UONGOZI wa Singida Black Stars, umeonyesha nia ya kumuhitaji kiungo mshambuliaji wa Gor Mahia ya Kenya, Mghana, Enock Morrison, ambaye hadi sasa hakuna mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya huko alipo, pindi uliopo utakapofikia tamati mwisho wa msimu huu.

Awali mabosi wa Singida walihitaji kumsajili mchezaji huyo katika dirisha dogo la Januari 2026, ingawa ilishindikana kukamilisha kutokana na kutokubaliana kwa baadhi ya vipengele, hivyo kwa sasa wanapambana kumpata mwishoni mwa msimu.

Chanzo kutoka ndani ya timu hiyo, kimeliambia Mwanaspoti, Enock ni miongoni mwa wachezaji wanaofuatiliwa kwa ukaribu na Singida, ambapo tayari mazungumzo ya mkataba huo wa awali yalianza kufanyika tangu kwenye dirisha dogo la Januari 2026.

SINGID 01

“Dirisha dogo la Januari 2026, tulifikia makubaliano na mchezaji mwenyewe, ila tulipoenda kwenye klabu yake kwa ajili ya kufikia muafaka tukashindwana kwa baadhi ya vipengele, kwa sasa tumerudi upya msimu ujao tena,” kilisema chanzo hicho.

Mtoa taarifa huyo amesema wanataka kukamilisha dili hilo mapema ili kuepuka usumbufu mkataba wake utakapoisha, kwani kwa sasa itakuwa ni rahisi kuliko kusubiri hadi msimu utakapoisha, kutokana na timu mbalimbali zilizoonyesha nia ya kumtaka.

SINGID 02

Awali vyanzo mbalimbali kutoka Ghana vilieleza mchezaji huyo pia anafuatiliwa kwa ukaribu na vigogo wa soka nchini Klabu ya Simba, ambayo imeonyesha uhitaji wa kumsajili, ingawa kwa sasa imerudi nyuma na kuiachia Singida kuwania saini yake.

Nyota huyo aliyezaliwa Januari 18, 2000, akiwa na uwezo wa kucheza kiungo wa kati kwa ufasaha mkubwa, huku akitokea pia upande wa kulia na kushoto, amezichezea timu mbalimbali, zikiwemo, King Faisal FC na Asante Kotoko zote za kwao Ghana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *