Dar es Salaam. Mwigizaji wa Bongo Movie, Shamsa Ford ni mmoja wa wasanii ambao wamedumu kwenye ndoa zao tangu waamue kuingia katika hali hiyo miaka ya nyuma.
Unajua nini kilichopo nyuma ya mafanikio hayo? Shamsa ambaye alikutana na mwandishi wa safu hii ya Dakika 5 Na… anafichua siri ya maisha yake ya ndoa kuendelea kutamba tangu mwaka 2023 alipoungana na mumewe, Hussen Lugendo ‘Mlilo’.
Mbali na ndoa, pia anafunguka changamoto katika tasnia ya filamu, tabia yake ya utani inayofanya wengi kumwelewa vibaya pamoja na tetesi zilizowahi kuhusishwa naye na wasanii wenzake na msimamo wake juu ya unyanyasaji wa wanawake.
Mwananchi: Kwanza hongera kwa kudumu kwenye ndoa, maana tangu ufunge ndoa na Hussen Lugendo ‘Mlilo’ mwaka 2023, imevunja utabiri wa wengi waliodhani haitadumu. Ni siri gani ya mapenzi yenu hadi leo?
Shamsa Ford: Kwanza kabisa ndoa siyo kitu cha mchezo kama watu wanavyofikiria. Ni uvumilivu, kuelewana na kumuweka Mungu mbele. Watu walizungumza sana mwanzo wakisema haitadumu, lakini sisi tulichagua kutosikiliza kelele za nje na ku-focus na maisha yetu.
Kikubwa ni kuheshimiana na kupeana nafasi. Pia kuwa marafiki kabla ya kuwa mume na mke kumetusaidia sana. Hakuna ndoa isiyo na changamoto, lakini namna unavyozishughulikia ndiyo inayoamua itaendelea au la.
Tunajitahidi kulinda faragha yetu na kutatua mambo yetu ndani bila kuyapeleka kwa watu. Nadhani hiyo ndiyo siri kubwa ya ndoa yetu.”
Mwananchi: Unaonaje mchakato wa utengenezaji wa filamu nchini kwa sasa?
Shamsa Ford: Umeboreshwa sana. Kuna wabunifu wengi na kampuni za uzalishaji zinaanza kuimarika. Bado kuna changamoto za bajeti na usambazaji, lakini ubunifu unakua kila siku.”
Mwananchi: Unajulikana ni mtu wa utani sana, hadi wakati mwingine hata kwenye mambo mazito ya wenzako huwa unaleta utani, hii imekaaje
Shamsa Ford: Ni kweli napenda sana utani, hiyo ni sehemu ya maisha yangu. Nafanya hivyo kupunguza presha au kumfanya mtu ajisikie vizuri. Lakini najua sio kila situation inahitaji utani.
Kuna wakati lazima uwe serious na kumpa mtu nafasi. Nimejifunza kusoma mazingira, kama hali ni nzito, nakuwa mtulivu. Utani sio kubeza matatizo ya watu, bali kuleta faraja, ila lazima uwe na mipaka.”
Mwananchi: Ni changamoto gani kubwa uliokumbana nayo kama msanii wa filamu?
Shamsa Ford: Changamoto kubwa ni bajeti za miradi mikubwa, mtandao wa usambazaji wa kitaalamu na wakati mwingine ukosefu wa rasilimali bora kwenye seti.
Mwananchi: Je, una uzoefu gani wa kufanya kazi na wakurugenzi tofauti na unapendelea mtindo gani wa uongozaji?
Shamsa Ford: Nimefanya kazi na wakurugenzi wengi. Napenda wale wanaotoa mwanga wazi kuhusu maono yao lakini pia wako tayari kusikiliza mapendekezo ya wasanii. Ushirikiano huleta matokeo bora.”
Mwananchi: Unachukua wapi msukumo wa kuboresha uigizaji wako?
Shamsa Ford: Msukumo unatoka kwenye maisha ya kawaida, watu ninaokutana nao, tamthilia za kimataifa na mafunzo ya kitaalamu ninayohudhuria.”
Mwananchi: Una mpango gani wa kitaalamu kwa miaka mitatu ijayo?
Shamsa Ford: Nataka kuongeza ujuzi wa kuigiza, kushiriki filamu za kimataifa na kukuza kampuni yangu ya uzalishaji ili kusaidia vipaji vipya.”
Mwananchi: Unashauri nini kwa wasanii wapya wa filamu wanaotaka kufanikiwa?
Shamsa Ford: Jifunze mambo mengi, kuandika, kuhariri na uzalishaji. Kuwa na nidhamu, tengeneza mtandao wa watu na usikate tamaa hata ukikabiliwa na changamoto.
Mwananchi: Kumekuwa na tetesi kuhusu wewe kukataa kuzungumzia Johari. Kuna ugomvi wowote kati yenu?
Shamsa Ford: Ni kweli niliwahi kukataa kufanya mahojiano kuhusu hilo, lakini si kwa sababu ya ugomvi. Nilihisi si sahihi kuzungumzia mambo hayo hadharani.
Mwananchi: Uliwahi kumtaja Nay wa Mitego kama ex uliyeachana naye vizuri. Una mtazamo gani kuhusu mahusiano ya zamani?
Shamsa Ford: Ni muhimu kudumisha heshima na amani hata baada ya mahusiano kuisha. Hakuna sababu ya kubeba chuki.
Mwananchi: Ujumbe wako kuhusu unyanyasaji wa wanawake?
Shamsa Ford: Unyanyasaji wa aina yoyote haukubaliki. Wanawake wanastahili heshima na usalama na kila mmoja wetu anapaswa kusimama kupinga vitendo hivyo.
Mwananchi: Ujumbe kwa mashabiki wako?
Shamsa Ford: Asanteni kwa kunipenda na kusapoti tasnia ya filamu. Endeleeni kuunga mkono kazi za ndani na kueneza hadithi zetu kwa fahari.