
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, ameamuru kuondolewa kwa wanajeshi wapatao 5,000 kutoka Ujerumani ndani ya mwaka mmoja, wakiwakilisha takriban 15% ya wanajeshi waliopo, Pentagon imetangaza siku ya Ijumaa, Mei 1. Licha ya kuondolewa kwa wanajeshi hao, zaidi ya wanajeshi 30,000 wa Marekani watabaki Ujerumani, ambayo inasalia kuwa kituo kikuu cha Marekani barani Ulaya.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Tunatarajia zoezi hilo kukamilika ndani ya miezi sita hadi kumi na miwili ijayo,” msemaji wa Pentagon Sean Parnell alisema katika taarifa. Zaidi ya wanajeshi 36,000 wa Marekani wako Ujerumani, kulingana na hesabu rasmi kufikia mwisho wa mwaka 2025.
Tangazo hili linakuja baada ya Rais Donald Trump mapema wiki hii kufikiria kupunguza wanajeshi wa Marekani waliopo Ujerumani, mshirika wa NATO, kufuatia kauli ya Kansela Friedrich Merz iliyomkasirisha. Siku ya Jumatatu Kiongozi huyo wa Ujerumani alisema kwamba “Marekani haina mkakati wowote” nchini Iran na kwamba Tehran “imeidhalilisha” nchi yenye nguvu duniani.
“Anadhani ni sawa kwa Iran kupata silaha za nyuklia. Hajui anachozungumzia!” Donald Trump alijibu kwa hasira siku ya Jumanne. Siku iliyofuata, rais wa Marekani aliandika kwamba Washington “inasoma na kuchunguza uwezekano wa kupunguzwa” kwa uwepo wa kijeshi wa Marekani nchini Ujerumani. “Uamuzi utafanywa hivi karibuni,” aliongeza. Kambi za Ujerumani zinajulikana kuwa muhimu kwa shughuli nchini Ukraine na Mashariki ya Kati. Zimekuwa muhimu sana kwa ajili ya vifaa vya mashambulizi nchini Iran, anaandika mwandishi wetu nchini Marekani, Vincent Souriau.
Kupunguzwa kwa wanaeshi wa Marekani pia kutangazwa nchini Italia na Uhispania
Donald Trump anawakosoa sana washirika wa Marekani wa Ulaya kwa kusita kwao kuchangia vifaa au wanajeshi katika mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya Iran au kulinda Mlango-Bahari wa Hormuz, ambao karibu umefungwa na Tehran. Kwa upana zaidi, katika mihula yake miwili, rais huyo wa Maekani kutoka chama cha Republican amekuwa akikosoa mara kwa mara nchi za Ulaya kwa kile anachokiona kama ukosefu wa kujitolea kwa ulinzi wao wenyewe, na NATO, ambayo anaishutumu kwa kutegemea sana ulinzi wa kijeshi wa Marekani. Mara kwa mara anangeza tishio la kujiondoa kwa Marekani.
Mbali na Ujerumani, Donald Trump alisema siku ya Alhamisi kwamba pia alikuwa akifikiria kupunguza vikosi vya Marekani nchini Italia na Uhispania, tena dhidi ya historia ya vita nchini Iran. “Labda, labda nitafanya hivyo. Kwa nini nisifanye hivyo?” alijibu katika Ofisi ya Oval ya White House, alipoulizwa kuhusu uwezekano huu. “Italia haikuwa na msaada wowote, na Uhispania ilikuwa na chuki, chuki kabisa,” alisema.
Mwishoni mwa mwaka 2025, Italia ilikuwa na wanajeshi 12,662 wa Marekani walio na wajibu wa kufanya kazi na Uhispania 3,814, kulingana na takwimu rasmi. Umoja wa Ulaya ulisisitiza siku ya Alhamisi kwamba uwepo wa wanajeshi wa Marekani barani Ulaya “pia unatumiwa kwa maslahi ya Marekani katika shughuli zake za kimataifa.”