Dar es Salaam. Tanzania na Uturuki zimeingia makubaliano mapya ya ushirikiano katika sekta muhimu za kimaendeleo hatua inayolenga kuimarisha uhusiano wa muda mrefu uliyonao nchi hizo mbili.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa kufungwa kwa Mkutano wa Kwanza wa Ushirikiano uliofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Mei 4 na kumalizika leo Jumanne, Mei 5, 2026.
Akizungumza baada ya kusaini hati ya makubaliano katika Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki leo jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa amesema maeneo yaliyoguswa ni pamoja na elimu, kilimo, afya, miundombinu, biashara, uwekezaji, fedha, diplomasia, pamoja na ulinzi na usalama.
Balozi Mussa amesema mkutano huo ni hatua muhimu katika kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan na mwenzake wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan, kufuatia mazungumzo ya ngazi ya juu yaliyofanyika wakati wa ziara ya Rais Samia nchini Uturuki mwaka 2024.
“Mkutano huu umetoa jukwaa rasmi la kubadili ahadi hizo kuwa mipango ya utekelezaji, ambapo pande zote mbili zimeonyesha utayari wa kuhakikisha kila jambo linatekelezwa kwa wakati,” amesema Balozi Mussa wakati wa kufunga mkutano huo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa (kulia) na Mkurugenzi Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki anayeshughulikia Kusini mwa Afrika Volkan Işıkcı, kwa pamoja wakionesha hati za makubaliano katika Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki leo Mei 5, 2026 Dar es Salaam.
Hata hivyo, moja ya mafanikio makubwa ya mkutano huo ni kusainiwa kwa mkataba wa kuepuka kutoza kodi mara mbili, hatua inayotajwa kuwa itarahisisha mazingira ya biashara na kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutoka nchi zote mbili.
Amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa haraka wa makubaliano hayo, akionya kuwa ucheleweshaji mara nyingi hurudisha nyuma malengo ya maendeleo yaliyokusudiwa.
Amesema Tanzania bado iko wazi kwa wawekezaji wa Uturuki, hususan katika sekta za kimkakati kama viwanda, kilimo, utalii na miundombinu, huku akihimiza ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki anayeshughulikia Kusini mwa Afrika, Volkan Işıkcı ameelezea utayari wa nchi yake kuendelea kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya Tanzania kupitia ushirikiano wa kudumu.
Işıkcı amesema Uturuki ina nia ya dhati ya kuongeza nguvu katika sekta za afya, elimu, ulinzi, usafirishaji na utamaduni. Aidha, ameimwagia sifa Tanzania kwa ukarimu wake na kusema mkutano huo umezidi kuimarisha urafiki wa muda mrefu uliopo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa (kulia) na Mkurugenzi Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki anayeshughulikia Kusini mwa Afrika Volkan Işıkcı, kwa pamoja wakionesha hati za makubaliano katika Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki leo Mei 5, 2026 Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, Tanzania imekaribisha wawekezaji kutoka Uturuki kuwekeza katika sekta za kimkakati kama viwanda, kilimo, utalii na miundombinu.
Katika kuelekea utekelezaji wa makubaliano hayo, Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Biashara, huku mkutano wa pili wa ushirikiano huu ukitarajiwa kufanyika jijini Ankara, Uturuki, mwaka 2027.