BEKI wa Dodoma Jiji, Abdi Banda amesema kitendo cha kila timu Ligi Kuu Bara kupiga hesabu kali za kumaliza msimu huu ikiwa nafasi nzuri, Kimeongeza ushindani na presha.
Banda amesema presha ya ligi imeongezeka kutokana na umuhimu wa mechi zilizosalia, hali inayofanya kila timu kupambana kwa nguvu kubwa zaidi uwanjani ili kuhakikisha haiangushi pointi.
“Ligi imekuwa ngumu sana kwa sababu kuna timu zinapigania kubaki Ligi Kuu na zingine kuwania ubingwa au nafasi za kushiriki mashindano ya CAF,” amesema Banda.
Akizungumzia maisha yake Dodoma Jiji, beki huyo amesema hali ni nzuri huku na kusisitiza kipaumbele chao kwa sasa ni kumaliza msimu wakiwa katika nafasi salama.
“Maisha ni mazuri, tunaendelea kupambana kuhakikisha tunamaliza msimu vizuri na kuiweka timu kwenye nafasi nzuri, ushindani bado ni mkubwa kuanzia ndani ya timu mpaka nje ila bado tunatumia kila nafasi tunayoipata,” amesema.
Kuhusu hatma yake Dodoma Jiji ambapo mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu, amesema: “Mwanzo wa msimu kweli niliweka wazi mipango yangu ya kurudi nje ya nchi kucheza soka, ila kwa sasa naangalia msimu utaishaje na jinsi ya kupambana timu ibaki kwenye nafasi nzuri, halafu ndipo nitajua hatua inayofuata.”
Banda pia alionyesha imani Dodoma Jiji inaweza kubaki kwenye nafasi nzuri iwapo wataongeza juhudi katika michezo iliyobaki.
“Inawezekana kabisa tukicheza vizuri mechi zetu zilizosalia. Tunaamini na tunaombea iwe hivyo kwani tukishinda mechi zilizobaki tunaweza kujihakikishia nafasi ya kusalia Ligi Kuu msimu ujao,” amesema.
Dodoma Jiji inashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi, ikiwa imecheza mechi 21, ikishinda sita, sare saba na kupoteza nane, ikifikisha pointi 25.