BAO la dakika ya 119 lililofungwa na mshambuliaji wa Simba, Seleman Mwalimu, limetosha kusitisha ukame wa mataji klabuni hapo, lakini pia likivunja rekodi tatu ndani ya Yanga. Wakati huohuo, likiivua ubingwa Yanga na sasa Simba ndiyo mabingwa wapya wa Kombe la Muungano ikilichukua kwa mara ya saba sawa na Yanga.
Rekodi ya kwanza ni ile ya Simba kuifunga Yanga kwa mara ya kwanza baada ya kupita takribani miaka mitatu bila ya ushindi ambapo mara ya mwisho ilishinda 3-1 kwa penalti katika Ngao ya Jamii iliyochezwa Agosti 13, 2023.
Rekodi ya pili ni ya kusitisha ubabe wa Yanga ambayo ilikuwa haijaonja vipigo katika mashindano ya ndani kwa muda mrefu huku ikileta ubabe Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB.
Mara ya mwisho ilifungwa mabao 3-1 na APR katika robo fainali ya Kombe la Mapinduzi 2024, mechi iliyochezwa Januari 7, 2024 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Baada ya hapo, imekuja kufungwa tena Aprili 29, 2026 uwanjani hapo.
Pia rekodi ya tatu ni ya kusitisha mwendo mzuri wa kocha Pedro Goncalves ambaye tangu atambulishwe Oktoba 25, 2025 alikuwa hajawahi kupoteza mechi yoyote ya mashindano ya ndani huku akifanikiwa kubeba Kombe la Mapinduzi 2026.
Mwalimu ambaye alitokea tena benchi kwa mara nyingine katika michuano hii, aliingia dakika ya 26 kuchukua nafasi ya Anicet Oura aliyeumia nyama za paja.
Mwalimu alirudia alichofanya kwenye michezo miwili ya kwanza dhidi ya Mafunzo na Mlandege kuifungia Simba bao pekee lililoipa ushindi timu hiyo.
Timu hizo zilicheza kwa dakika 90 zikimaliza bila kufungana zikionyesha kushambuliana kwa tahadhari.
Baada ya kumalizika dakika 90, mchezo huo ukaingia kwenye dakika 30 za nyongeza, lakini bado zikiendelea kukosa umakini kumalizia mashambulizi yake.
Simba bao lake lilipatikana baada ya kiungo Clatous Chama kuchezewa vibaya na Edmund John akiwa eneo la hatari na mwamuzi Dickes Nyagrowa kuamua ipigwe penalti, Mwalimu akafanya kweli.
Bao hilo limekuwa la tatu kwa Mwalimu kwenye mashindano ya Muungano akilingana na Prince Dube wa Yanga.
Simba ubingwa huo wa Muungano unakuwa wa saba kihistoria ambapo mara ya mwisho iliuchukua mwaka 2024.