Moshi. Wakaangaji wa kahawa nchini wameiomba Serikali kuhakikisha kahawa inayouzwa katika masoko mbalimbali ya kimataifa inawekwa nembo ya “Made in Tanzania” kwa lengo la kuitangaza zaidi bidhaa hiyo katika soko la dunia.

Wadau hao wametoa ombi hilo leo Mei 8, 2026 wakati wa kongamano la pili la wakaangaji wa kahawa ambalo limefanyika katika ofisini za makao makuu ya Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB).

Akizungumza katika kongamano hilo, Katibu wa wakaangaji wa kahawa nchini, Ombeni Urio amesema uwepo wa nembo hiyo katika vifungashio vya kahawa  itasaidia kuitambulisha zaidi duniani  bidhaa hiyo inayozalishwa kwa wingi hapa nchini.

“Sisi kama wakaangaji wa kahawa tunaomba nembo ya “Made in Tanzania” iwekwe kwenye vifungashio vya kahawa.

“Hii italiongezea Taifa letu umaarufu na kuonyesha fahari yetu kwamba Tanzania tunazalisha kahawa bora yenye ubora wa hali ya juu,”amesema Urio.

Aidha, amesema Tanzania ina kiwango kikubwa cha uzalishaji na usafirishaji wa kahawa nje ya nchi na kwamba kahawa inapopelekwa nje ikiwa na nembo ya “Made in Tanzania”, inalitangaza na kuliheshimisha Taifa letu kimataifa.

Baadhi ya wakaangaji wa kahawa wakiwa katika kongamano la pili kahawa mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro kujadili masuala mbalimbali katika tasnia ya kahawa. Picha na Janeth Joseph

“Watu wakijua bidhaa hii imetengenezwa Tanzania, tunakuwa tunainyanyua nchi yetu na kuitangaza duniani kupitia sekta ya kahawa. Hii inaonyesha kuwa kahawa ya Tanzania ni mali ya kujivunia na ina nafasi kubwa kwenye soko la dunia,”amesema.

Akizungumza  Mwenyekiti wa chama cha kahawa Tanzania (TCA), Olga Shuma amesema sekta hiyo ya kahawa itafika mbali endapo maboresho hayo makubwa yatatekelezwa.

“Nimefurahi kusikia tunao wakaangaji wa kahawa tumefikia  29,  nategema ndani ya miaka mitano ijayo tufike wakangaji 100 na tunaweza tukafika mbali zaidi.Kufika tunaweza kufika huko tunakoelekea na muda ni sasa, sio kesho wala keshokutwa,” amesema Shuma.

Aidha, amewataka wakaangaji hao wa kahawa kuwa na taasisi itakayowasaidia kubeba changamoto zao kwa pamoja ili kupatiwa ufumbuzi.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa nchini (TCB), Primus Kimaryo, amesema wataendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wazalishaji wa kahawa nchini ili kupiga hatua zaidi katika tasnia hiyo.

“Tutajaribu kukaa pamoja kuangalia namna gani tunaingia kwenye kupata fursa katika nchi za jirani na ndani ya nchi kwa sisi ambao ni wakangaji wa kahawa. Tunataka ile ‘Made ni Tanzania’ kuweka chapa kwamba hii bidhaa ni ya Tanzania,”amesema Kimaryo

Amesema”Nyie ndio mnaofanya Watanzania kunywa kahawa ndani ya nchi yao, tunataka kujenga utamaduni wakunywa kahawa ya kwetu na kila mtu akija kunywa kahawa ya kwetu aseme ni kweli amekunywa kahawa ya Tanzania,”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *