KUNA mambo mawili yanayomuhusu mshambuliaji wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa la Ivory Coast, Didier Drogba, katika ziara yake ya siku tatu hapa nchini huku akielezea utayari wake wa kushirikiana na Tanzania katika kukuza sekta ya michezo, hasa soka, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika kwa mara ya kwanza Ukanda wa Afrika Mashariki mwaka 2027.
Drogba, ambaye alikuwa nchini kuanzia Mei 3 hadi 5 mwaka huu, alitoa kauli hiyo baada ya kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan.
Nyota huyo anayetajwa kuwa mmoja wa washambuliaji bora wa Kiafrika kucheza Ligi Kuu England, alisema amefurahishwa na mwaliko alioupata kutoka Serikalini, akieleza kuwa ni fursa adhimu kwake kuchangia maandalizi ya mashindano hayo makubwa barani Afrika.
Rais Samia alimwomba Drogba kuwa balozi wa AFCON 2027, mashindano ambayo kwa mara ya kwanza katika historia yataandaliwa kwa pamoja na nchi tatu za Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda, yakitarajiwa kuanza Juni 19 hadi Julai 17, 2027.
Mazungumzo hayo yalifanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma ambapo pia Drogba alipata fursa ya kuhudhuria uwasilishaji wa bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mei 4, 2026 kufuatia mwaliko huo maalum.
Kwa mujibu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, uzoefu wa Drogba katika soka la kimataifa utakuwa na mchango mkubwa wa kuboresha miundombinu ya michezo na kukuza vipaji vya vijana nchini.
“Tunatarajia kuona mchango wake ukisaidia kujenga mfumo endelevu wa michezo utakaowanufaisha vijana wengi,” ilieleza taarifa ya wizara hiyo.
Drogba, ambaye aliwahi kung’ara akiwa na Chelsea huku akiifungia klabu hiyo jumla ya mabao 164 katika mashindano yote aliyoshiriki, alisisitiza kuwa yupo tayari kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwemo maendeleo ya akademi za soka.
“Ninaheshimiwa kwa mwaliko huu na nina matumaini ya kuchangia maono ya michezo ya Tanzania,” alisema Drogba.
Mbali na kumteua kuwa balozi wa AFCON 2027, Rais Samia aliagiza wizara husika kushirikiana na Drogba katika kubadilishana uzoefu wa uendeshaji wa vituo vya kukuza vipaji (Sports Academies), ikiwa ni hatua ya kuimarisha msingi wa maendeleo ya michezo nchini.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha Tanzania inanufaika si tu kwa kuandaa mashindano, bali pia katika kujenga kizazi kipya cha wanamichezo wenye ushindani wa kimataifa.
Akiendelea kuzungumza, Drogba alieleza kuvutiwa na juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuinua sekta ya michezo, akitaja ongezeko la bajeti ya sekta hiyo kuwa ni ishara ya dhamira ya kweli ya maendeleo.
Alisisitiza kuwa, michezo ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, akieleza kuwa inaweza kuwainua vijana na kuimarisha mshikamano wa jamii.
“Sekta ya michezo ina nafasi kubwa katika kuleta maendeleo ya jamii. Inaweza kuwasaidia vijana na kuijenga jamii imara,” alisema.
Mbali na mchango wake kwa taifa, Drogba alitoa ushauri kwa vijana wanaotamani kuwa wanasoka, akisisitiza umuhimu wa elimu sambamba na vipaji vya michezo.
“Wengi wanataka kuwa wanasoka lakini elimu ndiyo msingi wa kila kitu. Inakusaidia kuwa mtu mwenye maadili, nidhamu na uwezo wa kufanya uamuzi sahihi,” alieleza.
Aliongeza kuwa mafanikio ya kudumu hayatokani na kipaji pekee, bali yanahitaji pia maarifa, maadili na nidhamu ya hali ya juu.
Drogba alisisitiza kuwa sekta ya michezo ina fursa nyingi za ajira kwa watu wengi, si kwa wachezaji pekee bali pia kwa makocha, viongozi wa timu, waendeshaji wa viwanja na wataalamu mbalimbali.
“Si kila mtu atakuwa mchezaji, lakini michezo ina nafasi nyingi sana. Ni sekta inayozalisha ajira na kuchangia uchumi kwa kiwango kikubwa,” alibainisha.