Dar es Salaam. Absa Tanzania mesema changamoto na misukosuko ya uchumi wa dunia zinaweza kuwa fursa muhimu kwa Tanzania kujijengea ushindani wa kiuchumi na biashara katika soko la kimataifa.
Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Mei 7, 2026 jijini Dar es Salaam katika hafla iliyoandaliwa na benki hiyo iliyowakutanisha viongozi waandamizi wa sekta mbalimbali za biashara kwa lengo la kujadili namna biashara za Tanzania, zinavyoweza kubadili sintofahamu ya uchumi wa dunia kuwa fursa za kimkakati.
Mkutano huo uliwaleta pamoja wataalamu wa uchumi wa jumla kutoka Absa Group nchini Afrika Kusini, pamoja na wataalamu wa ndani, ambao walijadili mwenendo wa uchumi wa dunia na kutoa mbinu za kusaidia biashara kukabiliana na changamoto zinazotokana na siasa za kimataifa, mfumuko wa bei, mabadiliko ya tabianchi na kuyumba kwa masoko ya fedha.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho, Mkurugenzi wa Mashirika Makubwa wa Absa Tanzania, Nellyana Mmanyi amesema kutokuwa na uhakika katika uchumi wa dunia sasa si jambo la muda mfupi, bali ni hali ya kudumu inayohitaji biashara kujipanga kimkakati.
Amesema mafanikio ya biashara katika mazingira ya sasa yatategemea uwezo wa taasisi kubadili changamoto kuwa fursa za ushindani.
Mkurugenzi wa Wateja wa Mashirika Makubwa wa Benki ya Absa Tanzania, Nellyana Mmanyi (wa pili kushoto), akizungumza na baadhi ya washiriki wa mkutano huo.
“Misukosuko ya kiuchumi duniani si hali ya mpito tena, bali ni uhalisia wa kudumu. Kwa Tanzania, huu ni wakati wa kuhitaji uongozi wenye taarifa sahihi, wepesi wa kufanya maamuzi ya kimkakati na ushirikiano unaounganisha uzoefu wa kimataifa na utekelezaji wa ndani,” amesema Nellyana.
Katika kikao hicho, timu ya watafiti wa uchumi kutoka Absa Group imewasilisha tathmini ya hali ya uchumi wa dunia na Afrika, ikieleza namna mvutano wa kisiasa duniani unavyoathiri masoko ya nishati, kuongeza mfumuko wa bei, pamoja na changamoto za viwango vya riba na athari zake kwa uhimilivu wa madeni.
Majadiliano hayo pia yamegusia athari za mabadiliko ya tabianchi katika usalama wa chakula na uthabiti wa kijamii, huku ikielezwa kuwa utegemezi mkubwa wa Afrika kwa bidhaa za nje na mazingira ya kifedha ya kimataifa unaongeza shinikizo kwa uchumi wa bara hilo.
Hata hivyo, wataalamu hao wamesema Tanzania inaendelea kuonesha uimara wa kiuchumi kutokana na mazingira tulivu ya sera za fedha, ukuaji mzuri wa pato la taifa ukilinganishwa na nchi nyingine za ukanda huo, pamoja na nafasi yake ya kimkakati katika mabadiliko ya biashara na nishati duniani.
Kwa upande wake Nellyana, amesema Tanzania ina msingi imara wa kiuchumi unaoweza kusaidia nchi kunufaika na mabadiliko ya sasa ya uchumi wa dunia kupitia uwekezaji, biashara na ukuaji wa muda mrefu.
Aidha, wataalamu wa Trade Finance na Global Markets wa Absa wamewasilisha mbinu mbalimbali za kusaidia biashara kujikinga dhidi ya hatari za kiuchumi, ikiwemo suluhisho za mtaji wa biashara, ulinzi wa minyororo ya usambazaji pamoja na matumizi ya mifumo ya kudhibiti hatari za ubadilishaji wa fedha za kigeni, viwango vya riba na masoko ya fedha.
Kwa upande wake, Mchumi Mwandamizi wa Absa Group, Phumelele Mbiyo amesema utekelezaji wa mikakati ndiyo jambo muhimu zaidi katika mazingira ya sasa ya uchumi wa dunia.
Amesema Absa inaendelea kushirikiana na wateja wake si tu kwa kutoa huduma za kifedha, bali pia kwa kuwapatia utaalamu, taarifa na mifumo ya kufanya maamuzi sahihi hata katika mazingira yenye sintofahamu kubwa.
Kupitia kikao hicho, Absa imesisitiza dhamira yake ya ‘Kuiwezesha Afrika ya kesho, pamoja… hatua moja baada ya nyingine,’ ikiwa ni sehemu ya juhudi za benki hiyo kusaidia biashara za Tanzania kupitia tafiti za kiuchumi, utaalamu wa kitaalamu na ushirikiano wa muda mrefu.