‎Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliyoketi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemkuta na kesi ya kujibu, aliyekuwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Gongolamboto Dominic Mushi (34) anayekabiliwa na kesi ya mauaji.

Pia sasa mshtakiwa huyo anatakiwa kujitetea mahakamani hapo.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano, Aprili 29, 2026 na Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube aliyepewa Mamlaka ya nyongeza kusikiliza kesi hiyo ya mauji, baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao.

Mushi anakabiliwa na shtaka moja la mauaji ya mkewe Diana Hugo, tukio analodaiwa kulitenda Oktoba 14, 2024 eneo la Kinyerezi Kichangani, lililopo Wilaya ya Ilala.

Diana ambaye alikuwa mfanyakazi wa Benki ya NMB Tawi la Airport, anadaiwa kuuawa na mumewe kwa kunyongwa na kisha mwili wake kukutwa ukiwa kitandani ukitoka damu eneo la puani, masikioni na mdomoni.

‎Katika maelezo yake ya onyo aliyoyatoa Kituo cha Polisi Stakishari, alidai kelele za kuomba msaada alizokuwa akizitoa mke wake siku hiyo usiku ilikuwa ni ndoto kwani mke wake alikuwa anaota.

“Baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka, Mahakama umeona mshtakiwa anakesi ya kujibu, hivyo anatakiwa kujitetea” alisema Hakimu Makube.

Makube baada ya kutoa maelezo hayo, wakili anayemtetea mshtakiwa Roman Lamwai alidai kuwa mteja wake hata kuwa na shahidi, badala yake atakitetea peke yake.

Lamwai baada ya kuieleza mahakama hiyo, mshtakiwa huyo alianza kujitetea kwa kueleza siku ya tukio na jinsi alivyojikuta akiwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana.

Akiongozwa na wakili Lamwai, Mushi alidai kuwa yeye ni mwajiriwa Jiji la Dar es Salaam.

Alidai kuwa awali alikuwa ofisa Mtendaji Kata ya Mchikichini na baadaye alihamishwa na kwenda kuwa ofisa Mtendaji wa Kata ya Gongolamboto.

Alidai kuwa Diana ni mke wake na walifungua ndoa mwaka 2021 na mara ya mwisho kumuona ilikuwa Oktoba 13, 2024 akiwa nyumbani kwake Kinyerezi Kichangani.

“Nakumbuka siku hiyo tulienda Kanisani na tukarudi nyumbani na tulishinda kwa pamoja mpaka jioni na tulipata chakula cha usiku kwa pamoja” alidai mshtakiwa na kuongeza.

“Baada ya hapo, tulipumzika Sebuleni na ilipofika saa tatu usiku Diana aliniaga anaenda kulala kwa sababu alikuwa anasikia usingizi, nilimruhusu na mimi nikaendelea kuangalia runinga,” alidai.

Alidai wakati akiendelea kuangalia runinga, ilipofika usiku saa nne au saa tano kasoro alisikia mlango unahingwa.

“Nilinyanyuka na kwenda kufungua huo mlango, na baada ya hapo sikumbuki ni kitu gani kiliendelea pale,” alidai.

Alida kuwa alipata ufahamu akiwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana, baada ya watu kwenda kumjulia hali huku mkononi akiwa amefungwa pingu.

Alipoulizwa na wakili wake, sababu ya kufungwa pingu mikononi ilikuwa ni nini?

Shahidi huyo alijibu kuwa hajui ingawa aliwauliza watu walipofika hospitali hapo kumjulia hali, ambapo walimueleza kuwa mke wake amefariki dunia.

Hata hivyo, Mushi alidai kuwa watu hao hawakumwambia sababu ya kifo cha mke wake.

“Mheshimiwa hakimu, toka siku ile nimepewa taarifa pale hospital, kuwa mke wangu amefariki nina maumivu ambayo hayajawahi kukoma toka siku ile hadi leo hii ninavyoongea mbele ya Mahakama yako” alidai mshtakiwa.

Akiendelea kutoa ushahidi wake, alidai kuwa alimuona mke wake 2021 na wakati anamuoa alikuwa anatambulika kwa majina ya Diana Damian Hugo, lakini baada ya kufunga ndoa, alibadilisha jina na kuitwa Diana Dominic Mushi.

Alipoulizwa iwapo walikuwa na mgogoro na mkewe, mshtakiwa huyo alidai kuwa hawakuwa na tatizo.

“Mimi Sijawahi kuthibutu kumrushia kofi Diana tangu nimemuoa na kabla ya kumuona wala hatujawahi kugombana na wala hatujawahi kuwa na ugomvi wowote na hicho ndio kitu kinachoniumiza kwa sasa” alidai Mushi.

Vilevile alidai kuwa hajawah kuwa na ugomvi na ndugu yoyote wa Diana wala mama mkewe wake.

Alipoulizwa kuhusu kumtishia mama yake Diana, baada ya kumpigia simu, mshtakiwa huyo alikana madai hayo.

Shahidi huyo alidai mara ya mwisho kumuona mama mkwe wake ilikuwa ni leo ndani ya mahakama hiyo, alipokuwa kusikiliza ushahidi huo.

Hata hivyo, mshtakiwa alidai hakuna mpelelezi aliyemhoji mama huyo kuhusiana na kesi inayomkabili Mushi.

“Pia, hakuna ushahidi wala vielelezo ambavyo vinasema siku ya tukio, Mimi nilimpigia simu mama mkwe na kumtisha.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *