Dar es Salaam. Idadi ya vijana 1,961 walioomba mikopo kupitia mfuko wa vijana na upungufu uliobainika umeifanya Serikali kutangaza kutoa mafunzo kwa vijana.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwaandaa vijana kwa ajili ya maombi ya mikopo kwa awamu zinazofuata ili wengi kutoka makundi mbalimbali wanufaike.

Taarifa kwa umma iliyotolewa jana Jumatano, Aprili 29, 2026, na Wizara ya Maendeleo ya Vijana imeeleza upungufu uliobainika wakati wa uombaji wa mikopo ni ya uandishi wa miradi.

Dosari nyingine iliyobainika ni kutowasilishwa kwa usahihi kwa nyaraka za maombi ya mikopo kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na wizara hiyo.

“Kwa kuwa utoaji mikopo ni programu endelevu kwa Serikali, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana imeona ni muhimu kufanyika mafunzo kwa vijana. Mafunzo hayo yatakuwa yakifanyika kikanda. Ratiba kamili ya mafunzo itatolewa kwa umma wakati ukifika,” taarifa ya wizara hiyo imeeleza.

Katika orodha ya wanufaika iliyotangazwa na wizara hiyo, uhakiki utakapokamilika wanufaika wote watakaokuwa na sifa na kupitishwa watapatiwa mafunzo ya siku tatu kuhusu elimu ya biashara, elimu ya fedha, elimu ya matumizi sahihi ya mkopo pamoja na elimu ya ujuzi inayoendana na mradi husika.

“Mafunzo yatakayofanyika katika ngazi ya kanda husika kwa tarehe itakayotangazwa Mei, 2026,” imeeleza taarifa hiyo.

Malalamiko yako hapa

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa ACT Wazalendo, Abdul Nondo, kupitia taarifa aliyoitoa kwa umma Aprili 29, 2026, amesema katika hatua ya maombi ya mkopo walishuhudia changamoto mbalimbali.

Wenyeviti wa serikali za mitaa kugoma kuwaandikia vijana barua za utambulisho kwa sababu vijana wengi walitakiwa kuonesha eneo wanalofanyia biashara, wakati wengi wao walikuwa wanaanza biashara.

“Changamoto nyingine ni muda wa maombi ya mkopo kuwa mfupi, ukosefu wa taarifa na uratibu usioeleweka,” amesema.

Nondo amependekeza Wizara ya Maendeleo ya Vijana kutoa ufafanuzi wa maana halisi ya wanufaika 1,961 na kueleza walipatikana kwa namna gani.

“Tunaitaka Wizara ya Maendeleo ya Vijana haraka ifungue dirisha la pili ili vijana wote ambao hawakupewa fedha katika awamu ya kwanza wapewe. Fedha hizi ni kodi za wananchi na ni mkopo, vijana watalipa,” amesema.

Sifa za muombaji

Kulingana na wizara hiyo, muombaji wa mikopo hiyo anatakiwa awe raia wa Tanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 35.

Pia awe na nakala ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) au namba ya NIDA, awe na eneo linalotambuliwa na mamlaka kwa ajili ya kufanyia biashara; mfano soko.

“Sifa nyingine awe mkazi wa eneo husika na awe na barua ya uthibitisho kutoka Serikali za Mitaa/Kijiji, awe aidha mtu mmoja, kampuni changa au kikundi cha kijamii kilichosajiliwa kinachofanya shughuli ya kiuchumi,” amesema.

Vilevile awe na andiko la mradi/biashara inayoombewa mkopo na akaunti ya benki au namba ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mwombaji.

Namna ya kuomba

Mwombaji wa mkopo atatakiwa kuwasilisha barua ya maombi ya mkopo ikibainisha jina la kikundi au mwombaji, aina ya mradi unaopendekezwa, kiasi cha mkopo kinachohitajika na mahali mradi utakapotekelezwa.

Mwombaji atatakiwa kuambatisha nyaraka zifuatazo wakati wa kuomba mkopo.

Jambo lingine ni andiko la mradi lisilozidi kurasa tano, kitambulisho cha Taifa au namba ya NIDA/Kitambulisho cha Mpiga Kura, utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN), leseni ya biashara kwa biashara inayoendelea.

“Barua ya utambulisho wa eneo la biashara kutoka kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa/Kijiji.

“Vilevile picha mbili za mkopaji zilizopigwa ndani ya muda usiozidi miezi mitatu kabla ya maombi na muhtasari wa kikao uliosainiwa na wanachama wa kikundi wenye ajenda ya maombi ya mkopo,” taarifa ya wizara inaeleza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *