Dodoma. Rais wa Kenya, Dk William Ruto atalihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jumanne Mei 5, 2026

Tangazo hilo limetolewa bungeni leo Jumatano Aprili 29, 2026 na Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo ambaye ameomba wabunge kuhudhuria siku hiyo kwa wingi.

“Waheshimiwa wabunge, nawatangazia kuwa, siku ya Jumanne ya Mei 5, 2026 Mheshimiwa William Ruto, Rais wa Kenya atalihutubia Bunge hili, katika hotuba hiyo ambayo itakuwa ya kitaifa pia,” amesema Sillo.

Sillo amesema mbali na Rais Ruto, viongozi wengine wa kitaifa pia watashiriki bungeni siku hiyo, hivyo akasisitiza ushiriki wa wabunge uwe wa kutosha siku hiyo ambayo alisema ni ya kihistoria.

Ujio wa Rais Ruto na kulihutubia Bunge umekuja ikiwa imepita miaka mitano tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipolihutubia Bunge la Kenya Mei 5, 2021.

Hotuba ya Ruto itasubiriwa kwa hamu kuona kama atajibu hotuba aliyoitoa Rais Samia alipolihutubia Bunge la nchi hiyo akijikita zaidi kwenye kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo.

Kwenye hotuba hiyo, Rais Samia alizungumzia jinsi alivyotamani kuimarisha na kurejesha uhusiano baina ya nchi hizo mbili ambazo ni majirani na zenye uhusiano wa kindugu.

Rais Samia alisema ustawi wa mataifa hayo mawili unaathiri ustawi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa pamoja, hivyo ni lazima uimarishwe kwanza.

“Kila mara panapotokea kutokuelewana kati yetu, tunadhoofisha uhusiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, bila kukusudia na pia tunaathiri utangamano wa Afrika Mashariki, hivyo hatuna budi kuendelea kuelewana,” alisema Rais Samia.

Alieleza wakati furani Jumuiya hiyo ilijaribiwa kufuatia maneno na vitendo ambavyo vilipima uimara wa dhamira za nchi wanachama wa jumuiya hiyo kuendelea na safari ya utengamano.

Katika miaka ya hivi karibuni, biashara kati ya Tanzania na Kenya imeendelea kuimarika, ikihusisha bidhaa kama vile saruji, sukari, nafaka, mafuta ya kula na bidhaa za viwandani.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, kumekuwa na changamoto za mara kwa mara za vikwazo vya kibiashara na tofauti za sera.

Licha ya hali hiyo, jitihada za kidiplomasia zimeendelea kuimarisha ushirikiano kwa manufaa ya wananchi wa pande zote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *