Unguja. Wakati Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais (OMKR) ikianisha vipaumbele vitano vya kutekeleza mwaka 2026/27 na kuomba kuidhinishiwa Sh35.558 bilioni, ufinyu na upatikanaji wa fedha usioendana na mahitaji umeendelea kuitesa wizara hiyo.

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/27 Barazani leo Mei 8, 2026, Kaimu Waziri wa OMKR, Hamza Hassan Juma amesema wizara inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo bajeti isiyoendana na mahitaji ya utekelezaji wa majukumu ya OMKR.

Ufinyu huo pia unachangia upungufu wa vifaa na vyombo vya usafiri katika wizara hiyo yenye taasisi nne ambazo ni watu wenye ulemavu, Tume ya Ukimwi, Mamlaka ya Kudhibiti na Kuzuia Dawa za Kulevya pamoja na Mazingira.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2025/26, OMKR iliidhinishiwa Sh27.182 bilioni, ambapo kati ya fedha hizo Sh6.941 bilioni ni mishahara, Sh5.883 bilioni matumizi mengineyo, Sh12.413 bilioni miradi ya maendeleo na ruzuku ya Sh1.944 bilioni.

Amesema hadi kufikia Machi 2026, jumla ya Sh9.283 bilioni sawa na asilimia 40 ndizo zilizopatikana kwa kazi za kawaida na Sh5.155 bilioni sawa na asilimia 97 kwa mishahara.

“Sh2 bilioni sawa na asilimia 45 kwa matumizi mengineyo na Sh761.939 milioni kwa ajili ya matumizi ya ruzuku sawa na asilimia 49 ndizo fedha zilizopatikana,” amesema.

Kwa upande wa kazi za maendeleo, Waziri Hamza amesema kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026 jumla ya Sh1.317 bilioni sawa na asilimia 11 zilipatikana kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Waziri Hamza amesema ili ofisi iweze kutekeleza programu zake kwa ufanisi katika mwaka wa fedha 2026/27, ameliomba Baraza kuidhinisha Sh35.558 bilioni.

Kati ya fedha hizo, Sh17.529 bilioni ni kwa matumizi ya kawaida, zikiwamo Sh7.453 bilioni kwa mishahara, Sh8.223 bilioni kwa matumizi mengineyo na ruzuku ya Sh1.906 bilioni.

Katika hatua nyingine, Waziri Hamza ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema, “Ongezeko la uzalishaji wa taka ni changamoto nyingine ambapo kwa siku umefikia tani 654 wakati uwezo wa manispaa zetu si zaidi ya asilimia 50, jambo ambalo linaendelea kuharibu mandhari ya nchi yetu.”

Vipaumbele

Waziri Hamza amesema vipaumbele ambavyo wizara imejiwekea katika mwaka huu wa fedha ni kuendelea na juhudi za uhifadhi wa mazingira nchini kupitia upandaji miti, matumizi ya nishati salama, utoaji wa elimu ya mazingira, doria pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kunusuru maeneo yanayoingia maji ya Bahari.

Kipaumbele kingine kilichoanishwa ni ujenzi wa miundombinu himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha harakati za kijamii na kiuchumi katika baadhi ya maeneo yaliyoathirika.

Kwa mujibu wa waziri huyo, jumla ya maeneo 148 yamebainika kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Pia, kujenga uelewa kwa jamii na wataalamu kuhusu masuala ya biashara ya kaboni na kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kuboresha ukaguzi, uchunguzi pamoja na utoaji wa huduma za tiba na marekebisho ya tabia kwa waathirika wa dawa za kulevya ni miongoni mwa vipaumbele vilivyowekwa.

“Kuendelea kutoa haki na fursa sawa kwa maendeleo jumuishi ya watu wenye ulemavu nchini kwa kuimarisha huduma za tiba, elimu na makazi na kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi kwa lengo la kufikia azimio la kumaliza Ukimwi ifikapo 2030,” amesema Hamza.

Ametaja malengo ya wizara kuwa ni kuimarisha usimamizi na uhifadhi wa mazingira pamoja na jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa maendeleo endelevu Zanzibar, pamoja na kuimarisha usimamizi na upatikanaji wa haki na fursa sawa kwa watu wenye ulemavu katika nyanja zote za kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Amesema pia wizara inalenga kuimarisha udhibiti na mapambano dhidi ya uingizaji, usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya, hatua itakayokwenda sambamba na mikakati madhubuti ya tiba na marekebisho ya tabia.

Aidha, amesema wizara itaendelea kuratibu mwitikio wa Taifa dhidi ya Ukimwi nchini kwa kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu kwa makundi maalumu, vifaa tiba na dawa za kufubaza VVU.

Akisoma maoni ya Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Machano Othman Said amesema kamati inaitaka Serikali kuhakikisha sera na mipango inatekelezwa kwa lengo la kudhibiti Ukimwi.

Pia, amesema kamati imeisisitiza Serikali kuhusu umuhimu wa kinga, uboreshaji wa huduma za afya na kuondoa unyanyapaa kwa wanaoishi na VVU ili kulinda utu na haki zao.

“Serikali itafute ufadhili wa mazingira na kupanua dhana ya uwezeshaji na ushirikiano na mashirika ya kimataifa ili kuongeza ufanisi katika uhifadhi wa mazingira,” amesema.

Amesema pia kamati imeona ipo haja ya Wazanzibari kushiriki mikutano ya kimazingira kama nyenzo endelevu itakayowezesha kukabiliana vyema na changamoto za mazingira.

“Kamati imeona ipo haja ya kuweka sheria mpya ya kuwabana wafanyabiashara wanaoendelea kutumia mifuko ya plastiki na kuongeza faini kwa watu wote watakaotumia mifuko hiyo, ili kulinda mazingira, hatua itakayosaidia kuwa na jamii yenye uwajibikaji kwa mazingira,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *