
Wakili maarufu wa Mali na mwanasiasa mkosoaji wa utawala wa kijeshi aliripotiwa kutekwa nyara usiku wa kuamkia Jumapili ya wikendi iliopita na watu waliokuwa wamejifunika nyuso katika mji mkuu Bamako, familia yake imethibitisha.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kutekwa kwake kumekuja wakati huu utawala wa kijeshi ukikabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi tangu uingie madarakani baada ya juma moja lililopita waasi wa Tuareg kwa kushirikiana na wanajihadi wa Kiislamu watekeleze mashambulizi mfululizo kwa lengo la kuangusha utawala uliopo.
Mountaga Tall alikuwa mwanachama wa vuguvugu la M5-RFP, vuguvugu ambalo ndilo lililoandaa maandamano yaliyopelekea kuangushwa kwa utawala wa rais Ibrahim Boubacar Keita mwaka 2020, ambapo baada ya jeshi kuchukua nchi alijitenga nalo na kuwa mkosoaji mkubwa.
Mkewe Tall ambaye alijaribu kuchukua picha wakati mume wake akitekwa, alidhulumiwa na watekaji ambao baadae waliondoka na simu yake na kutokomea kusikojulikana.
Haya yanajiri wakati ambapo siku ya Ijumaa, ofisi ya mwendesha mashtaka ilidai kuwa wanajeshi kadhaa wamekamatwa kwa tuhuma za kushirikiana na wanajihadi hao na waasi wa Tuareg, huku mwanasiasa Oumar Mariko aliyeko uhamishoni pia akitajwa kuhusika.