Dar es Salaam. Akiwa na umri wa miaka 25 tu, Latricia Ian ameandika historia yake katika ulimwengu wa mitindo na urembo nchini Tanzania. Baada ya kuwa mrembo atayeiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya urembo duniani yatayofanyika Vietnam kuanzia Agosti 9 hadi Septemba 5, 2026.
Mrembo huyu mzawa wa Kilimanjaro ambaye ni Miss World Tanzania wakati akizungumza na Mwananchi amefichua kuwa safari yake kwenye urembo ilianza tangu akiwa mdogo alipokuwa akihamasishwa na wazazi wake kutembea catwalk.
“Mimi ni Mchaga. Nilianza kitambo kupenda urembo tangu nipo O-Level ndio nilianza kushiriki kwenye majukwaa. Lakini tangu nikiwa mdogo wazazi wangu walikuwa wananiambia nifanye catwalk,” anasema.
Latricia anasema mara ya kwanza kushiriki kwenye mashindano ya urembo ilikuwa wakati anasoma Kibosho Girls Secondary School, ambapo mwaka 2019 alishiriki shindano la Miss Kibosho.
“Nilipofika O-Level ndio nikashiriki Miss Kibosho maana nimesoma Kibosho Girls,” anasema.
Hata hivyo safari yake haikuishia hapo kwani alipoendelea na masomo ya juu Institute of Accountancy Arusha (IAA) akisomea Banking and Finance, alishiriki tena kwenye mashindano na kunyakua taji.
“Nilivyotoka hapo Kibosho nikaingia kushiriki chuo. Nilikuwa nasoma IAA. 2024 nikiwa mwaka wa tatu tukafanya mashindano nikashinda.
“Kisha nikaanza kusikia kuna kitu kinaitwa Miss Higher Learning, mashindano ya vyuo vikuu. Chuo changu kikanisapoti kwa upande wake. Nikashiriki na nikashinda tena,”anasema
Hatahivyo, safari yake kuelekea Miss Tanzania ilikwama kwa muda baada ya mashindano hayo kutofanyika kwa miaka kadhaa nchini.
“Safari ya Miss Higher Learning ilikuwa inafikia Miss Tanzania lakini kwa kipindi hicho miaka yote miwili haikufanyika 2024 na 2025,” anasema
Ilipofika mwaka huu 2026 ndipo fursa mpya ilipojitokeza kupitia mashindano ya Miss World Tanzania. Latricia aliamua kujaribu tena bahati yake.
“Katika mwaka huu 2026 ikaja Miss World Tanzania nikajiingiza tena kwenye mashindano ambayo nayo yanalazimu kuanzia kwenye kanda,” anasema.
Kwa kuwa tayari alikuwa mshindi wa Miss Higher Learning, alishiriki katika hatua ya Dar es Salaam Zone na kushika nafasi ya pili.
“Nikaenda Dar es Salaam Zone nikawa Second Runner kisha tukachukuliwa sisi wanne kwenda Miss World hadi kuwa mshindi,” anasema.
Kwa mujibu wa Latricia, mashindano hayo yalikuwa na ushindani mkubwa.
“Mashindano yalikuwa magumu. Kila mashindano ninayoenda huwa nasema ni magumu lakini hili lilizidi kwa ugumu kwa sababu tulikuwa wasichana 20 na wote tulikuwa vizuri na wengi ni washindi kutoka kwenye zone zao,” anasema.
Hata hivyo, aliweka malengo yake mbele ya Mungu kabla ya fainali.
“Nakumbuka nilimwambia Mungu kwamba nikifanikiwa kuingia kumi bora nitafanya jitihada kupata taji,” anasema.
Aidha anasema tofauti na mashindano mengine aliyowahi kushiriki, kambi ya Miss World Tanzania ilikuwa na mafunzo mengi yenye kujenga.
“Kwenye mashindano mengine tulikuwa tunafundishwa namna ya kutembea na cha kufanya jukwaani. Lakini kwenye haya tulikuwa na madarasa mengi namna ya kuongea, afya, BASATA na mambo mengine mengi,” anasema.
Ameongeza kuwa walikuwa wanapata mafunzo karibu siku nzima.
“Ilichukua kama wiki nzima tunaingia darasani na kutoka jioni, tunakuwa na masomo kama matano. Kisha jioni ndio tunaanza kufanya dancing na namna ya kutembea na hilo lilikuwa jambo zuri sana,” anasema.
Latricia amesema pamoja na msaada wa familia, bado ilibidi ajitahidi kuwashawishi wazazi wake kuelewa ndoto yake.
“Kwanza ni kumshawishi mzazi mpaka aelewa. Wazazi wangu walikuwa wananisapoti sana tangu awali, jambo lilikuwa ni kuwashawishi kwa ninachokitaka na nitakitumiaje kwa njia nzuri,” anasema.
Changamoto nyingine pia ilikuwa uwa upande wa fedha.
“Mimi napenda kujitegemea kuliko kutegemea mtu, hivyo ilinifanya nifanye kazi ili nijisapoti kwenye safari yangu,” amesema.
Baada ya kuhitimu mwaka 2024, alifanya kazi katika kampuni ya uzalishaji nafasi ya Finance Manager kwa mwaka mmoja.
Anasema tangu ashinde taji la Miss World Tanzania, maisha yake yamebadilika kwa kiasi kikubwa.
“Maisha yamebadilika kwa kiwango kikubwa. Popote ninapoenda watu wanageuka kushangaa, nimekuwa mtu wa ndani,” anasema.
Amesema hata mambo yake ya kawaida sasa anayafanya kwa tahadhari.
“Natamani hata kwenda Kariakoo lakini kwa sasa siwezi,” anasema.
Hata hivyo anaona umaarufu huo kama fursa ya kufikisha ujumbe kwa watu wengi.
“Kikubwa nimepata uwezo wa kufikia watu naweza kuzungumza na watu na ujumbe ukawafikia wengi,” anasema.
Latricia ambaye ni Miss World Tanzania anakiri kuwa amekutana na maoni hasi mitandaoni, lakini hayamkatishi tamaa.
“Komenti mbaya nimekutana nazo ingawa sio nyingi sana. Wapo wanaosema vibaya lakini sitaki zikae kwenye akili yangu kwa sababu zitaniathiri,” amesema.
Ameongeza kuwa yeye ni mtu wa kusamehe.
“Mimi ni mtu ambaye muda wote nasamehe,” amesema.
Maandalizi ya Miss World Vietnam
Kwa sasa Latricia anajiandaa kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Miss World yatakayofanyika Vietnam.
“Nimejipanga vizuri kwa Vietnam nikianza na project yangu. Nakutana na designer na watu wa public speaking, nina madarasa mengi ya kujenga uwezo na ratiba yangu imejaa,” amesema.
Mashindano hayo yatachukua siku 28, hivyo kwa upande wake maandalizi ya mavazi ni jambo la muhimu.
“Tutakuwa na siku 28 kwa hiyo nitakuwa na nguo za siku zote na nitatumia designer wa ndani,” anasema.
Akizungumza kuhusu mavazi ambayo hawezi kuvaa kamwe amesema, “Miss World sisi hatuvai mavazi ya utupu, hata mimi pamoja na familia yangu hatufanyi hivyo,” amesema.
Kwa sasa amesema uzito wake ni kilo 52 huku akisisitiza jamii kuwa na tabia ya kufanya mazoezi kwa ajili ya kulinda afya na mwonekano.
“Mimi nakula sana lakini mwili haunenepi, nikiongezeka sana nimefika kilo 55,” amesema.
Mtazamo kuhusu mahusiano
Kuhusu mahusiano, Latricia amesema anathamini heshima.
“Mwanaume ambaye ananiambia siwezi kufanya kitu kwa sababu mimi ni mwanamke siwezi kuwa naye. Mimi nataka kusikilizwa na kuheshimiwa,” anasema.
Anasema pia pesa au mwonekano sio kigezo cha mapenzi kwake.
“Mambo ya mwonekano au pesa sio kigezo, unaweza kuwa na pesa lakini ukawa huna furaha,” amesema.
Utakumbuka Latricia alinyakua taji la Miss World Tanzania Aprili 19, 2026 nakuondoka na zawadi mbalimbali ikiwamo gari aina ya Mercedes-Benz A-Class lenye thamani ya zaidi ya Sh40 milioni. Kitita cha fedha taslimu Sh10 milioni, bima ya safari pamoja na taji la ushindi, huku jumla ya thamani ya zawadi zote ikifikia zaidi ya Sh100 milioni.