara moja kufuatia tukio hilo. Trump amesema angependa hafla hiyo ipangwe upya ndani ya siku 30 zijazo.

Tukio hilo linaongeza orodha ya vitisho vya kiusalama dhidi ya Trump, ambaye tayari aliwahi kulengwa katika majaribio mawili ya kumuua mwaka 2024 wakati wa kampeni zake za uchaguzi.

Uchunguzi zaidi unaendelea huku vyombo vya usalama vikifanya msako nyumbani kwa mshukiwa huyo huko California kubaini iwapo kulikuwa na mipango mingine iliyokuwa ikiandaliwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *