Dar es Salaam. Serikali na watunga sera wametakiwa kuboresha mifumo ya kisheria na kanuni ili kukomesha adhabu ya viboko na aina nyingine za ukatili unaotweza utu wa watoto.

Wito huo umetolewa leo Jumatano, Aprili 29, 2026, jijini Dar es Salaam na asasi za kiraia wakati Tanzania ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Adhabu za Viboko inayofanyika kila ifikapo Aprili 30 kila mwaka.

Mashirika yaliyotoa wito huo ni  Save the Children Tanzania, Shirika la Wanawake katika Sheria Maendeleo barani Afrika (WiLDAF), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (Unicef), Shirika la Afya Duniani (WHO), HakiElimu, Jukwaa la Haki za Watoto Zanzibar (ZCRF) na Wanasheria Wanawake Zanzibar (Zafela).

Mengine ni Shule Direct, Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Jukwaa la Haki ya Mtoto Tanzania (TCRF), Msichana Initiative, Kituo cha Sheria na Haki za Biandamu (LHRC), Fawe Tanzania, Jumuiya ya Watu WanaoishinaVirusi Vya UkimwiZanzibar(Zapha+) Shirika la Msaada wa kisheria na Haki za Binaadamu Zanzibar(Zalho),Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa) naShirika la Kikristo la Huduma za Kijamii (CSSC).

Pia, mashirika hayo yameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuingiza na kupanua matumizi ya nidhamu chanya kitaifa kupitia sera zilizo wazi, mafunzo ya kina kwa walimu pamoja na ufuatiliaji endelevu, huku walimu wakishauriwa kuunda mazingira salama na jumuishi darasani yanayoheshimu utu wa mtoto, kwa kuzingatia Waraka wa Elimu Na. 24 wa mwaka 2002 unaohamasisha nidhamu isiyo ya ukatili.

Aidha, wazazi na walezi wametakiwa kutumia mbinu za malezi chanya zisizo na ukatili, wakati viongozi wa dini wakihimizwa kupinga mitazamo inayohalalisha ukatili na badala yake kuhimiza maadili ya huruma, heshima na ulinzi wa mtoto.

Pia, yamedai kuwa, licha ya Tanzania kusaini mikataba mbalimbali ya kupinga adhabu ya viboko, bado vitendo hivyo vinaendelea na ni miongoni mwa aina za ukatili dhidi ya watoto.

Mkurugenzi wa Nchi wa Save the Children Tanzania na Mwenyekiti wa muungano huo, Angela Kauleni, amesema kuna haja ya kuchukua hatua za haraka kukomesha vitendo hivyo, hasa katika mazingira ya kujifunzia.

“Adhabu za viboko, ikiwamo kupiga kwa fimbo, makofi na kudhalilisha kwa maneno, zinaendelea kuwaathiri watoto shuleni, madrasa na majumbani nchini Tanzania,” amesema Kauleni.

Amesema licha ya kuenea kwake, ushahidi unaonesha adhabu hizo haziboreshi nidhamu wala matokeo ya elimu, bali husababisha madhara makubwa kwa watoto na kuharibu mustakabali wao pamoja na ndoto zao.

Amesema kulingana na utafiti walioufanya, zaidi ya asilimia 70 ya watoto nchini hupitia ukatili wa kimwili, huku walimu wakitajwa miongoni mwa wahusika wakuu katika mazingira ya shule.

Kauleni  amesema tafiti zinaonesha adhabu za viboko husababisha hofu, kujitenga, kupungua kwa ushiriki darasani, kushuka kwa ufaulu pamoja na madhara ya muda mrefu ya kihisia na kisaikolojia.

“Adhabu za viboko zinadhoofisha utu wa mtoto na uwezo wake wa kujifunza na kufanikiwa. Kuzikomesha ni hatua muhimu katika kujenga mazingira salama na yenye ufanisi ya kujifunzia,” amesema.

Kauli ya CWT

Hata hivyo, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania, (CWT), Suleiman Ikomba amesema adhabu ni nyepesi inayotolewa na mwalimu kwa utaratibu kwa mwanafunzi mwenye makosa.

“Nawaomba hao wadau wanapokuja na jambo wafikirie kwa kina, kulikuwa na maana kubwa ya kuwa na adhabu ya viboko, kwetu adhabu hii inaufanisi mkubwa kwanza kumpunguzia mwalimu kazi, ya kufanya shughuli yake kwa ufanisi. Kusema atumie mbinu mbadala ni kumuongezea mwalimu mzigo kwa sababu ili iwe adhabu lazima usimamizi uwepo,” amesema Ikomba.

Amesema shule nyingi zina wanafunzi wengi na mwalimu mmoja anakuwa na masomo zaidi ya moja ya kufundisha, kusema atumie njia mbadala atatumia muda mrefu na kuwanyima wengine hali ya kufundisha.

Mkuu wa Ulinzi wa Mtoto wa Unicef Tanzania, Miranda Armstrong amesema ukatili hauna nafasi katika elimu na kusisitiza umuhimu wa kuchukua hatua madhubuti.

Amesema licha ya Tanzania kuridhia mikataba ya kimataifa ya haki za mtoto, bado adhabu za viboko zinaruhusiwa kisheria katika baadhi ya kanuni za elimu, hali inayosababisha pengo kati ya ahadi na utekelezaji wake.

“Nidhamu chanya ni mbinu mbadala yenye ufanisi inayojenga uhusiano bora kati ya walimu, wazazi na wanafunzi, huku ikiwasaidia watoto kukuza kujiamini, huruma na stadi muhimu za maisha,” amesema.

Makumba Mwemezi, mtafiti na mchambuzi wa sera kutoka HakiElimu, amesema wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na Serikali kushawishi kukomeshwa kwa adhabu ya viboko, pamoja na kufutwa kabisa kwa muongozo unaoelekeza wanafunzi kupigwa fimbo.

“Asasi za kiraia tumekuwa tukizunguka mikoa mbalimbali kutoa elimu ya kuachana na ukatili, hususan adhabu ya viboko, kwa sababu tunajua wakati mwingine huendelezwa na tamaduni zetu,” amesema Mwemezi.

Amesema wamejifunza kutoka mataifa jirani yenye tamaduni zinazofanana na Tanzania, kama Kenya, Uganda na Sudan Kusini, baadhi yao wamefanikiwa kutumia mbadala wa adhabu ya viboko unaofanya kazi vizuri.

“Kuna miongozo ambayo shule hizi inatoa, ikimwelekea mwalimu kutumia mbadala wa viboko. Mfano, mwanafunzi anaweza kupewa kazi ya kufanya wakati wa mapumziko.

“Wakati wenzake wanapumzika, yeye hufanya kazi hiyo, adhabu hiyo inatosha kumrekebisha ili asirudie kosa,” amesema Mwemezi.

Amesema kinachohitajika sasa ni mabadiliko ya mifumo, akieleza kuwa kutokana na ukubwa wa nchi, si rahisi kufikia maeneo yote kwa wakati mmoja.

“Tunachohitaji sasa ni mabadiliko ya mifumo. Nchi ni kubwa na hatuwezi kufika kila eneo kwa wakati mmoja, lakini Serikali na watunga sera wakiamua, jambo hili linaweza kukomeshwa mara moja,” amesema Makumba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *