Dar es Salaam. Wakati dunia ikikabiliwa na mabadiliko makubwa ya kisiasa na kiuchumi yanayochochewa na vita, migogoro ya kimataifa na ushindani wa mataifa makubwa, mjadala wa umoja wa Afrika umeanza kurejea kwa nguvu mpya miongoni mwa viongozi wa bara hilo.

Ni mjadala unaoamsha tena ndoto ya muda mrefu ya Afrika kujenga nguvu ya pamoja kisiasa, kiuchumi na hata kijeshi, ili iweze kujitegemea na kushindana kwa ufanisi katika jukwaa la kimataifa.

Msukumo mpya wa mjadala huo umechochewa na kauli ya Rais wa Kenya, William Ruto, aliyetoa wito wa “kufumua muundo wa Afrika” ili kuendana na kasi ya changamoto za sasa.

Ndoto ya Umoja wa Afrika iliyoasisiwa na wapigania uhuru wa bara hili, akiwamo Kwame Nkrumah na Julius Nyerere, imeanza kufufuka kwa nguvu mpya huku viongozi na wachambuzi wakitafakari chimbuko lake, sababu za kushindwa kwake na uwezekano wa kuijenga upya katika mazingira ya sasa ya dunia.

Akizungumza Aprili 10, 2026 katika kikao cha usalama cha Umoja wa Afrika (AU), Rais Ruto alisema mfumo wa sasa wa taasisi za bara hilo umebeba urasimu mkubwa unaochelewesha uamuzi wa pamoja.

“Afrika inahitaji mfumo wa uamuzi wa haraka na wa pamoja, kwa sababu changamoto za sasa haziheshimu mipaka wala muda wa kusubiri taratibu ndefu za kiutawala,” alisema, akisisitiza umuhimu wa mageuzi ya kina ya taasisi za bara hilo.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kauli hiyo imekuja wakati Afrika ikikabiliwa na changamoto zinazovuka mipaka ya nchi, zikiwamo ugaidi, mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya kisiasa pamoja na ushindani wa kiuchumi kutoka kwa mataifa ya nje.

Hali iliyoongeza uzito wa mjadala huu ni kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyesisitiza umuhimu wa mshikamano wa kitaifa na kikanda, akieleza kuwa mustakabali wa Afrika unahitaji umoja imara unaotokana na utashi wa ndani wa mataifa yake.

Kauli hizi zinaashiria kuibuka kwa fikra mpya kuhusu nafasi ya Afrika katika dunia inayobadilika kwa kasi.

Hata hivyo, wachambuzi wanaeleza kuwa kuelewa mustakabali wa umoja wa Afrika kunahitaji kurejea kwenye chimbuko lake na ndoto iliyozaliwa wakati wa harakati za ukombozi wa bara hilo.

Kwa mujibu wa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo, fikra za kuunganisha Afrika zilijengwa juu ya msingi wa mapambano dhidi ya ukoloni.

Viongozi wa mwanzo walitambua kuwa uhuru wa kisiasa usingekuwa na maana bila umoja wa bara zima.

Anasema wengi wanaozungumzia falsafa ya Nkrumah hawaielewi kwa kina, akibainisha kuwa mwaka 1963 Nkrumah aliandika kitabu kilichokuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘Africa Must Unite’ (Afrika lazima liungane), akisisitiza kuundwa kwa dola moja ya Afrika yenye serikali kuu.

“Huu haukuwa mjadala wa kawaida, ulikuwa mkakati wa ukombozi wa kiuchumi na kisiasa. Nkrumah aliamini bila umoja, Afrika ingeendelea kutawaliwa kwa njia mpya za kiuchumi,” anasema Dk Masabo.

Kwa upande wake, Mwalimu Nyerere aliendeleza mjadala huo kwa mtazamo wa hatua kwa hatua, akipendekeza kuanza na muungano wa kikanda ili kujenga uzoefu kabla ya kufikia umoja wa bara zima.

Katika historia, Nyerere aliwahi kuwa tayari kuchelewesha uhuru wa Tanganyika ili kuunda taifa moja la Afrika Mashariki pamoja na Kenya na Uganda, ingawa wazo hilo halikufanikiwa kutokana na tofauti za kisiasa na ratiba tofauti za kupata uhuru kwa nchi hizo.

Tofauti hizi za kimtazamo kati ya Nkrumah aliyesisitiza umoja wa haraka na Nyerere aliyependelea hatua za taratibu, ndizo zilizochangia kuundwa kwa Jumuiya ya Umoja wa Afrika (OAU) mwaka 1963.

Chombo hicho kililenga kuimarisha mshikamano lakini kikaheshimu mamlaka ya nchi wanachama.

Hata hivyo, OAU ilikosolewa kwa kuwa na uwezo mdogo wa kuingilia masuala ya ndani ya nchi wanachama, jambo lililoifanya ishindwe kukabiliana kikamilifu na migogoro ya kisiasa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoikumba Afrika kwa miongo kadhaa.

Mwaka 2002, kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika (AU) kulionekana kama hatua ya kuboresha OAU, kwa kuongeza ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kiusalama.

AU ilianzisha mifumo mipya kama Baraza la Amani na Usalama pamoja na mipango ya maendeleo ya pamoja.

Hata hivyo, licha ya maboresho hayo, AU imeendelea kukumbwa na changamoto zilezile, ikiwemo ukosefu wa utashi wa kisiasa, utekelezaji hafifu wa uamuzi wa pamoja na utegemezi wa kifedha kutoka kwa wahisani wa nje.

Dk Masabo anasema moja ya sababu kubwa ya kukwama kwa ndoto ya umoja ni viongozi kushindwa kulinda rasilimali za bara na kuendelea kutegemea mifumo ya nje kiuchumi na kisera.

“Tunaendelea kugawanyika kwa misingi ya kikoloni. Leo kuna makundi ya Anglofoni, Frankofoni na Arabofoni ndani ya bara hili. Hali hii inatufanya tushindwe kujiona kama wamoja,” anasema.

Hoja hiyo inaungwa mkono na Dk Zemelak Ayele wa Chuo Kikuu cha Addis Ababa, anayesema Afrika ina msingi imara wa kuungana kutokana na historia na utamaduni unaofanana, lakini tatizo kubwa ni ukosefu wa mshikamano wa kisiasa.

“Taasisi zipo, lakini hazipewi nguvu. Umoja hauwezi kuja bila utashi wa kweli wa kisiasa,” anasema.

Mbali na changamoto za kisiasa, wachambuzi wanaeleza pia kuwapo kwa vikwazo vya kiuchumi vinavyozuia umoja wa Afrika. Bara hili linaendelea kuwa na kiwango kidogo cha biashara ya ndani, huku nchi nyingi zikitegemea zaidi kuuza malighafi nje kuliko kushirikiana kibiashara ndani ya bara.

Takwimu zinaonesha kuwa biashara ya ndani ya Afrika bado iko chini ikilinganishwa na mabara mengine, jambo linalopunguza uwezo wa bara kujenga nguvu ya pamoja ya kiuchumi.

Hata hivyo, kuanzishwa kwa soko huru la Afrika (AfCFTA) kunatajwa kuwa hatua muhimu kuelekea umoja wa kiuchumi.

Soko hilo linatarajiwa kuongeza biashara ya ndani, kuimarisha viwanda na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.

Kwa mtazamo wa kijamii, wataalamu wanasema umoja wa Afrika hauwezi kufanikiwa bila kujengwa kwa utambulisho wa pamoja wa Kiafrika.

Hili linahusisha kuimarisha elimu, historia na utamaduni unaowaunganisha Waafrika badala ya kuwagawa.

Vyombo vya habari, mitalaa ya elimu na sanaa vinatajwa kuwa na nafasi kubwa katika kujenga fikra ya umoja kwa kizazi kipya.

Kwa upande wake, mwanadiplomasia Profesa Benson Bana anaona ndoto hiyo bado ina uhalali wake licha ya kuchelewa kwake.

“Hii ni ndoto ya waasisi wetu. Inaweza kuchukua muda mrefu, hata miaka 100, lakini bado inawezekana. Muhimu ni kuendelea kuifikiria na kukijenga kizazi hadi kizazi,” anasema.

Anasisitiza kuwa Afrika lazima ijikomboe kutoka utegemezi wa kiuchumi na kuacha mifumo inayoiweka chini ya ushawishi wa mataifa ya nje ili kufikia umoja wa kweli.

Aidha, anaongeza kuwa teknolojia na mabadiliko ya kidijitali vinaweza kuwa nyenzo muhimu katika kuharakisha umoja wa Afrika. Kupitia mifumo ya kidijitali, nchi zinaweza kurahisisha biashara, kubadilishana taarifa na kuimarisha ushirikiano bila vikwazo vya kijiografia.

Katika mtazamo mpana, mjadala huu mpya unaonesha kuwa ndoto ya Umoja wa Afrika haijafa, bali imechelewa kutokana na mchanganyiko wa changamoto za kihistoria, kisiasa na kiuchumi.

Kadiri viongozi wanavyoanza kuijadili upya, swali linalobaki ni kama bara hili litajifunza kutoka kwa waasisi wake na kuchukua hatua madhubuti, au litaendelea kubaki katika mjadala usio na mwisho.

Kwa wachambuzi, jibu liko wazi kuwa umoja wa Afrika hauwezi kuwa ndoto ya viongozi pekee, bali lazima uwe mradi wa wananchi wenyewe ili uweze kudumu na kuzaa matokeo halisi.

Hii inamaanisha kuwashirikisha wananchi katika uamuzi, kuimarisha taasisi za kidemokrasia na kuhakikisha kuwa faida za umoja zinawafikia watu wa kawaida, si viongozi pekee.

“Wazo hili limekuwa likisuasua kutimia kwa sababu limebaki kuwa la wanasiasa na viongozi. Linapaswa kushushwa kwa wananchi ili liweze kutimia,” anasema Profesa Bana.

Tanzania iongoze safari

Mwanadiplomasia, Dk Bana anaitazama Tanzania kama nchi yenye nafasi na ushawishi mkubwa wa kuongoza safari ya kufufua ndoto ya umoja wa Afrika kwa wakati huu.

Anasema historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni mfano hai wa mafanikio ya kuunganisha mifumo miwili tofauti na kuunda taifa moja lenye mshikamano.

Anasema uzoefu huo unatoa somo muhimu kwa mataifa mengine ya Afrika kuhusu namna ya kushughulikia tofauti za kisiasa, kiutamaduni na kiutawala katika mchakato wa kuunganisha nchi.

“Rais Samia ameliona hili. Kauli yake si ya kawaida; ni wito kwa Afrika kufikiria upya mustakabali wake. Tanzania ina historia, ina uzoefu na ina uhalali wa kuongoza mjadala huu,” anasema Dk Bana.

Anasema ili ndoto hiyo itimie, ni muhimu kurejea katika misingi ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Umoja wa Afrika (OAU), ambayo lengo lake kuu lilikuwa kupigania uhuru wa bara, kulinda mamlaka ya nchi wanachama na kuimarisha mshikamano dhidi ya ukoloni na uingiliaji wa nje.

Aidha, anabainisha kuwa kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika (AU) kulilenga kwenda hatua zaidi kwa kujenga ushirikiano wa kiuchumi, kukuza maendeleo ya pamoja, kuimarisha amani na usalama, pamoja na kuweka mazingira ya Afrika kujitegemea katika mfumo wa dunia unaobadilika kwa kasi.

Kwa mujibu wa Dk Bana, mjadala unaoibuka sasa unaweza kuwa daraja muhimu la kuunganisha historia na mustakabali wa bara, iwapo viongozi watachukua hatua za vitendo badala ya kubaki kwenye matamko.

Anasisitiza kuwa safari ya umoja wa Afrika haiwezi kuwa ya haraka kama ilivyotamaniwa na waasisi wake, lakini inaweza kufikiwa kwa kujenga taasisi imara, kuimarisha biashara za ndani ya bara na kuondoa utegemezi wa mifumo ya nje.

Kwa mtazamo wake, Tanzania inaweza kuwa kitovu cha kuanzisha mjadala huo kwa vitendo, kwa kuhimiza ushirikiano wa kikanda, kuimarisha diplomasia ya uchumi na kuendeleza maono ya waasisi wake katika mazingira ya sasa ya dunia.

Hata hivyo, wachambuzi hao wanakubaliana kuwa kufufuka kwa mjadala huu si jambo la bahati mbaya, bali ni matokeo ya shinikizo la kimataifa linaloibana Afrika kutafuta njia mbadala za kujijenga upya.

Kwa kuzingatia historia, ndoto ya Afrika kuungana haikuwa tu wazo la kisiasa, bali pia ilikuwa mkakati wa kuikomboa kiuchumi, kiusalama na kiutamaduni.

Swali linalobaki sasa si kama Afrika itaungana, bali ni lini na kwa namna gani itachagua kufanya hivyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *