Dar es Salaam. Kwa zaidi ya miaka sita, Raymond Yunus (38) aliishi na maumivu makali ya kiungulia. Kila alipokula, chakula kilirejea kifuani na kumletea hali ya kuungua (kiungulia) isiyovumilika.
Alizunguka hospitali mbalimbali, akipewa dawa za kupunguza tindikali ya tumbo, lakini nafuu ilikuwa ya muda mfupi. “Sikuamini kama kuna siku nitaweza kula bila maumivu,” anasema na kuongeza; “Nilishazoea kuishi na hali hiyo.”
Lakini maisha yake yalibadilika ndani ya saa chache baada ya kufanyiwa upasuaji wa kisasa unaofahamika kama upasuaji wa matundu (Laparascopy).
Tofauti na upasuaji wa kawaida unaohitaji kufungua tumbo kwa mshono mkubwa, yeye alifanyiwa matundu madogo yaliyomwezesha kutibiwa bila kovu kubwa.
Daktari bingwa wa upasuaji kwa njia ya matundu kutoka Hospitali ya CCBRT, Elias Chrisant (wa kwanza kushoto) akimfanyia mgonjwa upasuaji wa matundu maarufu (Laparascopy)
“Kesho yake asubuhi niliamka nikanywa maji, nikala bila shida. Kiungulia kilikuwa kimeisha kabisa,” anasema kwa mshangao.
Raymond mkazi wa Jiji la Dar es Salaam ni miongoni mwa wagonjwa wachache nchini wanaonufaika na teknolojia hiyo mpya ya kitabibu ambayo wataalamu wanasema ina uwezo wa kubadili kabisa namna upasuaji unavyofanyika Tanzania.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu Jumatatu Mei 4, 2026, Daktari bingwa wa upasuaji kwa njia ya matundu kutoka Hospitali ya CCBRT, Elias Chrisant anasema hiyo ni njia ya kisasa inayotumia matundu madogo badala ya kufungua tumbo lote.
“Upasuaji wa matundu ni mbinu ya kisasa, tunatumia matundu madogo sana kuingiza vifaa maalumu pamoja na kamera inayotusaidia kuona ndani ya mwili kama jicho letu.
“Badala ya mshono mkubwa, mgonjwa hubaki na alama ndogo sana, karibu sawa na tundu la penseli.”
Dk Chrisant anasema katika upasuaji huo, madaktari hutengeneza matundu madogo kwenye tumbo la mgonjwa, kisha huingiza vifaa maalumu vyenye upana mdogo na kamera inayorusha picha kwenye skrini.
“Picha zinakuwa wazi na zinatusaidia kuona vizuri tishu za ndani na kufanya upasuaji kwa usalama zaidi,” anafafanua.
Teknolojia hiyo hutumika kutibu magonjwa mbalimbali ya ndani ya tumbo.
Miongoni mwa magonjwa hayo ni mawe kwenye mfuko wa nyongo, henia (udhaifu wa ukuta wa tumbo), uvimbe wa utumbo mpana, uvimbe kwenye kizazi, pamoja na tatizo la kidole tumbo.
Pia, hutumika kufanya uchunguzi wa kina kwa wagonjwa ambao vipimo vingine havijatoa majibu sahihi.
“Kuna wakati mgonjwa amefanya vipimo vingi bila kupata majibu ya uhakika. Hapo tunaweza kutumia upasuaji wa matundu kama njia ya uchunguzi,” anasema.
Faida zake kwa mgonjwa
Tofauti kubwa kati ya upasuaji wa kawaida na huu wa matundu anasema iko wazi katika maumivu, muda wa kupona na gharama za baadaye.
“Faida kubwa ni kwamba mgonjwa anakuwa na maumivu kidogo sana au wakati mwingine hana kabisa,” anasema Dk Chrisant.
“Muda wa kukaa hospitali unapungua kwa kiasi kikubwa. Mgonjwa anaweza kufanyiwa upasuaji asubuhi na jioni anarudi nyumbani, au kesho yake asubuhi anaruhusiwa.”
Anasisitiza kuwa, hali hiyo humwezesha mgonjwa kurejea kwenye shughuli zake za kila siku haraka, tofauti na upasuaji wa kawaida unaohitaji wiki kadhaa za mapumziko.
“Kwa mtu anayefanyiwa upasuaji mkubwa, anahitaji muda mrefu wa kupona. Lakini kwa upasuaji wa matundu, anakuwa na kovu dogo na muonekano mzuri, jambo ambalo lina umuhimu pia kwa wagonjwa wengi,” anaeleza.
Gharama halisi
Ingawa gharama za upasuaji wa matundu zinaweza kuonekana kubwa, Dk Chrisant anasema ukweli ni kwamba zinaweza kuwa nafuu zaidi ukitazama kwa mtazamo mpana.
Daktari bingwa wa upasuaji kwa njia ya matundu kutoka Hospitali ya CCBRT, Elias Chrisant (kushoto) akitoa huduma hiyo kwa mgonjwa
“Watu wanaweza kuona gharama ya upasuaji wa matundu ni kubwa, lakini ukijumlisha gharama za kuuguza kidonda, kukaa hospitali muda mrefu, kushindwa kufanya kazi na kupoteza kipato unaweza kukuta umetumia zaidi kuliko ulivyodhani,” anasema.
Anabainisha kuwa katika Hospitali ya CCBRT, wagonjwa wengi wanahudumiwa kupitia bima za afya ambazo huchangia kwa kiasi kikubwa gharama za matibabu.
Je, kuna hatari?
Kama ilivyo kwa aina nyingine yoyote ya upasuaji, upasuaji wa matundu nao una hatari zake, ingawa kwa kiwango kidogo.
“Kila upasuaji una riski zake. Inaweza kutokea changamoto ya kifaa au hali ya mgonjwa kubadilika wakati wa upasuaji, na tukalazimika kubadilisha mbinu na kufanya upasuaji wa kawaida,” anaeleza Dk Chrisant.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa, faida zake ni nyingi zaidi kuliko hasara.
Akizungumzia maandalizi ya upasuaji wa matundu, anasema hayana tofauti kubwa na yale ya upasuaji wa kawaida. Wagonjwa wengi hutakiwa kutokula kabla ya upasuaji ili kuepuka hatari ya kutapika wakati wa usingizi wa dawa.
“Tunapomuweka mgonjwa kwenye usingizi, anakuwa hawezi kupumua mwenyewe, hivyo mashine humsaidia. Kama atatapika, kuna hatari ya chakula kuingia kwenye njia ya hewa,” anafafanua.
Changamoto zinazoikabili huduma hii
Licha ya faida zake, huduma ya upasuaji wa matundu bado inakabiliwa na changamoto kadhaa nchini ikiwamo uhaba wa wataalamu wenye ujuzi wa mbinu na gharama za vifaa.
“Si kila daktari anapata mafunzo haya, na hata akipata, anahitaji timu nzima yenye ujuzi wakiwamo wauguzi na wataalamu wa usingizi. Bila timu, huduma haiwezi kutolewa,” anasema.
Aidha, vifaa vinavyotumika ni vya kisasa na vinahitaji uwekezaji mkubwa, jambo linalofanya huduma hii kupatikana zaidi katika hospitali za mijini.
Ushuhuda wa wagonjwa
Dk Chrisant anatoa mfano wa mgonjwa aliyekuwa akisumbuliwa na kiungulia kwa zaidi ya miaka sita bila mafanikio ya tiba.
Katika tukio jingine, mgonjwa mwenye henia alifanyiwa upasuaji na siku iliyofuata alishangaa kuona uvimbe umetoweka bila kuwa na kidonda kikubwa.
“Wagonjwa wengi wanashangaa kwa sababu hawategemei matokeo ya haraka kiasi hicho,” anasema.
Nani anafaa kufanyiwa?
Si kila mgonjwa anaweza kufanyiwa upasuaji wa matundu. Uamuzi hutegemea aina na ukubwa wa tatizo.
“Kuna wagonjwa wenye uvimbe mkubwa sana, mfano wa ukubwa wa kichwa cha mtoto, hawawezi kufanyiwa kwa njia hii. Tunafanya tathmini ya kina kabla ya kutoa uamuzi,” anafafanua.
Hata hivyo, anabainisha kuwa watoto, vijana na wazee wanaweza kufanyiwa upasuaji huu iwapo watakidhi vigezo.
Kwa sasa, idadi ya hospitali zinazotoa huduma hii bado ni ndogo, na wagonjwa wanaofanyiwa ni wachache ukilinganisha na wanaofanyiwa upasuaji wa kawaida.
Hata hivyo, matumaini ni makubwa. “Ninaona hii ni teknolojia inakua kwa kasi. Madaktari wengi sasa wanajitahidi kujifunza, na taasisi kama CCBRT tunatoa mafunzo kwa wataalamu wengine,” anasema Dk Chrisant.
Anatoa rai kwa Serikali na wadau kuwekeza zaidi katika mafunzo na vifaa ili huduma hii iwafikie Watanzania wengi zaidi, hasa katika hospitali za mikoa.
“Katika nchi zilizoendelea, hii ndiyo njia ya kwanza ya upasuaji wa magonjwa ya tumbo. Ni wakati sasa na sisi tukaiendeleza,” anasisitiza.
Akitoa rai kwa jamii, Dk Chrisant anashauri wananchi kujenga utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya mapema badala ya kusubiri hali kuwa mbaya.
“Kadri unavyowahi kugundua tatizo, ndivyo unavyoongeza uwezekano wa kutibiwa kwa njia rahisi kama hii,” anasema.
Kwa jumla, upasuaji wa matundu unatoa tumaini jipya kwa wagonjwa, tiba salama, nafuu kwa muda mrefu na inayowawezesha kurejea haraka katika maisha yao ya kawaida.
Ni teknolojia inayobadilisha si tu namna madaktari wanavyofanya kazi, bali pia maisha ya wagonjwa wanaotibiwa.