
Moshi. Wakati bajaji zikiendelea kufanya biashara kama daladala katikati ya Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, baadhi ya wananchi wamelalamikia kupandishiwa nauli kiholela, hali inayowafanya baadhi ya wananchi wenye kipato cha chini kushindwa kumudu gharama ambazo madereva wa bajaji wamejipangia, na hivyo kulazimika kutembea kwa miguu.
Bajaji hizo, ambazo zimesajiliwa kama chombo cha usafiri wa kukodi, zimegeukia biashara hiyo baada ya kuondolewa kwa daladala katika njia zote za manispaa hiyo, na hivyo wananchi kukosa usafiri mbadala.
Kutokana na kukosekana kwa usafiri wa umma (daladala), wananchi hao wamejikuta wakilazimika kulipa nauli kati ya Sh1,500 badala ya Sh700, na Sh5,000 badala ya Sh3,000 kwa mtu mmoja.
Hayo yanatokea licha ya Serikali kutangaza bei elekezi ya nauli kuanzia Mei mosi mwaka huu, ambapo kwa usafiri wa daladala imeongezeka Sh100, na hivyo kufanya nauli kupanda kutoka Sh600 hadi Sh700 kwa umbali usiozidi kilomita 10.
Awali, wananchi hao walikuwa wakitumia usafiri wa daladala kabla bajaji hazijaingia mjini, na baadaye daladala hizo zilishindwa kufanya usafirishaji kutokana na ushindani uliokuwepo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wameiomba Serikali kuingilia kati hali hiyo, ili kudhibiti bei hizo na kuwatafutia usafiri wa umma (daladala), wakieleza kuwa wanashindwa kumudu gharama za bajaji kutokana na baadhi ya madereva kupandisha nauli.
Germana Joseph, mkazi wa Manispaa ya Moshi, amesema gharama za usafiri wa bajaji zimekuwa kubwa kutokana na kukosekana kwa daladala, hali inayowapa mzigo mkubwa wananchi wenye kipato cha chini.
“Hali imekuwa ngumu, gharama za maisha zimepanda. Ukija kwenye usafiri wa bajaji nao ni pasua kichwa. Fikiria nauli ilikuwa ni Sh700 kutoka mjini hadi Msaranga, baada ya mafuta kupanda, bajaji wametupandishia nauli hadi Sh1,500. Kwa hiyo mwananchi analipa Sh3,000 kila siku kwenda na kurudi. Huu ni mzigo kwetu.
“Kama bajaji zimeamua kufanya usafiri wa umma, kwanini hazizingatii bei elekezi ambayo Serikali imetoa, ambapo imeongezeka Sh100 tu? Kwanini wao wamepandisha nauli mara mbili ya nauli ya awali? Tunaomba Serikali itusaidie, wananchi tunateseka,” amesema mwananchi huyo.
Mwananchi mwingine, Jasmin Ally, mkazi wa Kahe, amesema awali nauli ilikuwa Sh3,000, lakini sasa imepandishwa hadi Sh5,000, akieleza kuwa huo ni mzigo kwa wananchi, hivyo kuziomba mamlaka husika kuingilia kati.
“Bajaji za huku Kahe tunapanda hadi watu sita badala ya watatu, na nauli unalipa hiyo hiyo. Yaani tumepandishiwa nauli kutoka Sh3,000 hadi Sh5,000 kwa mtu mmoja, kwenda na kurudi mjini ni Sh10,000. Huyu mwananchi wa kawaida anapata wapi hii nauli kila siku? Tunahitaji kusaidiwa,” amesema Ally.
Yustela Moshi ameiomba Serikali kuingilia kati na kuangalia namna ya kudhibiti upandishwaji wa nauli hizo kiholela, akisema baadhi yao wanalazimika kutembea kwa miguu kutokana na gharama kuwa kubwa.
“Kila siku kupanda bajaji kwa Sh3,000 huu ni mzigo mkubwa kwangu. Naamka asubuhi na mapema, natoka nyumbani mdogo mdogo kupitia njia za uchochoroni hadi kufika ninakokwenda. Maisha ni magumu sana, ukitoa hiyo hela kila siku, watoto si watakufa njaa?” amehoji mama huyo.
Akizungumzia hilo, mmoja wa madereva wa bajaji wa manispaa hiyo, Ramadhan Mussa, amesema nauli imepanda kutokana na bei ya mafuta kuwa juu pamoja na gharama za uendeshaji.
“Wananchi wanaona bei ya mafuta ilivyopanda, lakini bado wanapiga kelele. Hatuwezi kufanya biashara ya hasara, hivyo ni lazima tupandishe nauli,” amesema dereva huyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bodaboda na Bajaji Manispaa ya Moshi, Hamadi Bendera, amesema suala la kupanda kwa nauli limepokea malalamiko kutoka kwa wananchi, na kwamba watakaa na kuona namna ya kuweka nauli rafiki.
“Juzi hata sisi tulikaa, katibu aliitisha kikao kuhusu kupanda kwa nauli, kuona ni kwa namna gani tunachakata, na tukaagiza viongozi kukaa na kuweka mfumo rafiki. Hata sisi hatupendi hali kama hii kujitokeza,” amesema mwenyekiti huyo.
Kauli ya RC
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amewataka madereva wa bajaji kuzingatia bei elekezi iliyotolewa na Serikali, na kumuagiza Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra) mkoani humo kufuatilia suala la upandaji wa nauli kiholela.
“Mafuta ni kweli yamepanda, lakini kupanda kwa mafuta isiwe kisingizio cha kuwaumiza wananchi. Ndiyo maana Serikali inafanya jitihada kuhakikisha huduma ya mafuta inapatikana nchini.
“Nawaagiza wakuu wote wa wilaya Mkoa wa Kilimanjaro kufuatilia bei elekezi za magari na bajaji zilizotolewa na Latra kama zinatekelezwa kama ilivyopangwa,” amesema Babu.
Alipotafutwa Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafiri Ardhini (LATRA) mkoani humo, Paulo Nyello, amesema wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali kwa bajaji zinazokiuka taratibu.
“Juzi tulifanya operesheni na tulikamata bajaji 385 zenye makosa mbalimbali, ikiwemo kutokuwa na leseni za usafirishaji, kukiuka masharti ya leseni pamoja na mambo mengine,” amesema Nyello.