Mbeya. Tambo za Kocha wa Mbeya City, Salum Mayanga na zile za Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ wa Mashujaa, zinanogesha zaidi vita yao katika kuwania pointi tatu za mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Mchezo huo ambao utapigwa leo Alhamisi saa 10:15 jioni, umekaa kimtego huku ukitarajiwa kuwa na upinzani kutokana na matokeo ya timu zote Ligi Kuu Bara msimu huu, ambapo wenyeji Mbeya City wapo nafasi ya 14 kwa pointi 17, huku Mashujaa wakiwa nafasi ya 11 kwa pointi 21.

Timu hizo zinakutana ikiwa Mashujaa haijapata ushindi katika mechi nne mfululizo za Ligi Kuu, ikiambulia sare pekee, huku Mbeya City ikikumbuka kipigo kizito cha mabao 6-0 kutoka kwa Yanga ambacho kilihitimisha safari ya Kocha Mecky Maxime, ndipo Mayanga atachukua nafasi yake.

Utamu wa mechi hiyo unakumbusha tukio la Mashujaa kuishusha Mbeya City msimu wa 2022-2023 walipokutana play pff kwenye Uwanja wa Sokoine na kuwalaza bao 1-0, huku mechi ya mwisho kukutana mkoani Kigoma msimu huu, Mbeya City ilikufa bao 1-0.

Mayanga anakutana na Mashujaa, timu aliyoachana nayo Februari mwaka huu ambapo hadi anaondoka timu hiyo ilicheza mechi 12 za Ligi Kuu Bara, ikishinda tatu, sare nne na kupoteza tano. Kuondoka kwake ndipo akatua Julio ambaye ameshinda mechi moja na sare nne, hajapoteza.

Mayanga ambaye utakuwa mchezo wake wa kwanza kuiongoza Mbeya City tangu atambulishwe kikosini hapo, atakuwa na kazi ya kufanya kusaka ushindi huku akisema wanafahamu ugumu na umuhimu wa mechi hiyo, akieleza kuwa maandalizi waliyofanya anaamini watashinda.

Alisema wachezaji wameonesha ari na morali katika mazoezi yao akifafanua kuwa wapo katika mazingira magumu, hivyo jambo moja kwao ni kushinda mchezo huo ili kufufua na kurejesha matumaini mapya.

“Wachezaji waliokuwa majeruhi wamerejea, muda niliokaa na timu nimerekebisha makosa, tunajua ugumu wa wapinzani ila tunalohitaji ni pointi tatu ili kurejesha matumaini mapya kikosini,” alisema Mayanga.

Kwa upande wake nahodha na straika wa timu hiyo, Eliud Ambokile, alisema kwa sasa hawafikirii zaidi matokeo ya mechi zilizopita badala yake yaliyotokea wamesahau na sasa akili ni mchezo huu.

“Ni mchezo mgumu kutokana na ubora wa timu zote na uhitaji wa pointi, wachezaji tuko tayari kupambania pointi tatu, tunaomba mashabiki waje kwa wingi kutusapoti,” alisema straika huyo.

Naye Julio alisema kwa sasa ligi haina cha ugenini wala nyumbani akiwapongeza baadhi ya waamuzi kwa kuchezesha vyema na kwamba kiu yao ni kupata pointi tatu.

Kuhusu mwenendo wa timu hiyo, kocha huyo alisema tangu ametua kikosini amefanya mabadiliko mengi na hajapoteza mchezo wowote, jukumu lililobaki ni la wachezaji kufunga.

“Nimerekebisha mengi ikiwamo morali, kutengeneza nafasi na sasa kazi iliyobaki ni utulivu wa mchezaji mwenyewe kufunga mabao, naendelea kutengeneza timu na mafanikio yapo kwakuwa sijapoteza mechi,” alisema Julio.

Mechi nyingine leo ni Fountain Gate dhidi ya Pamba Jiji kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kuanzia saa 8:00 mchana.

Kocha wa Fountain Gate, Fred Felix Minziro, alisema: “Nimezungumza na vijana na kuwaeleza umuhimu wa kupata matokeo mazuri kwenye mechi ya kesho (leo) dhidi ya Pamba Jiji, wamenielewa na imani yangu watafanya kazi nzuri.”

Naye nahodha msaidizi wa Fountain Gate, Derick Mukombozi, alisema: “Hautakuwa mchezo rahisi kwetu, lakini tumepata maandalizi mazuri na tupo tayari kupambania alama tatu.”

Saa 12:30 jioni, JKT Tanzania itaikaribisha KMC kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar ikiwa ndiyo mechi ya kufunga siku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *