Ni mara ngapi umesikia kuwa Mchumia juani hulia kivulini? Hii ni methali ya kiswahili yenye maana ya kuwatia moyo watu katika shughuli mbalimbali wanazofanya Kila siku wawe na Imani kuwa ipo siku watayafurahia matunda ya kazi yao.
Methali hii huwapa watu nguvu, bidii, moyo, ujasiri, tumaini na weledi katika kufanya kazi. Hivyo ndivyo golikipa wa Yanga, Hussein Masalanga alivyopambana kujitafuta huku na kule na sasa amejipata huku akionekana kulinda vizuri lango la Wananchi, Yanga.
Masalanga hapa anatoa funzo kubwa kwa wachezaji wengine ambao wana ndoto ya kuja kuzichezea Klabu kubwa hapa nchini ni kwamba wasikate tamaa kwani hakuna mtu anayeijua kesho yake. Nani angemfikiria Masalanga pamoja na umri alionao kupata nafasi ya kujiunga na Yanga ambayo mara nyingi imekuwa ikivutiwa na wachezaji vijana ambao watakaa kikosini kwa muda mrefu.
SAFARI YAKE ILIPOANZIA
Safari ya Masalanga ilianzia katika Klabu ya Ihefu ambayo ilibadilishwa jina na sasa ikitambulika kama Singida Black Stars baadaye alijiunga na Tabora United kisha alirejea tena Singida Black Stars na Januari 18, 2026 alijiunga rasmi na Wananchi, Yanga.
Kipa Hussein Masalanga alipokuwa na kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’. katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025). Picha na Mtandao
AFCON ILIVYOMTANGAZA
Katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2024) yaliyofanyika Desemba 2025 hadi Januari 2026 huko Morocco, Masalanga alikuwa mmoja kati ya magolikipa watatu waliokuwa wameitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’. Hata hivyo, katika magolikipa hao watatu waliokuwa wameitwa kikosini na kocha wa timu hiyo Miguel Gamondi, Masalanga hakupewa nafasi ya kusimama kwenye milingoti mitatu kutokana na kwamba yeye ndio alikuwa chaguo namba tatu la kocha, lakini hisivyokuwa matarajio ya wengi kwa bahati mbaya aliyekuwa kipa namba moja, Yakoub Suleiman kutokea Simba alipata majeraha na kupelekea kupewa nafasi magolikipa wawili waliokuwa wamebakia ambao ni aliyekuwa chaguo la pili, Zuberi Foba wa Azam na Masalanga.
Kipa wa Azam FC, Zuber Foba. Picha na Mtandao
WALIVYOGAWANA MECHI AFCON
Katika mashindano ya AFCON 2024 kule Morocco, Tanzania ilicheza jumla ya mechi nne ambapo tatu zilikuwa za hatua ya makundi na moja ilikuwa ya robo fainali ambapo iliweka historia ya kufika hatua hiyo kwa mara ya kwanza tangu ilipoanza kushiriki mashindano hayo mwaka 1980.
Katika mechi ya kwanza kipa aliyesimama langoni alikuwa ni Foba ambapo Tanzania ilikubali kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Nigeria, kipa huyo wa Azam pia alipewa nafasi ya kucheza katika mchezo uliofuata ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya majirani zetu Uganda.
Hata hivyo, katika mchezo wa mwisho wa kundi C kocha Gamondi alimpa nafasi Masalanga ambaye alisimama vyema langoni Tanzania ilipopata sare nyingine ya bao 1-1 dhidi ya Tunisia na kujihakikishia kufuzu katika hatua ya robo fainali kama timu iliyofanya vizuri kwenye nafasi za tatu za makundi.
Baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mechi dhidi ya Tunisia, kocha Gamondi alimuamini tena kipa huyo na kumpa nafasi nyingine katika mechi ya robo fainali dhidi ya waliokuwa wenyeji wa michuano hiyo Morocco. Katika mtanange huo ambao ulionekana kuwa mgumu kadri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda, Masalanga naye alionyesha ugumu golini kwa kupangua michomo kadhaa ya wapinzani hao.
Ugumu iliokuwa ikiuonesha Stars katika mechi hiyo ulizidi kuwaongezea wenyeji presha kubwa ya kutafuta matokeo ambapo muda mwingi walionekana kulishambulia lango la Tanzania na katika majaribio ya kulitafuta bao yalisababisha safu ya ulinzi ya Stars kufanya makosa na Brahim Diaz ndiye aliyefunga bao la ushindi kwa ustadi baada ya kuwatoka mabeki na kuupiga mpira uliozamia pembeni chini ya lango kumuacha Masalanga bila cha kufanya. Licha ya kuondoshwa kwenye mashindano lakini kipo huyo bado alionyesha uwezo mkubwa.
Kipa Hussein Masalanga wakati akitambulishwa kujiunga na Yanga akitokea Singida Black Stars. Picha na Yanga
WANANCHI WALIVYOMBEBA
Baada ya kuonyesha makali yake huko Morocco, Wananchi Yanga walionyesha nia ya kuhitaji huduma ya kipa huyo na wakafanikiwa kumpeleka Jangwani huku wengi wakiuchukulia kama usajili wa kawaida. Masalanga ambaye anasifika kwa uwezo wa kurusha mpira mbali kwa mikono, vile vile hakupewa na fasi kubwa kwenye kikosi cha kocha Pedro Gonçalves ambacho kina makipa wazoefu kama Djigui Diarra na Abuutwalib Mshary.
Kipa wa Yanga, Hussein Masalanga wakati akirusha mpira katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Pamba Jiji kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba, Mwanza. Picha na Mtandao
ALIVYOWASHANGAZA WANANCHI
Ule Upepo wa AFCON ulimrudia tena Masalanga pale Jangwani wakati safari hii kipa namba moja, Diarra alikuwa katika kifungo cha adhabu ya kutocheza mechi tatu kutokana na utovu wa nidhamu alioonyesha katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar.
Masalanga mwenye umri wa miaka 34 alianza kuitumikia Yanga katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Pamba Jiji ambapo Wananchi waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Mchezo mwingine ni ule wa Kombe la FA ambapo Yanga ilipata ushindi wa bao 1-0 katika Uwanja wa KMC Complex Mwenge, Dar es Salaam.
Aliendelea kuaminiwa na kusimamishwa tena katika mechi nyingine ya Ligi Kuu ambayo Yanga ilipata ushindi mnono wa mabao 6-0 ikiichapa Mbeya City. Masalanga katika mechi zote tatu alizocheza Jangwani hakuruhusu nyavu zake kutikiswa hadi aliporejea Diarra katika mashindano ya Kombe la Muungano huko Visiwani Zanzibar, alikuta lango hilo liko salama.
Ni dhahiri kabisa Masalanga aliifanya kazi nzuri baada ya Diarra kutokuwepo kikosini na alihakikisha pindi alipokuwa langoni Wananchi wasione mapungufu na kumkumbuka kipa namba moja jambo ambalo alifanikiwa. Kipa huyu ambaye alitumia muda wake mwingi kuzitumikia timu za daraja la kati, sasa anafaidi maisha mazuri huko Jangwani kwa Wananchi.