
Ukatili uliopangwa unaofanywa na walowezi Waisraeli dhidi ya Wakristo na jamii zisizo za Kiyahudi katika mji wa al-Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu umeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na kituo cha habari cha QNN siku ya Jumapili, Mratibu wa Ofisi ya Uhusiano ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni (WCC) katika mji wa al-Quds, Youssef Daher, ameonya kuwa vitendo vya ukatili vinavyofanywa na walowezi dhidi ya Wakristo na jamii zisizo za Kiyahudi katika mji huo mkuu wa Palestina uliotekwa na Israel ni sehemu ya sera ya kimfumo yenye ajenda ya wazi ya kuwafukuza wasio Wayahudi.
Daher amesisitiza kuwa shambulio la hivi karibuni dhidi ya mtawa wa kike kutoka Ufaransa halikufanywa na “mtu mwenye matatizo ya akili” wala halikuwa tukio la bahati mbaya. Mshambuliaji huyo alikuwa akishikilia nafasi ya uongozi kama mkuu wa chama kimoja cha Israel, jambo ambalo Daher anasema linaashiria mwelekeo uliopangwa wenye lengo la kuwasukuma nje ya mji watu wasio Wayahudi.
Amelitaja tukio hilo kuwa kitendo cha kigaidi kinachovuka mipaka ya tabia ya mtu mmoja na kuwakilisha jaribio la kimfumo la kuwatisha Wakristo. Ameongeza kuwa vitisho vinavyozidi kuongezeka sasa vinawalazimisha Wakristo katika al-Quds, wakiwemo wenyeji na wageni, kuishi kwa tahadhari ya kudumu na hofu ya mashambulizi ya ghafla.
Daher ameonya kuwa hali hiyo sasa inahatarisha usalama wa Wakristo wote, Waislamu na wasio Wayahudi wengine katika mji huo mkuu wa Palestina unaokaliwa kwa mabavu na Israel. Amebainisha kuwa makundi ya walowezi wa Israel yanafanya kazi kama mitandao iliyopangwa ya watu wenye itikadi kali, inayofuata mbinu ya wazi ya dhuluma na ubaguzi dhidi ya watu wasio Wayahudi.
Baraza la Makanisa Ulimwenguni (WCC) na taasisi nyingine zimekusanya takwimu zinazoonyesha ongezeko kubwa la ukatili unaofanywa na walowezi wa Kizayuni. Daher aliripoti takriban mashambulizi 187 katika mwaka wa 2025 pekee, yakiwemo mashambulizi dhidi ya watu binafsi na mali zao. Ameelezea idadi hiyo kuwa rekodi ya juu isiyo na mfano, akibainisha kuwa inaonyesha mabadiliko kutoka matukio ya nadra kuelekea sera iliyopangwa.
Daher pia amelaani mwitikio hafifu kutoka kwa mamlaka na taasisi za kidini za Israel, akisema hatua wanazochukua hazilingani na ukubwa wa ukatili unaoendelea. Amesema hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa kukomesha manyanyaso dhidi ya Wapalestina walio chini ya uvamizi.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot, ametoa wito wa mshambulizi wa mtawa huyo wa Ufaransa huko al-Quds kupewa adhabu kali. Kupitia mtandao wa X, alionyesha huzuni na mshikamano wake na mtawa huyo wa kike na kumtakia nafuu ya haraka baada ya kile alichokiita “shambulio la kushtusha.”