Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki mechi 11 kufunga pazia la msimu wa 2025-2026 katika Ligi Kuu Bara, ushindani hauko tu kwa washambuliaji au viungo, bali hata kwa mabeki ambao wamegeuka kuwa nguzo muhimu pande zote mbili za uwanja.

Mbali na jukumu lao la msingi la kulinda lango, mabeki hawa wameongeza thamani kwa timu zao kwa kufunga mabao na kutoa pasi za mwisho, jambo linalowafanya kuwa na mchango mkubwa zaidi katika mafanikio ya timu zao.

Kwa kawaida, beki anatambulika kama mchezaji wa kuzuia, kukaba na kuhakikisha washambuliaji wa timu pinzani hawapati nafasi ya kufunga.

Hata hivyo, soka la kisasa limebadilika kwa kasi, likiwataka mabeki kuwa na uwezo wa kushambulia, kutengeneza nafasi na hata kufunga mabao.

Ndiyo maana katika msimu huu, ushindani wa tuzo ya Beki Bora unazidi kupamba moto, huku takwimu zikianza kuzungumza kwa niaba ya wachezaji wenyewe.

Pamoja na sintofahamu iliyopo kuhusu Tuzo za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa msimu wa 2024-2025 ambazo bado hazijatolewa, hali hiyo haijawazuia wachezaji kuendelea kuonesha ubora wao uwanjani. Kila mmoja anapambana kuhakikisha anajijengea jina na kuweka alama itakayomuweka kwenye rada za tuzo zijazo.

Katika msimu uliopita, Antony Tra Bi wa Singida Black Stars, Dickson Job (Yanga) na Lusajo Mwaikenda (Azam), walitajwa kuwania tuzo hiyo. Hata hivyo, msimu huu umeibua sura mpya na ushindani mpya unaoonyesha wazi kuwa hakuna anayelala.

Kwa upande wa mabao, mabeki watano wamejitokeza kwa ubora wa hali ya juu, kila mmoja akiwa amefunga matatu.

Ibrahim Imoro wa Singida Black Stars ni miongoni mwao, akionesha uwezo mkubwa wa kupanda mbele na kutumia vizuri nafasi anazopata.

Vilevile, Mohamed Hussein wa Yanga, ameendelea kudhihirisha ubora wake, si tu kwa kulinda, bali pia kwa kufunga mabao muhimu kwa mabingwa hao watetezi wa ligi.

Magata Charles wa Mtibwa Sugar naye ameingia kwenye orodha hiyo, akionesha kuwa hata timu zisizo kwenye presha kubwa ya ubingwa zinaweza kuwa na wachezaji bora wenye mchango mkubwa.

Rushine De Reuck wa Simba ni jina lingine linaloonekana kuwa na ushawishi mkubwa katika safu ya ulinzi, huku akifunga pia mabao matatu ukiwa ni msimu wake wa kwanza ndani ya Ligi Kuu Bara.

Chanda Chewe wa TRA United anafunga orodha hiyo, akionesha uimara wake katika pande zote mbili za uwanja, akifunga mabao matatu.

Lakini si mabao pekee yanayowapa mabeki alama ya ziada, kwani asisti pia zimekuwa kipimo muhimu cha ubora wao.

Ibrahim Imoro anaongoza kwa asisti nne, akionesha kuwa si mfungaji tu bali pia ni mtengeneza nafasi mahiri, jumla raia huyu wa Ghana amehusika na mabao saba.

Israel Mwenda wa Yanga naye ana asisti nne, akithibitisha kuwa beki wa pembeni anaweza kuwa silaha kubwa ya kushambulia na amekuwa akitumika kupandisha mashambulizi ya timu hiyo.

Anuar Kilemile wa JKT Tanzania na Baraka Filemon wa Mbeya City, wamechangia asisti tatu kila mmoja, wakionesha uwezo wao wa kusaidia mashambulizi kutoka nyuma.

Takwimu hizi zinaweka wazi kuwa mabeki hawa si wa kawaida, bali ni wachezaji wanaobadilisha taswira ya nafasi yao uwanjani.

Wakati wachezaji hao wakiendelea kuonyesha ubora wao, historia ya tuzo hii inaonesha kuwa kwa muda mrefu imekuwa ikizunguka katika klabu kubwa za Kariakoo, yaani Simba na Yanga.

Kuanzia msimu wa 2020-2021 ambapo Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alitwaa tuzo hiyo akiwa Simba, kisha Henock Inonga Baka msimu wa 2021-2022 akiwa Simba, ni dhahiri ushindani umebaki kwa timu za kariakoo.

Baadaye Dickson Job na Ibrahim Bacca waliinasa tuzo hiyo wakiwa Yanga katika msimu wa 2022-2023 na 2023-2024, hali inayoonyesha ubora wa timu hizo katika kuzalisha mabeki bora.

Hata hivyo, msimu huu unaonekana kuwa na ushindani mpana zaidi, ambapo hata wachezaji kutoka klabu nyingine wanapata nafasi ya kuonekana.

Hii ni dalili nzuri kwa maendeleo ya soka la Tanzania, kwani inaongeza ushindani na kuhamasisha ubora zaidi.

Kadiri msimu unavyoelekea ukingoni, macho yote yatakuwa kwa mabeki hawa kuona nani ataibuka kidedea. Je, wataendeleza utawala wa Kariakoo au tutashuhudia sura mpya ikitwaa tuzo?

Jibu litapatikana mwishoni mwa msimu, lakini kwa sasa kilicho wazi ni kwamba mabeki wamechukua nafasi yao na wanaonesha wazi kuwa nao wana ligi yao.

TAKWIMU ZAO

Ibrahim Imoro (Singida BS- mabao 3, asisti 4)

Mohamed Hussein    (Yanga – mabao 3)

Magata Charles (Mtibwa Sugar – mabao 3)

Rushine De Reuck (Simba – mabao 3)

Chanda Chewe (TRA United – mabao 3)

Israel Mwenda (Yanga – asisti 4)

Anuar Kilemile (JKT Tanzania – asisti 3)

Baraka Filemon (Mbeya City – asisti 3)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *