PENGINE utakuwa ukijiuliza mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake, Stumai Abdallah wa JKT Queens yuko wapi, kwani mara ya mwisho alicheza dhidi ya Yanga Princess, Januari 18 mwaka huu.
Tangu hapo, zimepita takribani mechi sita bila ya uwepo wa Stumai ambaye alikuwa na kiwango bora msimu uliopita.
Taarifa za ndani zinaeleza, mshambuliaji huyo anapitia changamoto za nje ya uwanja zinazomfanya asionyeshe kiwango kizuri mazoezini na hata kwenye mechi.
Hadi sasa, Stumai amefunga bao moja dhidi ya Bilo Queens katika mechi 10 za Ligi Kuu ya Wanawake alizocheza msimu huu, tofauti na msimu uliopita na hadi raundi ya 15 tayari alikuwa amefikisha mabao 23, takwimu zilizomfanya kuwa tishio kwa safu za ulinzi za wapinzani.
Chazno kutoka JKT kilisema nyota huyo anapitia changamoto ambazo hawawezi kuziweka wasi ila akikaa sawa atarejea uwanjani.
“Ni kweli alikuwa hafanyi vizuri tofauti na misimu mitano nyuma, kuna changamoto kidogo yuko nayo, si vyema tukiziweka hadharani lakini tunaamini atakuwa sawa muda si mrefu,” kilisema chanzo kutoka JKT Queens.
Wakati Stumai nje, JKT Queens imekuwa ikiwatumia washambuliaji wawili, Jamila Rajabu ambaye hadi sasa ana mabao saba na Neema Shau.
Mbali na changamoto hiyo, JKT Queens imeanza kujiandaa mapema kama Stumai ataondoka kutokana na ofa zilizopo mezani.
Inaelezwa timu kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Misri zimepeleka ofa JKT Queens ili kupata saini ya mshambuliaji huyo wa timu ya taifa, Twiga Stars.
“Pia kuna ofa anazo, kuna nchi nyingi ikiwemo Misri zinamhitaji na kwa kuwa bado ana mkataba na JKT Queens wanaangalia ofa nzuri itakayomfaa kwa masilahi yake,” kimefichua chanzo.
Kwenye misimu mitano aliyoitumikia JKT Queens, Stumai amekuwa na kiwango bora na msimu wa 2019-2020 alicheza mechi 18 akifunga mabao 22, kisha 2020-2021 alicheza mechi tatu na kufunga mabao saba, huku msimu uliofuata akikaa nje muda mrefu akiuguza jeraha la goti.
Wakati Jentrix Shikangwa wa Simba Queens anachukua kiatu cha dhahabu msimu wa 2022-2023, Stumai alimaliza na mabao 14 kwenye mechi tisa ikiwa siku chache tangu atoke kuuguza majeraha yaliyomfanya aukosa msimu wa nyuma yake.
Msimu uliofuata alicheza mechi 18 na kuweka kambani mabao 19, wastani wa kufunga bao moja kwa kila mechi na msimu jana alikuwa mfungaji bora akiweka kambani mabao 27 kwenye mechi 18.
TAKWIMU ZAKE
2019-2020 – mechi 18, mabao 22
2020-2021 – mechi 3, mabao 7
2021-2022 – hakucheza alikuwa majeruhi
2022-2023 – mechi 9, mabao 14
2023-2024 – mechi 18 mabao 19
2024-2025 – mechi 18 mabao 27
2025-2026 – mechi 10, bao 1