Maswa. Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Anna Gidarya ameitaka jamii kupitia makundi mbalimbali kuhakikisha utoaji wa chanjo ya matone ya polio kwa watoto wenye umri wa miaka 0 hadi 10 unafanikiwa kwa kiwango kikubwa, ili kulilinda kundi hilo dhidi ya ugonjwa huo unaoweza kusababisha ulemavu wa kudumu.

Akizungumza leo Mei 6, 2026 katika kikao cha uhamasishaji wa kampeni hiyo amesema jumla ya watoto 193,943 wanatarajiwa kufikiwa katika zoezi hilo.

Amesema utoaji wa chanjo hiyo ni hatua ya tahadhari kufuatia kubainika kuwepo kwa kirusi kinachosababisha ugonjwa wa polio katika moja ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Kutokana na hali hiyo, amesema Serikali imeamua kutoa chanjo hiyo katika mikoa sita ambayo ni Simiyu, Mara, Mwanza, Geita, Shinyanga na Singida, ili kuzuia uwezekano wa kusambaa kwa ugonjwa huo.

Amesema ili kufanikisha kampeni hiyo, Serikali imeona umuhimu wa kushirikisha makundi mbalimbali ya jamii ili kuhakikisha watoto wote wanaofikiwa wanapatiwa chanjo.

“Niwaombe viongozi wa dini, waganga wa tiba asili na wanasiasa tuungane kwa pamoja katika maeneo yetu kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika kampeni hii ya chanjo ya polio kwa watoto wetu,” amesema.

Gidarya ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Itilima mkoani humo, amesisitiza kuwa chanjo hiyo ni salama na haina madhara yoyote kwa watoto.

Sehemu ya wadau mbalimbali wa sekta ya afya wilaya ya Maswa walioshiriki mkutano wa kampeni ya uhamasishaji wa chanjo ya ugonjwa wa polio kwa watoto chini ya mwaka 0-miaka 10. Picha na Samwel Mwanga

“Chanjo hii haina madhara yoyote kwa mtoto, na hata katika awamu ya kwanza mmejionea. Mtoto hapati maumivu wala kulia anapopewa matone haya,” amesema.

Christopher Msaghee kutoka Wizara ya Afya amesema hadi sasa wilaya ya Maswa imepokea dozi 203,650 za chanjo ya polio ambazo zimesambazwa katika vituo vya afya na zahanati zote wilayani humo.

Naye Ofisa Afya Mkoa wa Simiyu, Bashir Salum amesema kampeni hiyo itatekelezwa kwa mtindo wa nyumba kwa nyumba na itawahusisha watoto wote, wakiwemo waliopata chanjo katika awamu ya kwanza na wale waliokosa.

“Lengo letu la kupita nyumba kwa nyumba ni kuhakikisha watoto wote wenye umri husika wanapatiwa chanjo hii ili kuimarisha kinga dhidi ya ugonjwa wa polio,” amesema.

Baadhi ya wananchi wamepongeza hatua hiyo ya Serikali na kuhimiza ushiriki wa wazazi. Mkazi wa Maswa, Esther Fisoo, amesema kampeni hiyo ni muhimu kwa ustawi wa watoto.

“Tunashukuru Serikali kwa kutujali. Nawashauri wazazi wote kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo hii muhimu,” amesema.

Naye Milembe Jagadi amesema ugonjwa wa polio ni hatari kwa kuwa unaweza kusababisha kupooza kwa mtoto, hivyo chanjo ni kinga muhimu.

“Ni ugonjwa hatari sana. Hakuna mzazi anayependa kuona mtoto wake anapooza, hivyo chanjo hii ni muhimu sana,” amesema.

Mratibu wa Chanjo kutoka Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania, Boniface Mabonesho amesema taasisi hiyo inashirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa.

Amesema timu za wahudumu wa afya zimeandaliwa kuwafikia watoto katika vituo vilivyopangwa pamoja na ngazi ya jamii ili kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa chanjo.

Kampeni hiyo ya chanjo ya matone ya polio itafanyika kwa siku nne, kuanzia Mei 7 hadi 10, 2026, katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Maswa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *