
Dar es Salaam. Wakati mwili wa James Temba (24) ukitarajiwa kuzikwa Moshi mkoani Kilimanjaro, rafiki, majirani na mwinjilisti wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wamezungumzia tukio hilo, huku Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Tahaliso) ikitaka uchunguzi wa kina.
Temba, aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), aliondoka nyumbani kwao Aprili 29 mwaka huu na baadaye mwili wake kukutwa katika Mto Msimbazi, jijini Dar es Salaam, ukielea ndani ya maji, huku ukiwa umekatwa kichwa.
Mei 3 mwaka huu, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam lilithibitisha kifo cha Temba na kueleza kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha kifo hicho, na watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumzia tukio hilo leo, Jumanne, Mei 5, 2026, rafiki wa Temba, Alex Christopher, amesema waliishi naye katika nyumba moja na kwamba hakuwa na tatizo na yeyote.
Kila siku kabla ya kwenda chuo, amesema walijuliana hali hadi Aprili 29, mwaka huu alipotoweka. Alimpigia simu mara kadhaa, iliita bila kupokelewa na baadaye ilizima.
Siku iliyofuata, amesema wazazi wake walikwenda kuripoti kituo cha polisi na ndipo walipewa taarifa ya kupatikana mwili uliokatwa kichwa.
Pamoja na wazazi kutambua mwili ule kuwa ni wa James, Alex amesema hakukubali mapema.
“Tulioneshwa video, nilikataa kwa sababu mwili wake ulionekana mpana na hakuwa hivyo. Nilimtafuta bodaboda wangu, nikaanza kuzunguka naye kwenda kwa marafiki zake wanaomfahamu, sikufanikiwa. Baadaye nilifuatwa tena na kuelezwa, lakini sikukubali. Niliamini atarudi,” amesema.
Alex amesema baada ya muda aliridhia taarifa zile baada ya kumsubiri rafiki yake kurejea bila mafanikio.
“Hakuwa na biashara yoyote, hana gari wala usafiri wowote, anapanda daladala na si mtu wa starehe. Kifo chake ni cha kikatili sana, adhabu hii ni kubwa mno, hata jambazi hukumu hiyo hapewi. Hii ni zaidi ya kisasi,” amesema.
Rogers Temba, baba mzazi wa mwanafunzi huyo amesema uchunguzi dhidi ya kifo cha mwanawe unaendelea polisi, huku akieleza kuwa maziko yatafanyika Alhamisi, Mei 7 Old Moshi, mkoani Kilimanjaro.
“Mwili utatolewa Hospitali ya Polisi Barracks kesho, Mei 6, 2026, na ibada itafanyika Kanisa la KKKT Tabata Magengeni, na baadaye mwili kusafirishwa kwenda Kilimanjaro kwa maziko Mei 7, 2026,” amesema.
Mwinjilisti
Katikati ya simanzi hiyo, Mwinjilisti wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mtaa wa Mchimbo, Exaud James, ambaye ni mlezi wa kiroho wa James, amesema hakuna anayeamini kama kijana huyo alikuwa na maadui wakubwa kiasi hicho.
Amesema James alikuwa mwema na alihudhuria ibada siku zote na matukio mengine kanisani, jambo lililothibitisha mwenendo wake mzuri na imani kwa Mungu.
Amesema James hakuwa mwimbaji wa kwaya, na hiyo ni kutokana na masomo yake, lakini hakukosa matukio mengine ya ibada.
“Tukio hili lilipotokea tumejiuliza kwa nini James, kwa nini hivyo. Hatukutegemea angekuwa na maadui wakubwa namna hiyo, kwa sababu ya mwenendo wake kanisani ni kijana anayempenda Mungu,” amesema.
Amesema vijana ni Taifa la sasa na kesho, hivyo jamii inapaswa kuwalinda, akipinga suala la umwagaji damu ya mtu, akieleza kuwa damu haifi.
“Hakuna jambo baya kama kumwaga damu ya mtu, huwa haifi. Mwanzo 4, Kaini alimuua ndugu yake Abili, na Mungu alipomuuliza yuko wapi ndugu yake, alijibu yeye si mlinzi wake, na Mungu akamwambia damu ya ndugu yako inakulilia toka kwenye ardhi,” amesema.
Amesema damu ya mtu haifi, na inapomwagika hudai malipizi ardhini hadi imwagike damu nyingine.
Jirani wasema haya
Jirani wa James, Vumilia Samwel, amesema kifo hicho ni cha kinyama na Serikali ichukue hatua kali kwa wahusika.
“Sijui ni kosa gani hili kubwa hadi mtu akatwe kichwa, huu ni unyama mkubwa sana. Kijana wa watu hakuwa na tatizo, alikuwa mkimya,” amesema.
Kwa upande wake, Vincent Masawe amesema Serikali inapaswa kulinda wananchi wake, kwani matukio ya mauaji na kupotezwa kwa watu yanaongeza hofu kwenye jamii.
TAHLISO yasisitiza uchunguzi
Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), Geofrey Kiliba, kupitia mtandao wake wa Instagram ametoa salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wanafunzi wa IFM kutokana na msba huo.
“Tukio hili hakika limegusa mioyo yetu sote kama jamii ya wanafunzi wa vyuo na Watanzania kwa ujumla. Ni tukio ambalo tumelichukulia kwa uzito mkubwa.
“Kwa niaba ya Tahliso, ninaliomba Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi wa kina na wa haraka ili wahusika wa tukio hili wabainike na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria,” imeeleza taarifa hiyo.
Kiliba, kupitia taarifa hiyo, amewasihi wananchi kutoa ushirikiano wa dhati kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa yoyote itakayosaidia kufanikisha uchunguzi wa tukio hilo.