Mwanza. Mhariri wa Makala wa Gazeti la Mwananchi, Abeid Othman ameibuka mshindi wa nafasi ya kwanza katika tuzo za Merck Foundation Media Recognition Awards 2025, katika kipengele cha “Diabetes & Hypertension” (Kisukari na Shinikizo la Damu) kwa nchi za Afrika Mashariki.
Othman ametambuliwa kwa mchango wake katika kuandika makala za kuelimisha jamii kuhusu athari na namna ya kujikinga na magonjwa hayo, ambayo ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza yanayowaathiri watu wengi nchini na duniani kwa ujumla.
Katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo iliyofanyika kwa njia ya mtandao leo Alhamisi Mei 7, 2026, mwandishi huyo pia ameongoza waandishi wengine wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kufanya vizuri katika tuzo hizo zinazotolewa kila mwaka na taasisi ya Merck Foundation.
Mhariri wa makala wa gazeti la Mwananchi Abeid Othman
Othman ameshika nafasi ya kwanza katika kundi la uandishi wa magazeti, huku Lucy Bosco, mwandishi wa kujitegemea anayeandika safu ya maisha na kisukari katika gazeti la Mwananchi, akishika nafasi ya pili.
Katika kipengele kingine cha “More Than a Mother” (Zaidi ya Mama) upande wa mtandaoni, mwandishi wa gazeti dada la The Citizen, Julius Maricha, ameshika nafasi ya tatu.
Akizungumzia ushindi huo, Othman amesema: “Kwa muda sasa nimekuwa nikisimamia jarida la afya. Sikutosheka tu kuwa mhariri wa kusoma kazi za waandishi, hasa vijana tunaowaandaa, bali niliona ipo haja ya nami mwenyewe kuandika.”
Ameongeza: “Nimeandika makala nyingi kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, hivyo haikuwa ajabu kwa Merck Foundation kutambua juhudi zangu, hasa ikizingatiwa kuwa hizi ni tuzo zinazotolewa kila mwaka.”