Dar es Salaam. Wadau wa maendeleo ya mtoto nchini Tanzania wameongeza msukumo katika kuimarisha malezi ya awali ya mtoto (ECD) yanayozingatia usawa wa kijinsia, wakisisitiza umuhimu wa kuziba pengo lililopo kati ya sera na utekelezaji wake katika ngazi ya jamii.

Hatua hiyo imekuja kufuatia semina ya siku tatu iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Aga Khan kupitia Taasisi yake ya Maendeleo ya Binadamu kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu ya Maendeleo Afrika Mashariki (IED, EA), iliyofanyika jijini Arusha.

Akizungumza katika semina hiyo, Kaimu Mkuu wa Utafiti wa IED, EA, Dk Fortidas Bakuza amesema bado kuna changamoto kubwa katika kuhakikisha sera nzuri zilizopo zinatafsiriwa katika vitendo vinavyoonekana katika jamii.

“Tunachokiona sera zipo na zimeandaliwa vizuri, lakini utekelezaji wake bado haujaimarika vya kutosha. Kupitia mafunzo haya, tunalenga kujenga wataalamu wenye uelewa wa kina ambao watahakikisha sera hizi zinatekelezwa ipasavyo,” alisema.

Aliongeza kuwa mabadiliko ya kweli katika malezi ya mtoto hayawezi kupatikana bila kuunganisha juhudi za sera na uelewa wa jamii.

Kwa upande wao, washiriki walisisitiza umuhimu wa kubadili mitazamo ya kijamii inayochangia kuwepo kwa mgawanyo usio sawa wa majukumu ya malezi ya mtoto, hasa kwa upande wa wazazi.

Mmoja wa washiriki Odo Ndonde, alisema ni wakati sasa jamii ikubali mabadiliko ya kijamii na kiuchumi yanayohitaji ushiriki wa wazazi wote wawili katika malezi ya mtoto.

“Katika baadhi ya jamii, bado kuna imani kuwa malezi ya mtoto ni jukumu la mama pekee. Hii si sahihi tena katika mazingira ya sasa. Tunahitaji kuhamasisha ushiriki wa baba ili mtoto apate malezi bora zaidi,” alisema.

Wadau hao pia waligusia changamoto zinazowakabili watoto wenye ulemavu, wakieleza kuwa bado wanakumbwa na ubaguzi unaotokana na mitazamo hasi ya kijinsia na kijamii, hali inayodhoofisha fursa zao za maendeleo tangu wakiwa wadogo.

Kwa mujibu wa wataalamu, malezi ya awali ya mtoto ni hatua muhimu katika kujenga msingi wa maendeleo ya baadaye, na hivyo kuzingatia usawa wa kijinsia katika hatua hii kuna mchango mkubwa katika kupunguza ukosefu wa usawa katika jamii.

Chuo Kikuu cha Aga Khan kimetoa wito kwa wadau mbalimbali ikiwemo serikali, mashirika ya kiraia na sekta binafsi kuongeza juhudi katika kuendeleza Ajenda ya Maendeleo Endelevu, hususan Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), kwa kuzingatia zaidi Lengo namba 5 linalohusu usawa wa kijinsia.

Kwa ujumla, wadau walikubaliana kuwa bila mabadiliko ya kimtazamo katika jamii na uwekezaji wa makusudi katika utekelezaji wa sera, jitihada za kufanikisha malezi bora ya mtoto zitaendelea kukwama, huku watoto wengi wakikosa fursa sawa za kukuza vipaji vyao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *