KOCHA Abdihamid Moalin ametoa kauli inayoonesha ana kazi ya kufanya Yanga baada ya kuchukua mikoba siku chache tangu kuondolewa kwa Pedro Goncalves.
Moalin akishirikiana na Patrick Mabedi, wamekabidhiwa kikosi cha Yanga kukiongoza hadi mwisho wa msimu huu baada ya klabu hiyo Mei 6, 2026 kutangaza kumtimua Pedro.
Moalin aliiongoza Yanga kuifunga Coastal Union mabao 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Mei 9, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar, ikiwa ni ya kwanza tangu apewe majukumu hayo na kuifanya timu hiyo kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo ikifikisha pointi 54.
Kocha huyo alizungumzia kiwango cha timu kwa jumla kipo vizuri, ingawa kuna maeneo yanahitaji maboresho hasa wastani wa kutumia nafasi za kufunga.
“Eneo ambalo tunahitaji kulifanyia kazi zaidi ni matumizi ya nafasi tunazozipata. Kuna wakati tunatengeneza nafasi nyingi lakini tunashindwa kuzitumia vizuri na hilo ni jambo ambalo tunapaswa kuliboresha,” amesema Moalin aliyerejea kikosini hapo awali kama msaidizi wa Pedro.
Kabla ya hapo, Moalin alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga wakati wa Kocha Sead Ramovic msimu wa 2024-2025, kisha akakaimu nafasi ya ukocha mkuu alipoondoka Mjerumani huyo, kisha akawa msaidizi wa Miloud Hamdi na kufanikiwa kubeba Kombe la Muungano 2025, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB.
Licha ya Moalin kutoa kauli hiyo, lakini Yanga inaendelea kushikilia rekodi ya kuwa timu yenye mabao mengi Ligi Kuu Bara msimu huu ikifunga 50, inayofuatia Simba yenye 35 kabla haijacheza na Tanzania Prisons. Toafuti ni mabao 15.
Msimu uliopita 2024-2025 ambao Yanga ilitwaa ubingwa wa ligi hiyo, ilifunga mabao 83, huku 2023-2024 yakiwa 71. Ili kufikia rekodi ya msimu uliopita, Yanga katika mechi nane zilizobaki inapaswa kufunga mabao 33 ikiwa ni wastani wa mabao manne kwa mechi.
TATIZO WASHAMBULIAJI
Kutokana na kile kilichozungumzwa na Moalin, imebainika tatizo lipo kwa washambuliaji na wamekuwa wakikosa utulivu mbele ya goli, huku ishu ya mfumo nayo ikigusiwa.
Nyota wa zamani wa Mbeya Kwanza, Boniface Nyagawa, amesema tatizo kubwa lililopo Yanga sio uwezo wa kutengeneza nafasi bali ni washambuliaji kushindwa kuwa watulivu wanapofika eneo la mwisho.
“Yanga wanacheza vizuri sana na wanatengeneza nafasi nyingi kila mchezo lakini washambuliaji wanahitaji utulivu zaidi mbele ya lango. Kuna wakati wanaonekana kuwa na haraka au presha ya kufunga ndiyo maana wanapoteza nafasi ambazo zilipaswa kuwa mabao,” amesema Nyagawa.
Kwa upande wake mshambuliaji wa zamani wa Stand United na Mbeya City, Abasarim Chidiebere, amesema.
“Tatizo si kutengeneza nafasi kwa sababu Yanga wanafanya hivyo vizuri sana, shida ipo kwenye umaliziaji. Wakati mwingine washambuliaji wanataka kufanya vitu vigumu badala ya kutumia nafasi kwa urahisi na hilo linawagharimu,” amesema Chidiebere.