Njombe. Wanachama sita wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (Jowuta), akiwemo Mhariri wa Gazeti la Mwananchi, Tamali Vullu, wametunikiwa hati ya mfanyakazi bora ya mwaka 2025/26.

Tuzo hizo zilitolewa jana katika sherehe za Mei Mosi kitaifa zilizofanyika kitaifa mkoani Njombe ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais Samia Hassan Suluhu.

Katika tuzo hizo, Jowuta iliwatangaza Idda Mushi mwandishi wa habari kutoka kituo cha ITV na Radio One  na Lucy Ngowi wa Gazeti la Mfanyakazi kuwa washindi wa kitaifa.

Mshindi wa kitaifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (Jowuta), Idda Mushi, akipokea tuzo kutoka kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika kitaifa mkoani Njombe.

 Mhariri Msanifu wa Gazet la Mwananchi, Tamali Vullu na Alfred Zacharia wa The Respondent wakitangazwa kuwa washindi kwa Mkoa Dar es Salaam.

Wengine waliotangazwa katika tuzo hiyo ni Ashura Kazinja wa Mtanzania Digital na Rashid Mtagaluka wa Gazeti la Pambazuko ambao wameshinda kwa Mkoa wa Morogoro.

Baada ya kukabidhi tuzo hizo kwa washindi pamoja na mambo mengine Rais  Samia, aliwataka kuendelea kuchapa kazi ili kulijenga Taifa.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (Jowuta), Musa Juma, akiwapongeza washindi wa kitaifa wa chama hicho, Lucy Ngowi (kushoto) na Idda Mushi, baada ya kutangazwa kwa ushindi wao.

Akizungumzia tuzo hizo, Mwenyekiti wa Jowuta, Mussa Juma amesema Jowuta mwaka huu imeshiriki kwa mara ya kwanza Mei Mosi na imeweza kutoa zawadi jambo amblo ni fahari kwao.

Kwani mbali ya utoaji zawadi pia waliweza kushiriki vikao vya maandalizi ya sherehe hiyo kwa wafanyakazi hatua ambayo imekifanya chama hicho kuzidi kuheshimika.

“Tunashukuru tukiwa chama kipya kwenye Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), tumeweza kuwatambua na kuwapa zawadi wafanyakazi waliofanya vizuri katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, jambo ambalo vyama vingine vimekuwa vikilifanya hilo kila mwaka.

“Hata hivyo mwakani tumejipanga  kuongeza zawadi kwa wanachama  katika mikoa mingine ili kutambua michango yao,” amesema.

Washindi wa tuzo ya Mfanyakazi Bora wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (Jowuta) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi pamoja na wanachama wa chama hicho, wakati wa sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi).

Ukiacha zawadi, pia amesema wana mpango wa kutoa mafunzo ikiwepo masuala ya Bima ya Afya, kujiwekea akiba, kujua utendaji wa taasisi mbalimbali za umma na binafsi.

Aidha amezishukuru taasisi za Serikali, binafsi na viongozi  mbalimbali ambao wamewezesha kwa namna moja katika kufanikisha mchakato huo.

Juma amezitaja taasisi hizo kuwa ni pamoja na ofisi ya Waziri Mkuu na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *