
Dar es Salaam. Rais wa mpito wa Mali, Kanali Assimi Goita amejiteua kuwa Waziri wa Ulinzi wa taifa hilo, huku akiendelea na majukumu yake ya urais wa kuiongoza nchi hiyo.
Jana, Jumanne Mei 5, 2026 mtandao wa idhaa ya Kiswahili wa DW, uliandika taarifa kuwa hatua Kanali Goita kuchukua jukumu hilo ilitangazwa kupitia televisheni ya taifa ya Mali.
Tangazo la Kanali Goita kuchukua Wizara ya Ulinzi linakuja wakati ambao kuna mvutano unaoongezeka kufuatia kukamatwa kwa baadhi ya wanajeshi, raia wa kawaida na viongozi wa kisiasa wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na makundi ya waasi waliohusika na mashambulizi ya hivi karibuni.
Uamuzi huo unakuja baada ya aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Jenerali Sadio Camara kuuawa Aprili 25, 2026 katika shambulio la kujitoa mhanga lililolenga makazi yake karibu na mji mkuu Bamako.
Mbali na Bamako, mji wa Kati ulikuwa miongoni mwa maeneo kadhaa yaliyoshambuliwa na wanamgambo wa Jama’at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM), kundi lenye mafungamano na mtandao wa Al-Qaeda, pamoja na waasi wa Azawad Liberation Front, kundi la wanaotaka kujitenga.
Mashambulizi hayo yanatajwa kuwa mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja. Wanamgambo hao pia walifanikiwa kuiteka miji muhimu na vituo kadhaa vya kijeshi.
Kwa mujibu wa amri ya Rais iliyosomwa kupitia televisheni ya taifa, Goita ataendelea na majukumu yake ya Urais huku Jenerali Oumar Diarra, aliyewahi kuwa Mkuu wa Majeshi, akiteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ulinzi.
“Rais wa mpito na Mkuu wa nchi, kwa kuzingatia katiba na hati ya mpito iliyorekebishwa, anaamuru yafuatayo: kifungu cha 1: Rais wa mpito, Mkuu wa Nchi, Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi, atatekeleza majukumu ya Waziri wa Ulinzi na masuala ya wastaafu wa Kijeshi.” Limesema tangazo.
Mali imekuwa chini ya utawala wa kijeshi tangu mapinduzi ya mwaka 2020, ambapo Serikali ya kijeshi iliahidi kurejesha usalama katikati ya mashambulizi ya mara kwa mara ya waasi.
Tangu jeshi lichukue madaraka, utawala huo umeigeukia Urusi kama mshirika mkuu wa usalama, hatua iliyosababisha washirika wa kama Ufaransa na ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa (UN) kuondoka nchini humo.