Rukwa. Jeshi la Polisi likiwashikilia watuhumiwa wawili kwa tuhuma za kuwafanyia ukatili watoto katika familia zao.

Tukio la kwanza limetokea katika Kitongoji cha Kasanzama, mji mdogo wa Laela wilayani Sumbawanga, ambako mwanamke mmoja anadaiwa kumuunguza mgongoni mtoto wake wa kiume (8) kwa pasi ya umeme, akimtuhumu kumuibia Sh2,000.

Wakazi wa eneo hilo wamesema matukio ya ukatili yamekuwa yakijirudia, wakimtaja mtuhumiwa huyo, Aisha Credo Mpepo (25), kuwa na tabia ya muda mrefu ya kumuadhibu mtoto wake kwa ukali uliopitiliza.

Mkazi wa eneo hilo, Anna Lunguya amesema waliamua kuchukua hatua ya pamoja baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya.
 

“Tumekuwa tukimwonya mara kwa mara lakini hakubadilika, ndipo tulipoamua kwenda kutoa taarifa polisi,” amesema Anna.

Mkazi mwingine, Eflazia Ntasima, amesema jamii haiwezi kuvumilia vitendo hivyo na kuitaka Serikali kuchukua hatua kali.
 

“Hatuwezi kukaa kimya wakati watoto wanateswa. Tunataka sheria ichukue mkondo wake ili iwe fundisho,” amesema Eflazia.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Shadrack Masija, amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa wawili kuhusiana na matukio hayo.

Amesema mtuhumiwa mwingine ni Fortunatus Benezet Mawela (60), mkazi wa Kijiji cha Singiwe wilayani Kalambo, anayeshtakiwa kwa kumchoma moto mjukuu wake wa kiume (16) tumboni na mapajani baada ya kumtuhumu kuiba ndizi.

Katika tukio tofauti, mwanaume mmoja, Bosco John Fatachi, amekutwa na hatia na Mahakama ya Wilaya ya Kalambo kwa kumtesa mtoto wa miaka 8 kwa kumpiga kwa waya wa umeme na kumfunga kamba mikono na miguu, akimtuhumu kumuibia pipi za Sh200.

Mahakama imemuamuru kulipa fidia ya Sh500,000 na faini ya Sh300,000 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.

Wakazi wameendelea kuitaka Serikali kuimarisha ulinzi wa watoto na kuhakikisha sheria zinatumika kikamilifu ili kukomesha vitendo hivyo.

Kwa upande wake, mzee wa mila katika kijiji cha Singiwe, Aniset Wakutwa, amesema kuporomoka kwa maadili na malezi duni kunachangia matukio hayo, huku mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Laela, Nestory Mikwasa, akihusisha ukatili huo na kukosekana kwa hofu ya Mungu.

Jeshi la Polisi limesema linaendelea kukamilisha taratibu za kisheria ili kuwafikisha mahakamani watuhumiwa waliobaki, huku likiwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya ukatili ili viweze kudhibitiwa mapema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *