
Kapteni Ibrahim Traoré, rais wa
muungano wa Mataifa ya Sahel (AES), amelaani
mashambulizi ya kupangwa nchi ya Mali, takribani saa 48 baada ya matukio hayo.
Katika
taarifa iliyotolewa Jumapili usiku, alitaja mashambulizi hayo kama “ya
kinyama na yasiyo ya kibinadamu” na kusema “yanaungwa mkono na maadui
wa mapambano ya ukombozi wa Sahel”.
Traoré
aliongeza kuwa mashambulizi hayawezi “kuyumbisha nia ya watu mashujaa wa
Sahel kuishi kwa uhuru, amani na heshima”. Pia alitoa salamu za rambirambi
kwa walioathirika.
Alisema
mashambulizi hayo yaliyoratibiwa yalipangwa kwa muda mrefu kwa madhumuni ya
kuathiri vikosi vya usalama vya Mali na kuwatia hofu raia.
Kapteni
Traoré alichukua urais wa zamu wa AES mwezi Desemba, akichukua nafasi ya
kiongozi wa kijeshi wa Mali, Jenerali Assimi Goïta.
AES
inayaleta pamoja mataifa ya Mali, Niger na Burkina Faso, ambayo yanaongozwa na serikali za
kijeshi zilizoingia madarakani kufuatia mapinduzi katika miaka ya hivi
karibuni.
Nchi hizo tatu zilijiondoa katika Jumuiya ya kikanda ya Ecowas na
tangu wakati huo zimeimarisha ushirikiano chini ya muungano huo.
Ubia huo
unalenga kuimarisha uratibu wa usalama, kuunganisha rasilimali na kukuza
utangamano wa kiuchumi, ikijumuisha mipango ya miundomsingi ya pamoja, usafiri
huria wa watu, na, kwa muda mrefu, soko la pamoja na sarafu.