Dar es Salaam. Fursa za uwekezaji zinazidi kuimarika nchini baada ya Tanzania na Belarus kuanzisha kamati ya pamoja itakayoratibu na kusimamia miradi ya uwekezaji na biashara kati ya nchi hizo mbili.
Mpango huo unaolenga kuongeza mtiririko wa mitaji na teknolojia, unatoa nafasi kwa wawekezaji kutoka Belarus kuingia moja kwa moja katika sekta za uzalishaji ikiwamo kilimo cha kisasa, uchakataji wa mazao, viwanda na teknolojia.
Akizungumzia hatua hiyo, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema Serikali inalenga kuona uwekezaji huo unakuwa na tija kwa uchumi wa Taifa kwa kuzingatia thamani ya rasilimali zilizopo nchini.
Profesa Mkumbo ameyasema hayo leo Jumatano, Aprili 29, 2026 mara baada ya kufanya mazungumzo na kusaini mkataba wa ushirikiao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Belarus Maxim Ryzhenkov ambaye yuko nchini kwa ziara ya kikazi iliyoanza Aprili 28.
“Tunachokifanya sasa ni kuweka mfumo madhubuti wa kufuatilia na kuratibu uwekezaji. Kamati hii ya pamoja itakuwa jukwaa la kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa ufanisi na changamoto zinatatuliwa mapema,” amesema Profesa Mkumbo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Belarus Maxim Ryzhenkov na Waziri wa Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo wakisaini mkataba wa ushirikiano katika uwekezaji baina ya mataifa hayo mawili.
Amesema makubaliano hayo yanaweka msingi wa Tanzania kunufaika na utaalamu wa Belarus, hasa katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na matumizi ya teknolojia katika uzalishaji.
“Tunataka kuona uwekezaji unaoingia nchini unaongeza thamani ya mazao yetu, unakuza viwanda na unachangia ajira kwa Watanzania. Belarus wana uzoefu mkubwa katika maeneo haya, hivyo ushirikiano huu ni muhimu sana kwetu,” amesema Profesa Mkumbo.
Profesa Mkumbo amesema hatua hiyo inalenga pia kuondoa vikwazo vinavyoweza kuwakatisha tamaa wawekezaji kwa kuweka utaratibu wa pamoja wa kushughulikia changamoto za kibiashara na kiuwekezaji.
“Kamati hii itakuwa na jukumu la kubaini fursa mpya, kufuatilia utekelezaji wa miradi na kuhakikisha kuwa mazingira ya uwekezaji yanabaki kuwa rafiki na yenye ushindani.
“Belarus inaonyesha nia ya kuwekeza zaidi nchini kwa kuzingatia mafanikio yake katika sekta za teknolojia, elimu na uchakataji wa mazao, hatua inayotarajiwa kuongeza kasi ya maendeleo ya viwanda nchini,” amesema Profesa Mkumbo.
Kwa upande wake, Waziri
Ryzhenkov amesema nchi yake iko tayari kuanzisha ushirikiano wa moja kwa moja kati ya vyuo vikuu na vituo vya utafiti vya Tanzania ili kuimarisha tafiti za pamoja zitakazonufaisha pande zote mbili.
“Tuko tayari kuanzisha mawasiliano ya moja kwa moja kati ya vyuo vikuu na vituo vya utafiti ili kuunda tafiti za pamoja zitakazowanufaisha wote na kuwaleta karibu zaidi wanasayansi wa nchi zetu,” amesema Ryzhenkov.
Amesema katika ziara yake, ametembelea maeneo muhimu ya kiuchumi ikiwamo bandari, na kubainisha kuwa Belarus inaangalia namna ya kushiriki katika shughuli za maeneo hayo ili kuongeza uwekezaji na biashara.
“Tumetembelea maeneo muhimu yanayohusika na shughuli za uagizaji na usafirishaji wa bidhaa na tunaangalia namna ya kushiriki katika mifumo hiyo,” amesema.
Ryzhenkov amesema pia kuna maombi kutoka kwa baadhi ya kampuni za Urusi zinazohitaji ushirikiano, hasa katika sekta ya mbolea na usambazaji wa bidhaa katika ukanda wa Afrika Mashariki, jambo linaloweza kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya kikanda.
Ameeleza Belarus inaichukulia Tanzania kama mshirika wake mkuu na soko muhimu la ukuaji katika ukanda huo, hivyo iko tayari kuanzisha miradi ya kuimarisha biashara si tu kati ya nchi hizo mbili, bali pia na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
“Tunaiangalia Tanzania kama mshirika wetu muhimu na soko kuu la ukuaji katika ukanda huu. Tuko tayari kuja na miradi itakayochochea biashara kati ya nchi zetu na pia kuwa msingi wa ushirikiano wetu na nchi nyingine za Afrika Mashariki,” amesema.
Aidha, amesema kamati ya pamoja ya biashara na uchumi ni nyenzo muhimu katika kuimarisha mahusiano hayo, akibainisha kuwa ushirikiano huo utagusa pia nyanja nyingine zikiwamo siasa, masuala ya kijamii na kibinadamu.
Katika hatua nyingine, Ryzhenkov amesema nchi yake iko tayari kurahisisha taratibu za viza ili kuchochea mwingiliano wa watu na wafanyabiashara kati ya nchi hizo mbili.
“Tutafanya kila tuwezalo kurahisisha masuala ya viza. Hili ni jambo muhimu kwa kukuza uhusiano wa biashara kati ya wafanyabiashara, watu kwa watu na nchi kwa nchi,” amesema.
Ameongeza kuwa kuna makubaliano mengine muhimu yanayoendelea kujadiliwa, yakiwamo ya ulinzi wa uwekezaji na ushirikiano kati ya mamlaka za forodha, ambayo yanatarajiwa kukamilika kabla ya ziara ya Waziri Mkuu wa Belarus.
Akizungumzia hatua hiyo Mwenyekiti wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Angelina Ngalula amesema wadau wa sekta binafsi wako tayari wa kunufaika na fursa hizo, wakipanga kutuma ujumbe wa wafanyabiashara nchini Belarus mwezi ujao kushiriki maonesho ya biashara na kuangalia fursa zilizopo.