MSHAMBULIAJI wa Mashujaa, Jafari Kibaya, amesema ana imani kubwa na Kocha Mkuu, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kuwa atairejesha timu hiyo kwenye ubora wake na kuifanya kuwa ngumu kufungika katika michezo yao ya Ligi Kuu Bara iliyobaki ili kuwa salama.
Julio ambaye ni nyota wa zamani wa CDA, Simba na Taifa Stars, aliwahi pia kuzinoa Simba, Mwadui, Taifa Stars na Coastal Union, hivi sasa amekabidhiwa kikosi cha Mashujaa baada ya klabu hiyo kuachana na Salum Mayanga.
Kibaya aliweka wazi kuwa, tangu kuwasili kwa Julio, kumekuwa na mabadiliko makubwa ndani ya kikosi hicho, hasa upande wa saikolojia ya wachezaji.
“Kocha amefanya kazi kubwa sana kutujenga kisaikolojia, kwa sasa tunaingia uwanjani bila presha yoyote,” amesema Kibaya.
“Hali hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kufanya Mashujaa kuwa timu ngumu kufungika na inayocheza kwa kujiamini zaidi, tunaamini atatuvusha salama.”
Mbali na hilo, mshambuliaji huyo amesema malengo yao kwa sasa ni kuanza kupata ushindi mfululizo ili kujiimarisha zaidi kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.
“Tunahitaji kushinda mara kwa mara ili kuongeza pointi na kupanda juu zaidi kwenye msimamo,” amesema Kibaya mwenye mabao mawili Ligi Kuu Bara msimu huu.
Julio mwenye jukumu la kuhakikisha Mashujaa inamaliza salama msimu huu wa Ligi Kuu Bara ili kuepuka nafasi ya kushuka daraja, alianza kazi ya kukiongoza kikosi hicho Februari 13, 2026, ambapo Mashujaa iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Mpaka sasa, kocha huyo hana rekodi ya kupoteza mechi hata moja tangu atue ndani ya kikosi hicho katika mechi tano, akishinda moja na sare nne. Mashujaa inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, ikiwa imeshinda mechi nne, sare tisa na kupoteza sita, ikifikisha pointi 21.