Katika taarifa yake iliyotolewa New York, Marekani Jumamosi usiku na Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric, Katibu Mkuu amelaani vikali vitendo hivyo vya vurugu na kutuma salamu za mshikamano kwa wananchi wa Mali wanaoathiriwa vibaya na hali hiyo.

Nini kimetokea?

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, mashambulizi hayo yalianza takriban saa kumi na mbili asubuhi kwa saa za eneo husika, yakilenga kwa karibu wakati mmoja miji kadhaa ya kaskazini na kusini mwa nchi: Kati, Kidal, Mopti, Gao na Sévaré.

Huko Bamako, uwanja wa ndege wa kimataifa ulilengwa, pamoja na makazi ya Waziri wa Ulinzi, Jenerali Sadio Camara, ambapo nyumba yake inaripotiwa kulengwa kwa shambulio la lori lililokuwa na vilipuzi, na kusababisha vifo. 

Amri ya kutotoka nje kwa saa 72 imetangazwa na Gavana wa mkoa wa Bamako, na mawasiliano yote ya anga yamesitishwa.

Kushambulia miundombinu ya raia ni kinyume cha sheria

Guterres amesisitiza umuhimu wa kulinda raia pamoja na miundombinu ya kiraia, akionya kuwa mashambulizi dhidi ya walengwa wasio na hatia hayawezi kuvumiliwa na yanakiuka misingi ya haki za binadamu na sheria za kimataifa.

Aidha, Katibu Mkuu ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na tishio linaloongezeka la misimamo mikali yenye vurugu na ugaidi katika ukanda wa Sahel. 

“Kuna umuhimu wa kuchukua hatua za pamoja na zilizoratibiwa ili kuzuia kuenea kwa vitendo hivyo pamoja na kushughulikia mahitaji ya haraka ya kibinadamu,” imesema taarifa hiyo ikimnukuu Guterres.

Amesisitiza kuwa ni vema kuimarisha uratibu wa usalama na ushirikiano kati ya nchi za eneo hilo ili kuhakikisha utulivu wa kudumu na ulinzi wa raia.

Kauli ya Mratibu Mkazi wa UN Mali

Mapema Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, ambaye pia ni Mratibu wa Kibinadamu Hanaa Singer-Hamdy amesema kupitia mtandao wa X zamani Twitter, kwamba, “mawazo yetu yako pamoja na raia wote walioathiriwa vibaya, hasa wale ambao tayari wamekumbana na changamoto kubwa na sasa wanakabiliwa tena upya na hali ngumu.”

Amesema  Umoja wa Mataifa unasalia thabiti katika dhamira yake ya kusaidia raia wenye uhitaji na utaendelea kufuatilia kwa karibu kinachoendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *