Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameeleza sababu za kumteua ubunge hadi uwaziri Evaline Munisi, akisema ameangalia wasifu wake na kwamba ana sifa za kuingia serikalini.

Uteuzi wa Evaline ambaye ni katibu mkuu wa chama cha NCCR- Mageuzi ulizua mjadala kwa wapo walioutafsiri uteuzi huo kama utekelezaji wa falsafa yake ya 4R na turufu ya kuimarisha mshikamano wa kisiasa nchini.

Lakini wengine wanadai ni mbinu ya kujaribu kuihadaa dunia kwa kuonesha dhamira ya maridhiano, huku wakisisitiza haina tija.

Leo Jumatano, Mei 6, 2026, Ikulu ya Chamwino, Dodoma, Rais Samia amemuapisha Evalini na kutoa sababu za kwa nini amemteua kwenye nafasi hiyo.

Evaline aliteuliwa Mei 2, 2026 kuwa Naibu Waziri-Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), akichukua nafasi ya Rahma Kisuo ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

Katika maelezo yake, Rais Samia alikumbuka maneno ya mwenyekiti wa zamani wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye kwa nyakati tofauti amekuwa akisisitiza Mama Tanzania, tumuhudumie Mama Tanzania, tumpende mama Tanzania.

“Nikasema hiki chama falsafa yao ni kumuhudumia mama Tanzania, nikaona nimvute mmoja kati yao aje tufanye kazi wote. Pengine tunapokea huku mtatusaidia kusema, jamani yaliyoko ni hivi si hivyo mnavyofikiria,” amesema.

“Evaline karibu sana ndani ya Serikali, umeapa kuwa naibu waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), bosi wako huyo hapo. Ndani ya ofisi hii una jukumu la kuhakikisha kazi za Tanzania zinakuwa za staha,’’ amesema.

Samia amemtaka Evaline kuhakikisha haki zinasimamiwa na stahiki za wafanyakazi zinakwenda vizuri katika sekta ya umma na binafsi.

Suala jingine alimtaka Evaline kusimamia ajira za vijana, akieleza kuwa Serikali imeshaanza mchakato wa kutafuta ajira nchi ya nchi.

“Kwa muda mrefu tulikuwa tunapata nafasi hizo, lakini katika wizara yenu kuna mambo yalikuwa hayaridhishi. Lakini mwaka huu, tumeanza kufungua kwa kupeleka vijana zaidi ya 7,000 wasimamiwe haki zao, mawakala na haki zao na Serikali za huko zifuatwe sheria zao, na vijana wetu wazifuate,” amesema.

Kuhusu mahusiano, Rais Samia amesema yamejengeka katika utatu wa Serikali, waajiri na waajiriwa, akimtaka Evaline kuliendeleza.

“Wewe ni hodari kwenye hili, tumefanya kazi pamoja kwenye vyama vya siasa nimeona uwezo wako, kwa hiyo najua utamsaidia bosi waziri wako,” amesema.

Katika sekta ya kazi, Rais Samia amesema jambo kubwa linalopaswa ni kuheshimiana, akisisitiza kila mtumishi anajua jukumu lake na mipaka yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *