Dodoma. Serikali imetangaza siyo lazima kwa mabasi kupita katika vituo vya mabasi mikoani kama hakuna abiria anayeshuka kwenye kituo hicho.

Aidha utaratibu wa mabasi kupika kwenye mizani kwa sasa hautakuwa lazima kwa mabasi yenye uwezo mdogo wa kubeba abiria au mizigo mikubwa, huku mabasi makubwa yakipewa ahueni ya kupima mizani wanapoanza safari na mizani ya mwisho katika safari.

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema mpango huo unalenga kupunguza gharama na usumbufu kwa wasafirishaji jambo alilosema litapunguza pia wahusika kutokupandisha nauli kiholela.

Dk Mwigulu amesema hayo leo Alhamisi, Mei 7, 2026 wakati akijibu swali la papo kwa hapo bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Viti Maalum, Janeth Mahawanga.

Mbunge huyo amemuuliza Waziri Mkuu, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na changamoto za kimaisha na kuzuia upandaji holela wa nauli ambazo zitaongeza ugumu wa maisha kutokana na changamoto za kidunia ambazo zimepelekea mafuta kupanda bei.

Waziri Mkuu amekiri kuwa, ni kweli kumekuwepo na madhara kwa mataifa mengi kutokana na kupanda kwa bei za mafuta na akasema kuwa kuna mashaka ya kuadimika kwa bidhaa hiyo katika nchi mbalimbali duniani hata siku zijazo.

Katika kutafuta suluhu ya kupunguza kero hizo, Waziri Mkuu amesema wameshakutana na wadau wa vyombo vya usafirishaji ambapo wamekubaliana kupunguza baadhi ya kero na usumbufu uliokuwa ukiongeza gharama bila ulazima.

Amesema mpango huo ni sehemu ya ruzuku ili kuhakikisha kuna kuwa na unafuu wa maisha kutokana na ukweli kuwa bidhaa hiyo ndiyo injini ya uchumi.

“Tumekaa na wadau ili kuhakikisha gharama za usafirishaji hazipandi ambapo baadhi ya gharama tumekubaliana zipunguzwe ili kusiwe na ugumu kwenye usafiri, kwa hiyo tumeona kuwa,hakuna ulazima wa basi kupita kituo cha mabasi kama hayana abiria,” amesema Dk Mwigulu.

Hata hivyo Waziri Mkuu amesema mipango mingi inaendelea kufanyika kwa kushirikisha wadau wa maeneo hayo ili kwanza wananchi waendelee kuwa na unafuu na nishati hiyo iendelee kupatikana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *