Dar es Salaam. Watoaji wa huduma na bidhaa katika migodi ya madini nchini wameanza kuungana ili kuwa na sauti moja ya kutetea maslahi yao na kuongeza ushiriki wa wazawa katika sekta hiyo.

Hatua hiyo imekuja baada ya kampuni nne kusaini makubaliano ya ushirikiano chini ya Umoja wa Makampuni Yanayotoa Huduma na Kusambaza Bidhaa Migodini (MSSPAT), katika hafla iliyofanyika Hoteli ya Rotana jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa umoja huo, Respicus Kandawa, amesema ushirikiano huo ni muhimu kutokana na kuongezeka kwa shughuli za uchimbaji madini nchini, hali inayofungua fursa zaidi za ajira na biashara.

Amesema lengo kuu ni kuhakikisha Watanzania wananufaika ipasavyo na uwepo wa migodi, sambamba na utekelezaji wa sheria ya ‘local content’ inayosisitiza ushiriki wa wazawa katika utoaji wa huduma badala ya kutegemea wageni.

Katibu wa MSSPAT, Benson Samson, akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano (MoU) kati ya umoja huo na kampuni nne kwa ajili ya utoaji wa huduma katika migodi.

“Kipindi cha nyuma niliwahi kufanya kazi mgodini, lakini nilishangaa kuona hata bidhaa zinazopatikana hapa nchini, kama nyama, zikiagizwa kutoka nje. Ilikuwa inaumiza,” amesema Kandawa.

Ameongeza kuwa mabadiliko ya sheria sasa yanatoa nafasi kwa wazawa kushiriki kikamilifu, hivyo kuna haja ya kuunganisha nguvu ili kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa wa vitendo.

Kwa upande wake, Katibu wa MSSPAT, Benson Samson, amesema kuanzishwa kwa ushirikiano huo kunachochewa na utekelezaji wa sheria ya ‘local content’ iliyoanza kuimarishwa mwaka 2025.

Amesema licha ya zaidi ya huduma 20 kutangazwa kutolewa na wazawa, bado baadhi ya sekta zinaendelea kutawaliwa na kampuni za kigeni.

Ametaja baadhi ya huduma hizo kuwa ni mazingira, bima, teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) pamoja na ulinzi.

Akizungumzia sekta ya ulinzi, Mwenyekiti wa Chama cha Ulinzi Binafsi Tanzania, Felix Kagisa, amesema licha ya kuwepo kwa walinzi zaidi ya 300,000 nchini, sekta hiyo bado inanufaisha zaidi kampuni za kigeni.

“Walinzi ni Watanzania, lakini faida inaishia kwa wageni. Sisi tunabaki kufanya kazi kupitia kampuni hizo,” amesema Kagisa.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Chama cha Sekta Binafsi ya Ulinzi, Kara Remtullah, amesema watatoa kipaumbele kwa vijana wa maeneo ya migodi ili wanufaike moja kwa moja na shughuli hizo.

“Tunaiomba Serikali kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria ili huduma hizi zitolewe na kampuni za wazawa, si kupitia mgongo wa kampuni za kigeni,” amesema.

Kwa upande wake, Elly Elikana kutoka Taasisi ya Mazingira ya Green Tech Hag amesema makubaliano hayo yatafungua fursa zaidi kwa wataalamu wa mazingira wazawa kushiriki katika shughuli za migodini.

Ametoa wito kwa taasisi nyingine kushirikiana na umoja huo, huku akiitaka Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha wataalamu wa ndani kunufaika na sekta ya madini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *