
Morogoro. Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Morogoro wameeleza wasiwasi wao kuhusu usalama wa afya kufuatia kuongezeka kwa biashara ya mishkaki na ndizi za kuchoma kando ya barabara ya Barabara ya Morogoro na katika vituo vidogo vya mabasi ya daladala.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti leo Alhamisi Mei 7, 2026, wananchi hao wamesema biashara hiyo ambayo zamani ilikuwa ikifanyika katika maeneo maalumu, sasa imehamia katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu huku baadhi ya mazingira yakitajwa kutokuwa salama kiafya.
Mkazi wa manispaa hiyo, Mariam Salumu amesema zamani maeneo ya kuuzia mishikaki yalikuwa yakifahamika wazi, lakini sasa biashara hiyo imeenea kando ya barabara, sokoni na katika vituo vya daladala.
“Miaka ya zamani wenyeji wa Morogoro na hata wageni walikuwa wanajua maeneo maalumu ya kuuzia mishkaki, lakini sasa biashara hiyo inafanywa pembezoni mwa barabara, sokoni na kwenye vituo vya daladala.
Wakati mwingine utakuta mchoma mishikaki ameweka jiko lake karibu kabisa na mfereji wa maji machafu,” amesema Mariam.
Ameongeza kuwa baadhi ya vifaa vinavyotumika kuchomea mishkaki havina usalama wa kutosha, akieleza kuwa wafanyabiashara wengi hutumia spoku za baiskeli ambazo wakati mwingine huwa na kutu.
“Wapo wachache wanaotumia vijiti, lakini wengi hutumia spoku za baiskeli ambazo zinaweza kuwa hatari kiafya endapo zitakuwa na kutu. Naiomba Manispaa kupitia maofisa afya waendelee kutoa elimu kwa wafanyabiashara hawa ili walinde afya za walaji,” amesema.
Kwa upande wake, Khasim Mfaume amesema pamoja na mazingira ya uchomaji wa mishkaki kutia shaka, pia kuna haja ya kufuatilia ubora wa nyama zinazotumika kutengenezea.
“Bei ya mishikaki kwenye maeneo tuliyozoea ni Sh300 hadi Sh500, lakini hizi zinazouzwa vituoni ni Sh100 tu. Inaleta maswali kuhusu ubora na sijui zinatola wapi,” amesema Mfaume.
Naye Musa Rajabu amesema uwepo wa majiko ya mishkaki karibu na daladala zinazotumia mafuta unaweza kusababisha ajali za moto.
“Kwenye vituo vya daladala utakuta jiko lipo karibu kabisa na tenki la mafuta la gari au moshi wa gari unaelekea kwenye chakula. Hii si salama kiafya na pia ni hatari kwa usalama wa wananchi wanaonunua na kula,” amesema.
Aidha, amesema biashara hiyo inawavutia wanafunzi wengi kukaa vituoni kwa muda mrefu wakinunua mishkaki ya bei nafuu badala ya kurejea nyumbani mapema.
Baadhi ya wafanyabiashara wa mishkaki katika vituo vya daladala wamesema wateja wao wakubwa ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari pamoja na wapiga debe wa vituoni, huku wakisisitiza kuwa mishkaki wanayouza hutokana na nyama halali ya ng’ombe waliochinjwa.
Mmoja wa wafanyabiashara hao katika kituo cha daladala cha mjini kati, Dotto Omary amesema hununua nyama moja kwa moja machinjioni kwa bei nafuu.
“Tunapata nyama machinjioni kwa Sh8,000 kwa kilo tofauti na buchani ambako ni Sh10,000, ndiyo maana tunaweza kuuza mshkaki mmoja kwa Sh100,” amesema Omary.
Kuhusu matumizi ya spoku za baiskeli, amesema wanalazimika kuzitumia kwa kuwa vijiti vya miti vina gharama kubwa na haviwezi kutumika mara nyingi.
“Mishkaki hii inachomwa kwenye moto mkali, hivyo naamini hakuna wadudu wa magonjwa wanaoweza kuhimili moto huu. Weusi unaoonekana kwenye spoku ni moshi wa mkaa, si uchafu,” amesema.
Amekanusha madai kuwa mishkaki hiyo hutokana na nyama zisizo salama au za wanyama wasioliwa.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Morogoro, Kharid Matengo amesema biashara yoyote inayofanyika nje ya maeneo rasmi hutafsiriwa kuwa biashara holela na kwamba, Manispaa inaendelea kuchukua hatua za kudhibiti hali hiyo.
Amesema kupitia Ofisi ya Ofisa Afya, ukaguzi wa maeneo ya biashara unaendelea kufanyika ili kuhakikisha mazingira ya biashara za chakula yanakuwa salama kwa wafanyabiashara na watumiaji.
“Tunazingatia mambo mbalimbali ikiwemo uwepo wa maji safi, choo salama na mazingira yanayokidhi viwango vya afya kwa biashara za chakula,” amesema Matengo.
Ameongeza kuwa Manispaa inaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara pamoja na kuwahamasisha kujiunga katika vikundi ili waweze kupata mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya halmashauri kwa lengo la kuboresha biashara zao.