WAKATI Tanzania Prisons ikijiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba, huku kocha mkuu wa kikosi hicho, Shedrack Nsajigwa akitoa matumaini, hesabu zinaingia na kutoka kwenye mkakati wa kubaki salama.
Prisons ambayo iliwahi kuonja kushuka daraja msimu wa 2011-2012 kabla ya kurudi 2012-2013, imekuwa na mwendelezo usioridhisha kwa misimu kadhaa mfululizo ikijikuta ikiponea chupuchupu kushuka daraja.
Kwa sasa timu hiyo ipo nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 14, ambapo Mei 10 mwaka huu itakuwa kibaruani kuikabili Simba iliyopo nafasi ya pili kwa pointi 43, mchezo ambao utapigwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam.
Katika mechi tisa zilizobaki kwa maafande hao, itakuwa nyumbani tatu dhidi ya Fountain Gate, Dodoma Jiji na Mtibwa Sugar, huku sita ikicheza ugenini ikianza na Simba. Wapinzani wengine ni Azam, Pamba Jiji, JKT Tanzania, Singida Black Stars na Mashujaa.
Nsajigwa ambaye alitua Februari, mwaka huu kuchukua nafasi ya Mkenya Zedekia Otieno hadi sasa ameiongoza michezo minane ikiwamo mmoja wa Kombe la Shirikisho, ambapo hajaonja ushindi akipoteza sita na sare mbili.
Akizungumzia mwenendo wa timu hiyo, Nsajigwa amekiri ugumu wa ligi akieleza kuwa licha ya mabadiliko aliyofanya kwa wachezaji, lakini tatizo kubwa ni makosa binafsi ya mtu mmoja mmoja uwanjani.
Amesema anafahamu mchezo dhidi ya Simba kuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani hao, akieleza kwamba wanahitaji kucheza kwa nidhamu na akili ili kufikia malengo, akitoa matumaini kuwa Prisons haishuki daraja.