
Unguja. Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zubeir Ali Maulid, amethibitisha kupokea vitabu 12 vya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2024/25.
Katika taarifa iliyotolewa leo Mei 7, 2026, wakati wa mkutano wa Baraza la Wawakilishi, Spika Zubeir amesema uwasilishaji wa ripoti hizo katika Baraza hilo utafanyika baada ya kukamilika kwa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya kila Wizara pamoja na Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa mwaka 2026/27.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kupitia kifungu cha 112(5), inamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwasilisha kwa Rais wa Zanzibar kila taarifa ya ukaguzi atakaoufanya angalau mara moja kwa mwaka, kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 112(3)(c) cha Katiba hiyo.
Ripoti hiyo iliwasilishwa kwa Rais Dk Hussein Mwinyi Aprili 30, 2026 na baada ya kuzipokea taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Rais alimkabidhi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman na kumuagiza aziwasilishe ripoti hizo Barazani.
Kwa mujibu wa maelekezo ya kifungu cha 112 (5) cha Katiba, Waziri Haroun, kabla ya kupita siku saba, bali ni katika siku ya kwanza ya kikao cha kwanza cha Mkutano huu wa tatu wa Baraza.
“Kwa maana jana Jumatano ya tarehe 06 Mei, 2026, Waziri Haroun alinikabidhi ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,” amesema Zubeir
Hata hivyo, hii ni mara ya pili ripoti hizo zinawasilishwa kwa Rais Dk Mwinyi kimyakimyaa bila kualikwa vyombo vya habari kama ilivyofanyika katika ripoti za awali alipoingia madarakani ambazo ziliwekwa wazi wakati wa uwasilishaji wake.
Spika Zubeir amezitaja ripoti hizo ni pamoja na ripoti ya ukaguzi wa kiufundi wa ujenzi wa majengo ya biashara, huduma za jamii na maeneo ya kihistoria kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25.
Ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Serikali Kuu, ripoti ya ukaguzi wa mifumo ya Teknolojia Habari na Mawasiliano (Tehama) katika Taasisi za Umma, ripoti ya ukaguzi wa kiufundi wa ujenzi wa nyumba za Biashara na makaazi nyumba 370 za fidia pamoja na nyumba za gharama nafuu.
Ripoti nyingine ni ya ukaguzi wa kiufundi wa ujenzi wa majengo ya Serikali na ununuzi wa vifaa vya maabara ya ZBS, ripoti ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo, ripoti ya ukaguzi wa kiufundi wa ujenzi wa kiwanda cha mwani pamoja na ujenzi wa viwanda vya uchakataji na usindikaji wa dagaa.
Ripoti ya ukaguzi wa kiufundi wa ujenzi na uimarishaji wa viwanja vya michezo, ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Tawala za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, ripoti ya ukaguzi wa kiufundi wa ujenzi wa vituo vya afya na nyumba za wafanyakazi Unguja na Pemba.
Nyingine ni ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Mashirika ya Umma na Taasisi zinazojitegemea za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ripoti ya ukaguzi wa kiufundi wa ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya bandari na jengo la abiria la Uwanja wa Ndege (AAKIA Terminal 2).
“Hivyo, waheshimiwa wajumbe, napenda kutoa taarifa kwenu kwa wananchi kuwa nimepokea ripoti 12 za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kama ifuatavyo:
“Kanuni ya 103 (7) ya kanuni za kudumu za Baraza la Wawakilishi, Toleo la 2024 inaeleza, bila ya kuathiri masharti ya kanuni ya 27 ya kanuni hizi, majadiliano juu ya makadirio yote yatajadiliwa baada ya kumalizika kipindi cha maswali na kabla ya shughuli nyengine zozote mpaka yatakapomalizika isipokuwa kama itaelekezwa vinginevyo.
“Kwa kuwa ripoti hizo zimewasilishwa katika kipindi cha mkutano huu wa Bajeti ya Serikali, na kwa kufuata masharti ya kanuni ya 103 (7), naomba kuelekeza kuwa, uwasilishwaji wa ripoti hizo katika Baraza hili, utafanyika baada ya Baraza hili kumaliza kushughulikia makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka ya kila Wizara na hatimaye Bajeti ya SMZ kwa mwaka 2026/27,” amesema.
Hata hivyo, ripot ya CAG ya mwaka 2023/24 licha ya kuwasilishwa katika Baraza la 10 bado haijajadiliwa.
Alipoulizwa kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi wa Shughuli za baraza, Othman Ali Haji amesema kwa mujibu wa kanuni za Baraza, ripoti inapowasilishwa barazani kisha inakabidhiwa kwa kamati ya hesabu za Serikali hivyo inapokamilisha kuipitia ndio inapata fursa kujadiliwa barazani.
“Kwa hiyo kwa sasa bado ripoti hiyo inapitiwa na kamati ya PAC, watakapomaliza itajadiliwa na hakuna ripoti amabyo itapitwa bila kujadiliwa,” amesema.