Arusha. Ni simanzi, vilio na majonzi. Ndivyo ilivyoonekana kwa waombolezaji na wanafamilia wa ndugu watatu wa familia moja waliofariki kwa ajali ya moto baada ya mabaki ya miili yao kuwasili nyumbani kwao kwa ajili ya kuagwa kabla ya kwenda kuzikwa mkoani Kilimanjaro.
Ndugu wa familia moja ambao ni bibi, Mkunde Ephata (85) na wajukuu zake wawili Jackson Geofrey (26) na Lerato Shabani (11), walifariki dunia alfajiri ya Aprili 28, 2026 baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuteketea kwa moto.
Leo Ijumaa Mei Mosi, 2026 mabaki ya miili hiyo yameagwa katika Kijiji cha Mji Mwema, Kata ya Usa River, wilayani Arumeru ambapo walikuwa wakiishi.
Maziko ya wanafamilia hao yanatarajiwa kufanyika leo katika Kijiji cha Msangeni, Ugweno wilayani Mwanga, Kilimanjaro.
Tofauti na ilivyozoeleka katika misiba mingine, kutokana na nyumba hiyo kuungua na kuisha yote, wanafamilia wa bibi na wajukuu hao walilazimika kufunga hema kubwa mbili nje ya nyumba hiyo na lingine katika uwanja uliopo jirani nao kuendelea kuomboleza.
Majeneza yenye miili ya ndugu watatu wa familia moja, bibi na wajukuu zake yakiwa nje ya nyumba yao kwa ajili ya kuagwa leo Mei 1, 2026, katika Kijiji cha Mjimwema, Usa River wilayani Arumeru. Picha na Janeth Mushi
Awali akizungumza na Mwananchi jana Alhamisi Aprili 30, 2026 nyumbani hapo, msemaji wa familia hiyo, Kitia Wilderson, amesema kuwa wanatarajia kuchukua mabaki ya miili hiyo alfajiri kati ya saa 11 hadi 12 kisha kufanya ibada fupi kabla ya kuanza safari kuelekea mkoani Kilimanjaro kwa maziko.
“Tunategemea kesho kati ya saa 11 na 12 alfajiri kuchukua mabaki ya miili hiyo ambayo yamehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti kilichopo kituo cha afya jirani na hapa.
“Kisha tutakuja hapa nyumbani tutatoa heshima za mwisho na kuanzia saa mbili asubuhi tunatarajia kuanza safari kuelekea Msangeni kwa maziko kesho hiyo hiyo saa tisa alasiri baada ya shughuli za ibada kumalizika,” ameeleza.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Shedrack Antony, akisimulia namna tukio hilo lilivyotokea, amedai kuwa alfajiri ya siku hiyo walisikia kelele na walipotoka nje walishuhudia moto mkubwa ukiwaka katika nyumba ya bibi huyo aliyekuwa akiishi na wajukuu zake hao wawili.
Jackson Geofrey (26) aliyefariki kwa ajali ya moto.
Ameeleza kuwa walianza kuamshana ila walishindwa kuwaokoa kwani waliteketea ndani kutokana na moto kuwa mkali na moshi kutanda sana.
“Huyu mama ni jirani yangu. Ilikuwa saa 11 alfajiri tulisikia kelele za kuomba msaada. Tulivyotoka nje tulishtuka moto umeshika nyumba upande mmoja, tukang’ang’ana kuvunja mlango kuwaokoa na tulivyovunja mlango tukamulika ndani, moshi mkubwa ukawa umetanda.
“Tukawa tunahangaika kutafuta walau kitambaa cha maji tujifunge ili kuingia kuwaokoa waliokuwa ndani, umeme ukaanza kupiga shoti na tukashindwa namna ya kuwaokoa,” ameeleza.
Shahidi huyo amedai kuwa walizunguka upande wa pili kwenda kuvunja mlango wa nyuma lakini walipofika kwenye mlango huo wa jikoni kuvunja mlango, moto ulikuwa umeshaingia na gesi ikalipuka.
Bibi Mkunde Efatha (85), mkazi wa Kijiji cha Mjimwema, Usariver wilayani Arumeru aliyefariki dunia baada ya nyumba aliyokuwa akiishi na wajukuu zake wawili kuteketea kwa moto.
“Baada ya kusikia kishindo cha gesi tukakimbia na tukawa tumeshapiga simu jeshi la zima moto. Walifanya haraka wakafika mapema na polisi walifika pia. Watu wakaambiwa wakae mbali. Wakazima moto ila tukaingia tukakuta wameteketea wote. Tulishindwa kuwaokoa, walipiga kelele kama mara mbili.
“Mtoto huyo alikuwa anapiga kelele anaita, mkubwa alishindwa kuhema na sehemu waliyokuwa moshi ulikuwa umetanda japo moto haukufika ila shoti ilikwamisha tusiweze kuwaokoa. Bibi kwa umri wake asingeweza kujiokoa, kuna muda alikuwa anapiga kelele anasema nisaidieni muwaokoe hata wajukuu wangu mimi nife tu, lakini moto ukawa mkubwa tukashindwa namna ya kuwaokoa,” amedai.
Shuhuda huyo ameeleza kuwa mtoto wa kiume Jackson alikuwa akipambana kuvunja mlango lakini kutokana na moshi kuwa mkubwa alishindwa kutoka na baada ya moto kuzimwa alikutwa amefariki mlangoni hapo.
Lerato Shaban (11)ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la saba,aliyefariki katika ajali hiyo.
“Mtoto mdogo alikuwa mlangoni anataka kumfuata bibi chumbani naye alifia hapo na bibi tumemkuta ameungulia kitandani, miili yao imeisha kabisa. Kiukweli ni tukio linalosikitisha sana.”
Kwa upande wake, mtoto wa marehemu, Neema Msuya, ameeleza kuwa kama familia wamepata pigo kubwa ambapo amesema binti yake alikuwa anasoma darasa la saba katika Shule ya Msingi Amani na kuwa Jackson ni mtoto wa kaka yake.
“Kwa kweli tunasikitika tu na ukweli ni kwamba ni kwa mapenzi ya Mungu hakuna cha kuongea sana ila tunaomba watu tushirikiane kwa ajili ya kumaliza hili suala na mapenzi ya Mungu yatimizwe. Mtoto wangu Lerato alikuwa kipenzi cha bibi ndiyo maana sikumchukua, nilimwacha aishi na bibi kwa sababu bibi anampenda sana. Akaendelea kukaa naye, ningemchukua labda baada ya kumaliza darasa la saba na kumpeleka sekondari.”
Sehemu ya mabaki ya nyumba ikiyoteketea kwa moto katika Kijiji cha Mjimwema,Usariver wilayani Arumeru ambapo kutokana na moto huo wamefariki watu watatu wa familia moja akiwemo bibi na wajukuu zake wawili. Picha na Janeth Mushi
Kamanda wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji Mkoa wa Arusha, Oswald Mwanjegele, akizungumzia tukio hilo amesema chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana.
“Kimsingi mpaka dakika hii chanzo hakijabainika lakini ilikuwa ni jana tulipokea taarifa kwamba eneo la Usa River kuna tukio la moto kwenye nyumba ya Mkunde Kitio, alikuwa huko ndani na watu wengine wawili.
“Moto uliwaka, nyumba nzima ilishika moto. Kwa dalili zinavyoonyesha moto ulianzia sebuleni. Kwa hiyo moto ukawa umewazingira, wakawa wanapiga kelele kuomba msaada kwa majirani. Majirani wakaendelea kupambana na moto na ulipowazidi ikabidi wapige simu zima moto,” amesema.