Arusha. Wadau wa sekta ya habari nchini wamewasilisha ajenda 15 serikalini wakitaka mabadiliko ya Kikatiba, kisheria na kiuchumi yatakayolinda uhuru wa vyombo vya habari, kuimarisha haki za wanahabari na kuhakikisha mustakabali imara wa tasnia hiyo nchini.

Maazimio hayo yamepitishwa kwenye maadhimisho ya 33 ya kitaifa ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yanayofanyika Arusha na kukutanisha wanahabari, watunga sera, viongozi wa asasi za kiraia na wadau wa habari wa ndani na kimataifa, kujadili hali ya uhuru wa habari na mustakabali wa uandishi wa habari nchini.

Lengo ni kushinikiza Serikali kufanya marekebisho ya Katiba, sheria za habari na sera za Taifa ili kuhakikisha kunakuwepo ulinzi madhubuti zaidi wa uhuru wa kujieleza, uhuru wa vyombo vya habari na usalama wa wanahabari.

Katika mkutano huo wa siku mbili, wadau hao walieleza kuwa licha ya hatua zilizopigwa, mfumo wa sasa wa sheria na udhibiti, bado unahitaji mageuzi ya haraka ili kuruhusu vyombo vya habari kufanya kazi kwa uhuru, weledi na ufanisi katika jamii ya kidemokrasia.

Akiwasilisha maazimio hayo leo Alhamisi Aprili 30, 2026 mbele ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tech and Media Convergency (TMC), Asha Abinallah amesema mapendekezo hayo yametokana na mijadala ya kina, majukwaa ya kitaalamu na mashauriano yaliyowahusisha wadau wa habari wa ndani na nje ya nchi.

“Maazimio haya yanawakilisha sauti ya pamoja ya sekta ya habari na yanalenga kujenga mazingira huru, salama na ya kidemokrasia, wanahabari wanaweza kufanya kazi bila hofu, vitisho wala vikwazo visivyo halali,” amesema.

Katika eneo la uchumi, Abinallah amesema kipengele hicho wanaitaka Serikali kuchukua jukumu la kupunguza mzigo wa kifedha kwa taasisi za habari kupitia misamaha ya kodi kwa vifaa vya habari, teknolojia za utangazaji, miundombinu ya kidijitali na vifaa vya uzalishaji wa maudhui.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amewataka wanahabari kuunda kamati maalumu itakayoshirikiana na wizara yake kuhakikisha maazimio hayo yanaanza kufanyiwa kazi kabla ya maadhimisho yajayo.

Makonda ametaka upande wa taarifa za umma,  taasisi za Serikali kuwa wazi zaidi kwa wanahabari

“Serikali ina wajibu wa kuhakikisha wanahabari wanapata taarifa sahihi kwa wakati ili kuzuia upotoshaji, taasisi za umma lazima ziache kuwakwamisha wanahabari badala yake zifungue milango kwa vyombo vya habari,”amesema.

Pia, amesema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya taasisi zitakazobainika kuficha taarifa za umma.
Mbali na mageuzi ya sheria na sera, Makonda amewataka wanahabari kujikita katika uwezeshaji wa kiuchumi na ubunifu, akisema ukosefu wa uhuru wa kifedha ni moja ya vitisho vikubwa kwa uhuru wa kweli wa kazi zao.

Amesema mazingira duni ya kazi na kipato kidogo huwafanya wanahabari kuwa rahisi kushawishiwa kisiasa au kibiashara, hali inayoweza kuhatarisha uadilifu na hadhi ya taaluma hiyo nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *