Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa salamu za rambirambi kutokana na kifo cha Rais mstaafu wa Botswana, Festus Mogae, akimtaja kuwa kiongozi aliyeacha alama katika kuimarisha utawala bora, uchumi na afya katika Taifa lake.

Mogae aliyekuwa na umri wa miaka 86, amefariki dunia leo, Mei 8, 2026 baada ya kuugua kwa muda mrefu. Taarifa ya kifo chake imetangazwa na Rais wa sasa wa Botswana, Duma Boko.

Kiongozi huyo, aliyetajwa kuwa kinara wa mapambano dhidi ya Ukimwi enzi za uhai wake, aliiongoza Botswana mwaka 1998 hadi 2008. Ni miongoni mwa wakuu wa nchi saba waliowahi kutwaa tuzo ya uongozi bora ya Mo Ibrahim.

Taarifa ya salamu za rambirambi za Rais Samia, imetolewa leo, Ijumaa Mei 8, 2026 na kutiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu.

Katika taarifa hiyo, Rais Samia amesema Mogae alitoa mchango muhimu katika uongozi wa Botswana na Afrika kwa ujumla, hususan katika kuimarisha utawala bora, kusimamia uchumi na kuongoza jitihada za kukabiliana na changamoto za afya ya jamii.

“Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Tanzania, Rais Samia anatoa salamu za pole kwa Rais wa Botswana, Duma Boko, familia ya marehemu, Serikali na wananchi wa Botswana,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa inaeleza Tanzania inaungana na Botswana katika kipindi cha majonzi na inaendelea kuthamini uhusiano wa kindugu na ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo mbili.

Aidha, kupitia taarifa hiyo, Rais Samia ameiombea familia ya Mogae, Serikali na wananchi wa Botswana faraja na nguvu katika kipindi cha majonzi, na kumuomba Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu mahali pema peponi.

Huyu ndiye Mogae

Kabla ya kuukwaa wadhifa wa urais mwaka 1998, Mogae aliwahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Botswana na baadaye kuwa Waziri wa Fedha.

Kitaaluma ni mchumi, lakini miongoni mwa sifa zake zinazoendelea kusikika hata alipoondoka madarakani ni uwezo wake wa kuimarisha uchumi, siasa za utulivu na kiongozi aliyesisitiza uwajibikaji.

Mwaka 2008 alitunukiwa tuzo ya mafanikio katika uongozi ya Mo Ibrahim kutokana na uongozi wake uliotajwa kuwa wa mfano katika bara la Afrika.

Hii inamfanya kuwa mmoja wa viongozi saba Afrika waliowahi kutwaa tuzo hiyo, ambayo kwa mara ya mwisho ilitolewa mwaka 2020.

Wengine waliowahi kupata tuzo hiyo ni Joaquim Chissano wa  Msumbiji mwaka 2007, Nelson Mandela wa Afrika Kusini (2007), Pedro Pires wa Cape Verde (2011), Hifikepunye Pohamba wa Namibia (2014), Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia (2017) na Mahamadou Issoufou wa Niger (2020).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *