Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini (IRGC) limetangaza kuwa limegundua makombora 15 ya Marekani ambayo hayakulipuka katika jimbo la Hormozgan kusini mwa Iran, na maelfu ya mabomu katika jimbo la kaskazini la Zanjan, chini ya mwezi mmoja baada ya uvamizi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran kusitishwa.

Kikosi cha Imam Sajjad cha IRGC, chenye makao yake makuu katika mji wa Bandar Abbas huko Hormozgan, kimesema katika taarifa ya Jumapili kwamba timu zake za kutegua mabomu zimefanikiwa kuzima makombora mazito zaidi ya 15 ya Marekani katika jimbo hilo.

Taarifa hiyo imesema mengi kati ya makombora hayo yalikuwa ya aina za GBU na BLU na aina nyingine za kisasa, ikiongeza kuwa silaha hizo zimekabidhiwa kwa vitengo vya kiufundi na utafiti vya IRGC kwa ajili ya uhandisi wa kinyume (Reverse Engineering).

Wakati huo huo, Kikosi cha Ansarul-Mahdi cha IRGC, chenye makao yake makuu katika mji wa Zanjan, pia kilitoa taarifa siku ya Jumapili, kikisema kwamba timu zake za kutegea mabomu kimekusanya zaidi ya mabomu 9,500 katika sehemu mbalimbali za mkoa huo.

Taarifa hiyo imesema timu za kutegea mabomu za IRGC huko Zanjan pia ziliharibu au kutenganisha roketi na makombora 55 wakati wa uvamizi wa hivi karibuni wa Marekani na Israel, ikiwa ni pamoja na makombora aina ya GBU-57 bunker buster, yenye uwezo wa kulipua mahandaki ya chini ya ardhi na kukabidhiwa kwa mamlaka husika.

Katika muktadha huo, ripoti na uchambuzi uliochapishwa katika magazeti ya Uingereza na Marekani katika siku za hivi karibuni imefichua mabadiliko ya aina yake katika mzozo kati ya Marekani na Iran.

Ripoti ya tovuti ya Uingereza “iPaper” imewanukuu wachambuzi wa zamani katika Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) wakisema kwamba kuna wasiwasi kwamba Iran imefanikiwa kupata na kuchunguza silaha kisasa za Marekani na Israel ambazo hazikulipuka, au zilizoanguka katika uwanja wa vita.

Wachambuzi wanasena kuwa Tehran kwa sasa inajihusisha na “uhandisi wa kinyume” wa makombora kama vile Tomahawk, drones za Reaper, makombora ya Jassm, na mabomu ya GBU-57 bunker-buster, kwa lengo la kuelewa muundo wake au kutengeneza mbadala wa ndani.

Uhandisi wa Kinyume ni mchakato wa kunakili muundo wa kitu kwa kuchunguza na kupima kipengee kilichopo ili kutengeneza data ya kiufundi inayohitajika ili kunakili na kutengeneza kipengee au bora zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *