Bado tupo kwenye mzozo na maofisa wa usafirishaji kutokana na mzozo wa mafuta. Na bado tunaifuatilia kauli ya kupunguza msafara wako kama hatua ya kubana mafuta.

Tunategemea hatua ya pili iwe ni Serikali kuuiga mfano huu kwa vitendo. Kufanya hivyo kutapunguza ununuzi wa mafuta Serikalini kwa kiasi kikubwa. Ni lazima tukubali kuwa misafara ya viongozi na watendaji wa Serikali ni mikubwa sana.

Kama itarekebishwa bila shaka malengo yatatimia. Baada ya hapo, tumulike matumizi ya Serikali kwa ujumla wake. Tume ya uchunguzi wa matukio ya wakati na baada ya uchaguzi imemaliza kazi.

Mambo makubwa iliyoyaona ni kutokushughulikiwa mapema kero za umasikini uliokithiri, ukosefu wa ajira, ubadhirifu na ufisadi kuwa ni baadhi ya sababu zilizotajwa kuwa chanzo cha hasira za wananchi. Na tulisikia ripoti ya CAG ilishatahadharisha juu ya upotevu wa fedha na matumizi makubwa ya Serikali tangu awali.

Katika wakati huu wa mzozo wa Marekani na Iran, tunashuhudia gharama za maisha zikipanda kwa kasi. Waswahili tunasema “njaa inafunza utafutaji,” kwetu shida inageuzwa kuwa fursa.

Ukimwona tajiri anakula kisamvu ujue ni kwa sababu ana nidhamu ya fedha au ya afya.

Lengo la kubana matumizi ya mafuta si la kuwa na akiba pekee, bali kumtayarisha mwananchi wa kawaida kupambana na hali ngumu. Wachina wanasema “usinifundishe kula samaki, bali kuvua samaki.”

Hata sisi tulijifunza hilo kwa kurekebisha mtalaa wa elimu, ile ya ufundi imeboreshwa. Mwanafunzi sasa anaweza kupata elimu itakayomwezesha kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa.

Badala ya kuzunguka na vyeti akisaka ajira isiyokuwapo, sasa anaweza kujiajiri na kutegemea mafunzo ya ufundi aliyopata shuleni au chuoni. Hili linatarajiwa kupunguza au kufuta sehemu ya kero za ukosefu wa ajira na umasikini uliokithiri.

Ndugu zetu Wachina walifanikiwa humo, lakini pia wakajiongeza katika kushughulika na viongozi wabadhirifu na mafisadi.

Walikuwa wakitoa adhabu kali sana kwa viongozi wasio waaminifu, hadi kufikia adhabu ya kunyonga mpaka kuua. Tunaweza kusema hii ndiyo sababu iliyowawezesha kuishi katika ujamaa wenye tija. Wameweza kuithibitishia dunia kuwa ujamaa si umasikini, pengine ni mfumo bora wa maisha zaidi ya ubepari.

Si lazima kuiga hukumu zao kama zilivyotolewa. Lakini tukiweza kuzifanyia kazi taarifa za wananchi na vyombo vya uchunguzi, tukawawajibisha wale wote wanaotajwa kufanya ufisadi na ubadhirifu. Tutakuwa tumepiga hatua kubwa katika kuelekea kulimaliza tatizo hilo. Kulikalia kimya kunaongeza hasira za wananchi na kusababisha yale yaliyotokea Oktoba mwaka jana kuwa sehemu ya maisha yetu.

Hapo awali, Waziri Mkuu aliwahi kukemea maisha ya mazoea. Kuna utaratibu wa Taasisi za Serikali kutumiana kalenda, shajara na hata vifurushi vya zawadi kila msimu. Alitoa mfano wa uchapishaji wa kalenda na shajara za zawadi. Akasema kwa ulimwengu wa sasa wa digitali, mtu anaweza kuwasha kiswaswadu na kujua tarehe ya siku husika. Pia anaweza kuhifadhi kumbukumbu zake kidigitali bila gharama yoyote.

Kutumia mamilioni ya shilingi kila mwaka kwa uchapishaji wa zawadi hizo ni ufujaji wa fedha za Serikali. Ulimwengu wa sasa ni wa kidigitali, kila mmoja ana kalenda na shajara katika simu yake. Na simu hizi ndizo hutumika kwa wepesi zaidi ya kalamu na makaratasi. Kama yupo anayeona tofauti, na anahitaji kutumia bidhaa za shajara na kalenda, ni bora akazinunue mwenyewe kuliko kuitwika Serikali mzigo usio na tija.

Tuna imani kuwa maagizo ya Waziri Mkuu yatafanyiwa kazi mara moja. Lakini pia Serikali itachukua hatua dhidi ya misururu mirefu ya misafara ya watendaji wa Serikali. Mtu wa kawaida anashtuka akifikiria gharama za gari mojamoja, zidisha kwa idadi ya magari kwenye masafara mmoja, zidisha kwa idadi ya misafara ya viongozi wote. Lakini la pili ni kiwango cha mafuta kinachonywewa na kila gari, zidisha kwa idadi ya magari ya msafara, zidisha kwa misafara yote.

 Mambo haya yanatoa majibu sahihi kuwa Serikali yetu ina matumizi yaliyopita kiasi. Bila shaka tunakubaliana kuwa gharama za magari hayo, na mafuta ya kutosheleza misururu hiyo ni zaidi ya bajeti ya nchi kubwa na tajiri.

Uamuzi wako wa kupambana na matumizi yasiyo ya lazima unapaswa kuzingatiwa na kila idara ya Serikali.

Ni lazima kuamua kuachana na manunuzi ya ziada. Kama tunajua kuwa vizuri vinagharamiwa, tujue pia namna ya kugharamia bila kuumiza watu.

Naomba nisinukuliwe vibaya. Umuhimu wa magari ya aina hiyo ni mkubwa, lakini ukubwa wake usiwe kutofautisha mtu na kiongozi wake.

Tunajua kuwa gari hizi zinamudu kwenye njia korofi, hasa kule vijijini.

Basi yatumike pale tu inapolazimu. Kama inawezekana, yawekwe kwa ajili ya kushughulikia hali ya huko, na viongozi watumie magari yenye unafuu wa matumizi yao mengine hasa wakiwa kwenye miundombinu rafiki.

Tunapodai matengenezo ya miundombinu, tunamaanisha kwa wote. Tutachekesha iwapo magari haya tunayonunua kwa gharama kubwa yakirandaranda mijini wakati yalipaswa kusaidia vijijini ambako miundombinu ni korofi.

Vinginevyo barabara zote zirekebishwe na tuachane kabisa na magari ya gharama kubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *