London, England. Baada ya zaidi ya miaka 40 tangu walipocheza nusu fainali ya mwisho ya mashindano makubwa ya Ulaya, Nottingham Forest wanarejea hatua hiyo muhimu wakitarajia kumenyana na Aston Villa katika mechi ya kwanza ya Europa League itakayopigwa leo kwenye Uwanja wa City Ground uliopo West Bridgford, Nottinghamshire, England.
Hii itakuwa nusu fainali ya kwanza ya mashindano makubwa ya Ulaya kuzikutanisha timu mbili za England tangu 2008/09, jambo linaloongeza uzito wa mchezo huo.
Forest wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na morali ya juu baada ya kuichapa Sunderland mabao 5-0 kwenye Ligi Kuu England huku kikosi hicho cha kocha Vítor Pereira kikiwa hakijapoteza mechi nane zilizopita za mashindano yote (ushindi tano na sare tatu).
Rekodi yao ya ushambuliaji pia ni bora katika michuano ya Europa League msimu huu, wakiwa wamepiga mashuti mengi zaidi (232) na yaliyolenga lango (88) kuliko timu nyingine yoyote iliyosalia, ingawa michezo yao ya nyumbani imekuwa na mabao machache kwani ni mechi mbili tu kati ya tisa zilizozidi mabao matatu.
Kwa upande wa Villa, chini ya kocha Unai Emery, wanakuja wakiwa na uzoefu mkubwa katika michuano hii na wameweka kipaumbele kikubwa kwenye Europa League licha ya kupoteza mechi yao ya mwisho dhidi ya Fulham katika ligi.
Emery ana rekodi nzuri ya kufika hatua za mwisho za mashindano haya huku Villa wakilenga kufuta kumbukumbu ya kutolewa katika hatua kama hii msimu wa 2023/24. Ushindi katika mchezo huu wa kwanza unaweza kuwaweka kwenye nafasi ya kufikia ushindi wa 10 mfululizo katika michuano ya Ulaya, rekodi ambayo ni timu moja tu ya England imewahi kuifikia.
Takwimu zinaonyesha mchezo unaweza kuwa mgumu na wa ushindani mkubwa, hasa ukizingatia kuwa Villa hawajashinda ugenini dhidi ya Forest tangu mwaka 2019 na mechi yao ya mwisho kwenye uwanja huo iliisha kwa sare ya bao 1-1.
Pia Villa wamefunga zaidi ya mabao mawili katika mechi moja tu kati ya saba za ugenini zilizopita huku vipigo vinne kati ya vitano vyao vya mwisho vikiwa kwa tofauti ya mabao mawili au zaidi.
Macho pia yataelekezwa kwa nyota wa Nottingham Forest, Morgan Gibbs-White, ambaye yuko kwenye kiwango bora baada ya kuhusika katika mabao sita ndani ya mechi tatu zilizopita pamoja na Morgan Rogers wa Villa ambaye timu yake haijapoteza mechi yoyote aliyofunga msimu huu. Usiku wa leo pia ni wa kihistoria kwa SC Freiburg, timu hiyo nayo inaingia kwenye nusu fainali ya UEFA Europa League ikiwa kwenye kipindi kigumu cha matokeo, jambo linalokuja wakati mbaya zaidi ambapo wanatakiwa kuvaana na SC Braga katika mchezo wa kwanza.
Braga wamefika nusu fainali ya mashindano makubwa ya Ulaya kwa mara ya pili katika historia yao baada ya kuiondoa Real Betis robo fainali lakini kiwango chao kwenye ligi ya ndani kimekuwa tofauti kabisa na mafanikio yao katika michuano hiyo ya Ulaya.
Kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Santa Clara mwishoni mwa wiki kimewaacha mbali kwa alama 26 kutoka kileleni mwa ligi ya Ureno, ingawa bado wana nafasi ya kushiriki michuano ya Ulaya msimu ujao.
Kwao, kushinda Europa League kunaweza kuwapa tiketi ya kurejea katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2023/24. Hata hivyo, rekodi yao si nzuri sana katika michezo ya kwanza ya hatua za mtoano, wakishinda mara mbili kati ya mechi 11 zilizopita, japokuwa wanafarijiwa na ushindi 12 katika mechi 16 za nyumbani katika michuano ya Ulaya.
Kwa upande wa Freiburg, mambo sio mazuri baada ya kupoteza kwenye DFB-Pokal kabla ya kufungwa mabao 4-0 na Borussia Dortmund mwishoni mwa wiki. Hii ni safari yao ya kwanza kufika nusu fainali ya Ulaya, lakini wamekuwa imara katika hatua zilizopita baada ya kumaliza kwenye nafasi nane bora katika hatua ya ligi na kuziondoa Genk na Celta Vigo kwa kishindo.
Hata hivyo, rekodi yao ya ugenini kwenye Europa League si ya kuridhisha, wakishinda mechi mbili kati ya tisa zilizopita, huku wakishindwa kufunga katika tatu kati ya nne za mwisho. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana michuano ya Ulaya, huku Braga ikiwa na rekodi mbaya dhidi ya timu za Ujerumani katika hatua za mtoano, ikiwa haijashinda wala kufunga katika mechi nne zilizopita (sare moja, ikipoteza tatu).
Katika upande wa wachezaji wa kuangaliwa, Ricardo Horta wa Braga ana rekodi ya kuhusika kwenye mabao 32 katika mashindano haya (mabao 18 na asisti 14), ikiwa ni idadi kubwa zaidi kwa mchezaji mmoja katika klabu moja tangu 2009/10. Kwa Freiburg, Yuito Suzuki ameonyesha ubora wake kwa kufunga katika mechi mbili kati ya tatu zilizopita za Europa League, huku mabao yake mengi yakija mapema kabla ya dakika ya 60.
Wakati mambo yakiwa hivyo katika michuano ya Europa League kwa upande wa Conference League napo kutakuwa mechi mbili za nusu fainali, Rayo Vallecano itacheza dhidi ya Strasbourg huku Shakhtar Donetsk ikiwa na kibarua kizito mbele ya Crystal Palace, mechi zote zitapigwa saa 4:00 usiku.